Serikali ina kasumba na makocha wa kigeni


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version

KASUMBA mbaya. Majibu ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Vijana, Dk. Fenella Mkangara yameendeleza kasumba ya viongozi wetu kuthamini makocha wa kigeni ambao hawatusaidii na kudharau wazalendo licha ya kuonyesha mafanikio.

Kauli yake bungeni, kwamba serikali inatafuta kocha wa kigeni kwa ajili ya kuinoa timu ya vijana chini ya miaka 23 inayonolewa sasa na Jamhuri Kihwelu imezua hofu, manung’uniko, na shutuma.

Dk. Mkangara amekuwa mmoja wa viongozi hodari kupanda jukwaani na kutoa wito Watanzania wanunue bidhaa za Kitanzania na serikali itumie wataalam wa Kitanzania, lakini linapofika suala la michezo, hasa soka macho na roho zao wanaelekeza kwa makocha wa kigeni.

Mafanikio

Rekodi zilizopo zinaonyesha makocha wazalendo ndio wana mafanikio ya kutolea mfano kuliko wa kigeni. Marijan Shaaban, Paul West Gwivaha, Syllersaid Mziray (wote marehemu) ni miongoni mwa wazalendo wenye mafanikio ya kushikika.

Mwaka 1974 timu  ya Tanzania Bara ambayo baadaye ilibatizwa jina la Kilimanjaro Stars ikiwa chini ya kocha mzalendo Marjani ilitwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa Kombe la Challenge mashindano yaliyofanyika nchini.

Shaaban alipata urahisi wa kukusanya wachezaji nyota wa klabu zote mashuhuri nchini hasa Yanga na Simba iliyotwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki chini ya Gwivaha.

Mwaka huo, Simba ilifanikiwa kutinga nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika ambako ilitolewa kwa mikwaju ya penalti na Mehla el Kubra ya Misri.

Pamoja na uwezo ulioonyeshwa na wazalendo hao, mara viongozi wa serikali wakaugua ugonjwa mbaya wa kuhusudu makocha wa kigeni. Akaletwa nchini  Ruud Guttenhoff wa Ujerumani, Vladmir Wolk wa Poland, Jeff Hudson wa Uingereza na wengineo.

Kati ya hao ni Mpoland Wolk aliyeipeleka Taifa Stars, kwa mara ya kwanza, katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kazi nzito iliyofanywa na Gwivaha na Joel Bendera. Huko iliishia hatua ya makundi.

Taifa Stars, Kilimanjaro Stars na hata timu za vijana hazikuonekana tena. Kilimanjaro Stars iliibuka mwaka 1994 ilipotwaa Kombe la Challenge, chini ya Syllersaid Mziray, akishirikiana na Sunday Kayuni.

Katika kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1996 nchini Afrika Kusini, Sunday Kayuni na Mzee Kheri waliiweka Taifa Stars katika nafasi nzuri ya matumaini, lakini presha kutoka serikalini iliwaengua akaajiriwa mpitanjia Clovis de Oliviera wa Brazil.

Mbrazil huyo alitokea Uarabuni alikovurunda, lakini alipigiwa debe akapewa timu hiyo. Matokeo yake kila mmoja alijilaumu kwa nini walimwita kocha huyo.

Makocha wengine Victor Stanculescu wa Romania aliyechukua baadaye uraia wa Marekani, Ray Whelan kutoka kampuni ya Bob Charlton wa Uingereza, na Bukhard Pape wa Ujerumani, walivuna mapesa na kuondoka kurudi kwao bila kuipa ushindi wowote Taifa Stars wala Kilimanjaro Stars.

Mwaka 2001, Mziray na mzalendo mwenzake Boniface Mkwassa walifanikisha Stars kutwaa Kombe la Castle huku Pape akiwa mkurugenzi wa ufundi.

Kile kinachoweza kuitwa mafanikio ya makocha wa kigeni ni mwaka 2009 Marcio Maximo wa Brazil alipoipeleka Stars katika fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wasio profeshnoo zilizofanyika Ivory Coast. Halafu mrithi wake, Jan Borge Poulsen wa Denmark alianza kwa kuiwezesha Kilimanjaro Stars kutwaa Kombe la Challenge Desemba 2010.

Matokeo ya sasa ya michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zimemweka Poulsen katika nafasi ngumu ya kufuzu kwa fainali za mwaka ujao.

Poulsen na wenzake hupewa mikataba bora, hulipwa mishahara minono, hupewa nyumba na gari na hupewa vifaa kadri programu yake inavyotaka, lakini kazi bure. Wazalendo wote mikataba yao ni ‘kauli mali’, hawapewi mshahara wa kueleweka, hawapewi nyumba wala gari kama ilivyo sasa kwa Julio ambaye amejenga matumaini ya kuipeleka timu yake ya vijana chini ya miaka 23 katika Michezo ya Olimpiki.

Katika hatua za awali za michuano ya kimataifa, licha ya  Julio kutokuwa na mkataba wala mshahara wa maana, amejitahidi kuwatoa kimasomaso Watanzania alipowatoa ‘vijana vijeba’ wa Cameroun kwa penalti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Cameroun ilishinda 2-1 kwao na Tanzania ikashinda 2-1 nchini na ndipo ikapigwa mikwaju ya penalti.

Vijana wa Julio wakapata tiketi ya kucheza na Nigeria ambao walinyukwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Julio ana historia ya kuwa na uchungu na nchi yake. Alipoona timu ya taifa inatajwa na jina lake linaachwa kila mara, alijipeleka mwenyewe kwenye mazoezi ya Stars, na akafanikiwa kupata namba ya kudumu.

Kwa hatua aliyofikia, serikali haikupaswa kumpa Julio salamu zisizotambua juhudi zake kwa  kusema inatafuta kocha mpya wa kigeni kwa ajili ya kunoa timu hiyo.

Hivi kuna ubaya gani serikali kuwa na programu ya kuendeleza makocha wake? Kwanini haikusubiri walau Julio akwame ndipo serikali itoe kauli hiyo? Makocha wa kigeni waliopewa timu hiyo, wameipa mafanikio gani hadi sasa?

Makocha wazalendo wana uchungu, uwezo mkubwa wakipewa kila aina ya msaada, huduma, mshahara mzuri na vifaa kama kwa makocha wa kigeni.

0789 383 979
0
No votes yet