Serikali inachezea roho za watu wake


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka madaktari waliogoma kote nchini kurejea kazini mara moja. Amesema watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo , watakuwa wamejifuta kazi. Hii ni amri.

Wala haikutarajiwa waziri mkuu Pinda angeamuru hivyo. Ilitarajiwa angekutana na madaktari; kuwasikiliza na kisha kutafuta suluhu ya matatizo yao .

Lakini haikuwa hivyo. Badala ya serikali kukutana na madaktari na kujibu hoja zao, imeamua kutumia vitisho.

Chanzo cha mgogoro huu ni madaktari kudai haki yao ya kulipwa posho za kujikimu.

Hili lilijibiwa kwa ukali kwa serikali kuamuru kuhamishwa kwa mkupuo “madaktari wote wanafunzi” na kuwasambaza katika hospitali nyingine jijini Dar es Salaam .

Uamuzi huo uliotangazwa na Lucy Nkya, naibu waziri wa afya, tarehe 16 Januari 2012, ndio uliochochea utambi katika mgogoro unaofukuta.

Hapo ndipo kiliamka Chama cha Madaktari Tanzania  (MAT) na kutangaza kuungana na wanataaluma wenzao katika mgomo.

Kabla ya kutaka kuonana na Pinda, madaktari waliwasilisha kilio chao kwa waziri wa afya, Dk. Haji Mponda, naibu wake Nkya, katibu wake mkuu, Blandina Nyoni na mganga mkuu wa serikali, Dk. Deo Mtasiwa.

Majibu waliyopewa yalikuwa ahadi tupu kama siku zote – kuboresha maslahi, ikiwamo posho ya kulala kazini, kufanya kazi katika mazingira hatarishi, vifaa, tiba na kuwapo wataalamu wa kutosha katika hospitali za umma.

Lakini madaktari wanataka serikali iboreshe huduma za afya na kuondokana na tabia ya kutumia mamilioni ya shilingi kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Hakuna aliyewasilikiza.

Wakaamua kuja na madai mapya, likiwamo la kuitaka serikali kuwaachisha kazi mara moja viongozi wa wizara kwa kushindwa kuwalipa kile walichostahili kwa wakati na hivyo kusababisha mgogoro na mgomo.

Ilitarajiwa hatua ya kwanza ya waziri mkuu ingekuwa kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuwafuta kazi waziri, naibu wake na katibu mkuu, kwa kushindwa kuchukua hatua ya kujadiliana na wawakilishi wa madaktari mara harufu ya mgomo ilipoanza kusikika.

Ilitarajiwa pia, waziri mkuu Pinda atangaze kuwa tayari kukutana na wawakilishi wa madaktari Jumatatu au kuwataka wamfuate Dodoma kwenye vikao vya Bunge, huku akiomba wengine kuendelea kutoa huduma.

Baada ya kikao chake na wawakilishi wa wafanyakazi wote angetoa taarifa ya majadiliano, badala ya hatua za kibabe alizochukua bila hata kukutana nao.

Lakini hili la kuamuru kwamba siku ya Jumatatu madaktari wote lazima warudi kazini na atakayeshindwa kufanya hivyo basi amepoteza kazi, linadhihirisha ubabe wa kutumia nyundo kuua sisimizi.

Hatua hii inazima fikra za suluhu na kuonyesha kuwa matatizo ya madaktari hayawezi kupatiwa ufumbuzi na serikali hii.

Kuamuru madaktari kurejea kazini kwa mabavu, hakuwezi kujenga morari wa kazi. Kwa nje kunaweza kuonekana tatizo limekwisha, lakini kumbe tatizo liko pale pale, au pengine limekuwa kubwa zaidi.

Madaktari wanaweza kwenda kazini, lakini wakaendelea kufikiria namna ya kufanya kazi zao za nje ili waweza kuishi au kuboresha vipato vyao.

Wanaweza kwenda kazini na kusaini mahudhurio, lakini wakagoma kufanya kazi. Wanaweza kuingia ofisini lakini wakakataa kutoa huduma inavyostahili. Je, serikali imejiruhusu katika hilo ?

Tatizo hili la madaktari kwa karibu wiki mbili sasa limekuwa katika mjadala nchini baada ya kufikia hatua ya mgomo. Lilianzia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye kusambaa nchini kote.

Mgomo ulianzia na madaktari 194 walioko katika mafunzo ya vitendo. Waliamua kuweka kando kauli mbinu yao ya muda mrefu ya “udaktari ni wito.”

Wakaweka chini zana zao za kazi, hasa baada ya juhudi za kudai posho na stahili nyingine kucheleweshwa na kushindwa kulipwa.

Lakini kutokana na utovu wa umakini katika kutatua mgogoro huo, madai yao ambayo yalipuuzwa au kucheleweshwa, yameibua mengine. Sasa wanataka madakari wote nchini kupatiwa makazi karibu na wanakofanyia kazi.

Wanadai, pamoja na mengine, kusitishwa kwa rufaa za wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi wakati wao wana uwezo wa kuwahudumia hapa nchini.

Katika kujaribu kuwatuliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia amesema serikali inarekebisha waraka kuhusu nani anastahili kupata nyumba na yupi hastahili.

Alisema tayari fedha kutoka Global Fund zimepatikana kwa ajili ya kujenga nyumba 10 kila wilaya; nyumba hizo zitajengwa kwenye wilaya 18 zilizopo pembezoni.

Lakini kuhusu suala la mishahara na posho, wakati Ghasia anasema linahitaji kukokotolewa kwa kuzingatia mfumo wa mishahara ya watumishi wa umma, Pinda anasema haliwezekani kwa kuwa viwango walivyoomba ni vikubwa mno na kipindi hiki ni katikati ya bajeti ya serikali ya 2011/2012.

Ni Pinda huyuhuyu ambaye awali alikiri kuwa ni haki ya madaktari wanafunzi kupata posho zao wanazodai kwa kuwa hawajaanza kupata mishahara.

Pinda alikiri pia kuwa serikali imechelewa kulipa posho za madaktari wengine kwa miezi miwili sasa.

Cha ajabu ni kwamba Pinda anageuka, anafuta au kusahahu aliyosema na kuamuru “madaktari wote kurejea kazini, tena mara moja” au watakuwa wamepoteza kazi.

Kwa muda mrefu serikali imekuwa na tabia ya kulimbikiza mishahara na posho mbalimbali za watumishi wake hasa wa kada ya elimu na afya. Mara nyingi madai haya yamekuwa yakilipwa baada ya shinikizo la mgomo.

Katika hili la sasa, serikali haikuchukua hatua za kuzuia mgomo huo licha ya kupewa muda wa kusikiliza madai hayo.

Hoja dhaifu zilizojengwa na Dk. Nkya kuwa pale Muhimbili madaktari hao wamekuwa wengi, hivyo wangeweza kuhatarisha ubora wa taaluma zao, haikuwaingia akilini na iliwakera baadhi yao .

Madaktari wamesema kwa miaka nendarudi wamekuwapo hospitalini hapo kwa idadi hiyo, na hata zaidi, bila kuhatarisha taaluma zao.

Hivi kwa nini serikali imekurupuka kuhamisha madaktari Muhimbili baada ya mgomo? Kwa nini baada ya kuwaondoa wao, imepeleka wengine wapya 51 na baadaye kurejesha baadhi yao katika kinachoonekana kuwa mbinu ya kuwagawa?

Kutokana na utata huo, MAT ililazimika kujumuika na wenzao waliotangulia kugoma na kuitaka serikali kuwarejesha wenzao bila masharti yoyote. Haikufanya hivyo.

Ni kuendelea kwa mgomo ambako kumefanya serikali kuwarejesha madaktari walioondolewa Muhimbili. Sasa swali linabaki hili: Je, zile sababu za awali zimekwisha?

Kwa ujumla hatua zilizochukuliwa na serikali katika kushughulikia madai hayo zinatoa picha kuwa haiko tayari kulipa kwa hiyari, wala kwa wakati, madai ya msingi ya madaktari.

Kutokana na hali hiyo, vema madaktari waendelee kushikamana hadi madai yao yatatuliwe.

Kauli za “udaktari ni wito” zimepitwa na wakati na haziwezi kuliokoa taifa katika mgomo huu.

Madaktari wanafanya kazi yao . Serikali itemize wajibu wake – kuwalipa posho na mishahara. Wananchi wapate huduma wanayostahili. Hakuna njia ya mkato.

0
No votes yet