Serikali imlete Ballali mahakamani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version

YUKO wapi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali ambaye serikali iliahidi taifa na wahisani kwamba "akihitajika atapatikana?"

Ballali ametajwa mahakamani kuwa alishiriki kupitisha baadhi ya malipo katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Mpaka sasa kiasi cha fedha kilichogunduliwa na wakaguzi kuwa kilikwapuliwa Sh. 133 bilioni.

Akizungumza na waandishi wa habari, 8 Mei 2008 ikulu mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema serikali haimtafuti Gavana Ballali na kwamba “kama ingemtafuta isingeshindwa kumpata.”

Rweyemamu alisema, “Kwanza (Ballali) ni private citizen (raia kama wengine), siyo mwajiriwa tena wa serikali. Anaweza kuishi popote. Lakini akihitajika, atapatikana… Dk. Ballali ana nyumba nchini Marekani. Yupo huko anaishi na familia yake.”

Maelezo ya Rweyemamu yalikuwa yakilenga kujibu kile kilichoitwa, “Kelele za wananchi, vyombo vya habari, nchi wahisani na asasi za kiraia,” waliokuwa wanataka serikali kutoa tamko mahali aliko Ballali na hatua zitakazochukuliwa baada ya kumfuta kazi.

Katika hilo, Salva alisema, “Serikali ina mkono mrefu ambapo ingekuwa inamtafuta Ballali, ingeweza kuutumia kumpata. Haijafanya hivyo kwa sababu haimhitaji. Ikimhitaji itampata.”

Miezi 11 imepita tangu Rweyemamu ahakikishie taifa na ulimwengu kuwa “Ballali akihitajika atapatikana.”

Leo baadhi ya wafanyakazi wa BoT, wakiwamo watuhumiwa wa wizi katika akaunti ya EPA na hata mashahidi wa upande wa serikali, wamemtaja Ballali kuwa ndiye aliyekuwa anapitisha malipo.

Mkuu wa Kitengo cha Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT, Iman Mwakosya ambaye ni mmoja wa washitakiwa na Mkurugenzi wa Mipango Mkakati wa BoT, Peter Noni, ambaye ni shahidi wa upande wa mashitaka, wamenukuliwa kwa nyakati tofauti wakidai Ballali ndiye aliingiza benki katika mgogoro.

Kwa upande wake, Mwakosya anasema aliagizwa na Ballali kushughulikia malipo ya Rajabu Maranda, Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kigoma. Maranda ni miongoni mwa watuhumiwa wa ukwapuaji katika EPA.

Naye Noni anasema, Ballali ndiye aliyekuwa anaidhinisha malipo, anapitisha nyaraka na ndiye aliyefanya utambuzi wa wote waliodaiwa “kuidai serikali.”

Noni hatafuni maneno. Anasema kuwa ndani ya BoT hakukuwa na utaratibu wa malipo ya EPA bali “malipo yote yalikuwa yanapitia kwa Gavana Ballali.”

Kutokana na mazingira hayo, ni muhimu Ballali apatikane na kuja kusaidia pale penye giza. Umuhimu wa Ballali kwa sasa ni mkubwa pengine hata kuliko wakati ule Rweyemamu alipokuwa anatoa kauli yake.

Kwanza, ni muhimu kwa sababu tayari imefahamika kuwa Ballali wakati wote alipokuwa BoT, hakujihangaisha kutaka kufahamu uhalali wa nyaraka zilizowasilishwa ofisini kwake na walioitwa “wadai wa serikali.”

Ni uzembe huu uliofanywa na gavana uliosababisha kuingiza hasara serikalini, kushusha hadhi ya BoT machoni mwa jumuiya ya kimataifa na nchi wahisani na kuporomosha uchumi wa taifa.

Pili, Ballali hakuuliza sababu iliyowafanya watendaji wake kugomea kuidhinisha baadhi ya nyaraka, jambo ambalo lilimlazimisha yeye mwenyewe kuingilia kati na kufanya kazi hiyo.

Hapa Ballali alikuwa ameshindwa kuheshimu mgawanyo wa madarakana. Matokeo yake serikali imepata hasara kwa mambo ambayo yangeweza kuepukika.

Tatu, chini ya uongozi wake, Ballali aliendesha BoT kama shamba la bibi; ule utaratibu wa uwekekaji fedha na utunzaji ulikuwa haufuatwi.

Kupatikana kwa Ballali kutaondoa minong’ono kutoka kwa wananchi kuwa nyuma ya Ballali walikuwamo viongozi wakubwa, akiwamo rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa.

Bila shaka Rweyemamu alikuwa anazungumza kwa niaba ya serikali. Kwa hiyo aliweka ahadi ya serikali ya kumpata Ballali pale atakapohitajika.

Sasa Ballali anahitajika leo. Aletwe kusaidia katika kesi zilizoko mahakamani. Ajibu tuhuma zinazotolewa na wafanyakazi waliokuwa chini yake. Bila shaka serikali inakumbuka ahadi yake kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.

Ballali huyu bila shaka atakuwa na mengi. Ni Salva mwenye kuweza kukidhi matakwa ya Watanzania na mahakama kwa kumleta.

Yako wapi mahojiano ya Kamati Teule ya Rais Jakaya Kikwete ambayo walifanya na Ballali? Je, inawezekana hawakumhoji kwa kuwa ikulu iliwahakikishia kuwa akihitajika atapatikana?

Ushahidi wa Ballali katika kesi za EPA ni muhimu kwani utasaidia mahakama kupata ukweli wa suala zima la EPA.

Napendekeza mahakama iitake serikali imtafute Ballali kama ilivyoahidi ili mzigo wa ushahidi uweze kuwa mwepesi na mahakama ipate msaada wa kufikia uamuzi haraka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: