Serikali ina ndoa na wakristo?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MAKALA iliyosema “Kikwete amepasua jipu la udini” katika safu ya “Tuseme Kweli” wiki iliyopita imeibua hisia kali. Wasomaji saba kati ya 123 waliotuma meseji zao hawakunipongeza.

Mmoja ameniita mzushi, mwingine amedai inachochea fujo, mwingine amedai nimeathiriwa na mfumo kristo huku meseji tatu zinatuhumu.

Msomaji mwenye simu Na 0767446064 amedai: Ninyi Mwanahalisi ni CHADEMA na makala yako ni mfumo kristo. Hamuwezi kuchukua nchi hii.

Mwenye Na 0779000950 amehoji: Nimesoma makala yako, naomba kuelimishwa waislamu walikuwa na shule au vyuo ambavyo vilitaifishwa hadi wadai warudishiwe? Kama vipo nitajie tafadhali.

Aidha mwenye Na 0712706454 anasema: Bwana Joster, makala uliyotoa ni tungo tata, inalenga kuchochea fujo. Watakusifu wengine ila kwa kweli haijatulia. Mchana mwema.

Vilevile mwenye Na 0713324300 anasema: Toka uhuru Tanzania imeongozwa na marais wanne; wawili wakristo na wawili waislamu. Kwa uzoefu wangu wakati wa marais wakristo, waislamu waliwashambulia sana na enzi za marais wailsmu, wakristo walishambulia mno. Je, mnataka tuwe na marais wapagani? Acheni uchochezi wenu!

Meseji kutoka simu Na 0787282385 ilisema: Unajifanya ni mtetezi wa waislamu kumbe ni mnafiki. Kwa nini unataja shule zilizojengwa na wakristo tu bila kutaja za waislamu? Unadhani waislamu tumelala hatujengi? Na hivyo vyuo walivyonavyo wakristo hujui vinatokana na msaada wa itifaki makubaliano (MOU) kati ya serikali na wakristo. Unadhani bila mkataba huu wangepata fedha? Acheni udini wenu huo!

Kutoka simu Na 0776749972 meseji ilisomeka: Katika makala yako, mbona umesahau kutaja mabilioni ya fedha wanayopewa waislamu kwa makubaliano maalum (MOU) ili wajenge vyuo vikuu vingi kama wakristo lakini hawajengi?

Wazo kutoka simu Na 0713888112 ilisema: Habari Joster. Katika MwanaHALISI umesema “…Jambo moja la msingi ni kwamba wakristo hawakutaka kuganda kwenye shule za zamani tu, wamejenga mpya na wamefungua vyuo vikuu vingi na hospitali. Taasisi na dini nyingine ziige”. Kitu usichokijua ni kwamba wakristo wanachotewa fedha zetu kwa makubaliano na serikali. Waislamu watoe wapi fedha au waibe? Nijibu haraka.

Nawapongeza wasomaji wote wa makala hizi mbili lakini nikiri wazi si rahisi kuwajibu wote walionitumia maoni yao, na wale waliopiga simu. Hili ni jambo la kawaida kwa kazi hii, huwezi kumridhisha kila mtu.

Maelezo yaliyomo katika meseji hizi ni tata. Wakati mbili zinadai kuna makubaliano mahsusi kati ya wakristo na serikali yao, moja inatuhumu waislamu kutumia vibaya mamilioni ya fedha wanayopewa na serikali.

Meseji kutoka simu Na 0787282385 na Na 0713888112 zinaeleza kuwepo makubaliano kati ya serikali na wakristo, kwamba serikali imewapa wakristo mamilioni ya shilingi kujenga shule na vyuo, wakati meseji Na 0776749972 inatuhumu waislamu kutafuna mamilioni ya shilingi wanayopewa na serikali kujengea shule na vyuo.

Meseji tatu hizi zituongoze sote kufika mahali pazuri. bali, hayo ni ya kweli?

Kama ni kweli serikali imekubaliana na wakristo kuna ubaya gani mkristo kusema waislamu wanaonewa kwa suala la shule?

Kama kweli hilo lipo, serikali haioni inapendelea waumini wa dini moja? Na hilo linatosha kuitwa ni uvunjaji wa katiba ya nchi. Serikali ijitazame kwa haya.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 2.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: