Serikali inahujumu wafugaji Ngorongoro


Navaya ole Ndaskoi's picture

Na Navaya ole Ndaskoi - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

NINACHANGIA mjadala ulioibuliwa na Profesa Ibrahim Lipumba, aliyesema Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kazi; ukweli unaowakera wapambe wa Kikwete.

Wawili miongoni mwao ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu na mbunge wa zamani wa Temeke, John Kibasso. Hawa waliandika kumtetea Kikwete.

Serikali ya Rais Kikwete inawahujumu wafugaji katika Hifadhi ya Ngorongoro. Profesa Issa Shivji pamoja na Dk. Wilbert Kapinga wamebainisha jinsi serikali inavyowadhulumu wafugaji katika kitabu The Rights of the Maasai Living in Ngorongoro Conservation Area kilichochapishwa miaka kumi na mbili iliyopita.

Rais Kikwete ameongeza kwa kiasi kikubwa dhuluma hii. Akihutubia Bunge jipya tarehe 30 Desemba 2005 Kikwete aliubeza kwa kiasi cha kutisha ufugaji wa asili. Alisema, "Ng’ombe hanenepi, mfugaji hanenepi."

Kikwete alipoapishwa kuwa Rais alimteua Pius Msekwa, Spika wa zamani wa Bunge kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Uteuzi huu ulifuatia kuchaguliwa kwa Samwel Sitta kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumgaragaza vibaya Msekwa. Msekwa anatoka Kisiwa cha Ukerewe katika Ziwa Victoria.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Emanuel Chausi, asili yake ni Ukerewe. Aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Hifadhi wakati Chausi akiwa Mhifadhi Mkuu, Elvis Musiba, kama ilivyo kwa Msekwa na Chausi, anatoka Ukerewe.

Chausi alipofariki dunia, Rais Kikwete akamteua Bernard Murunya naye kutoka Kanda ya Ziwa kuwa Mhifadhi Mkuu.

Tarehe 5 Desemba 2009 Kikwete alimteua Msekwa kwa mara nyingine tena kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga alimteua Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Ndugai pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Mwangunga alimwondoa Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele. Kama mwakilishi pekee wa kuchaguliwa wa wafugaji waishio katika hifadhi hii, kuna desturi ya mbunge wa Ngorongoro kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Ngorongoro.

Kwa nini Mwangunga alimwondoa Telele na kumwingiza Ndugai kwenye bodi? Tarehe 9 Julai 2009 Telele alimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni kwa nini Serikali inawafukuza kikatili wafugaji Loliondo?

Telele aliendelea kuwapigania wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro. Tarehe 6 Novemba 2009 aliwasilisha maelezo binafsi bungeni akitaka maelezo kuhusu hujuma dhidi ya wananchi Loliondo.

Spika wa Bunge, Samwel Sitta aliiamuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayoongozwa na Ndugai kwenda Loliondo kuchunguza madai ya Telele.

Mwangunga alimzawadia Ndugai ujumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili amlinde na kashfa ya Loliondo?
Kamati ya Ndugai iliandika taarifa ya kutetea yale aliyosema Mwangunga bungeni kumjibu mbunge wa Ngorongoro.

Wakati mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele akifanya juhudi ili wafugaji waliodhulumiwa Loliondo watendewe haki na ukweli ujulikane, akina Ndugai walienda Ngorongoro na kutoa matamshi ya ajabu na ya kutisha dhidi ya wafugaji.

Vyombo vya habari vikaripoti kuwa kuna wafugaji karibu 65,000 katika Hifadhi ya Ngorongoro. Madai haya hayana msingi. Mbali na wafugaji pia kuna wafanyakazi wa hoteli za kitalii pamoja na wafanyakazi wa hifadhi na familia zao katika hifadhi hii.

Ifahamike kuwa mwaka wa fedha 2008/2009 watalii 454,000 walitembelea Hifadhi ya Ngorongoro na magari 400 kwa siku.
Hadi pale kanuni za hisabati zitakapobadilishwa, Watanzania 65,000 hawawezi kamwe kuwa wengi kuliko watalii 454,000.

Serikali ya Kikwete inadai pia kuwa kuna ng’ombe 13, 6550 pamoja na mbuzi na kondoo 19, 3056 katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Moringe ole Parkipuny, mbunge wa kwanza wa Ngorongoro alisema mwaka 2008 kuwa wilaya ya Ngorongoro ilikuwa na mifugo chini ya 275,000.

Mifugo hii hulishwa pamoja na hawa wanyamapori. Kama wanyamapori zaidi ya milioni 2 hawaharibu mazingira, mifugo chini ya 275,000 itaharibu vipi?

Kwa nini wafugaji wa Kimaasai wanaishi katika hifadhi ya Ngorongoro? Mwaka 1951 Profesa Bernhard Grzimek, Mjerumani katili aliyepata kuwa mwanachama mwandamizi wa Chama cha Nazi cha muuaji Adolf Hitler, alifika Afrika na Tanganyika.

Aliandika kitabu na kutengeneza filamu maarufu iliyoitwa Serengeti Shall Not Die. Grzimek aliijaribu kuishawishi serikali ya Tanganyika chini ya wakoloni Waingereza kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuwafukuza wafugaji wa Kimaasai.

Lakini miaka ya 1950 vita vya Mau Mau vilipamba moto Kenya. Wakenya walishawashinda Waingereza. Waingereza waliona kuwa kuwaondoa wafugaji Serengeti na Ngorongoro kama alivyoshinikiza Profesa Grzimek kungeleta vita Tanganyika.

Hatimaye Grzimek, akishirikiana na wakoloni wengine wabaguzi wa rangi, alifanikiwa kuishinikiza serikali ya Tanganyika kuanzisha Hifadhi ya Taifa Serengeti. Wamaasai wakaondolewa kimabavu kupisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti 1959.

Serengeti, hifadhi ya kwanza Tanganyika, ni kubwa zaidi ya nchi ndogo 45 duniani zikiwekwa pamoja.

Hata hivyo, serikali iliogopa kuwafukuza wafugaji moja kwa moja. Baadhi ya wafugaji walielekea Loliondo kujiunga na wenzao waliokuwa kule. Baadhi yao wakahamia Ngorongoro kujiunga na wenzao waliokuwa wakiishi Ngorongoro.

Hifadhi ya Ngorongoro yenye ukubwa wa karibu kilometa za mraba 8,298 ilianzishwa. Wafugaji waliruhusiwa kuishi pamoja na mifugo yao huku wanyamapori pamoja na biashara ya utalii vikiendelea; yaani matumizi mseto ya maliasili na ardhi.

Tarehe 27 Agosti 1959 gavana, Richard Turnbull aliliambia Baraza la Maasai kuwa serikali iliamua kuwaacha Wamaasai Ngorongoro kwa kuwa wamepoteza kilomita za mraba zaidi ya 14,000 Serengeti.

Alisisitiza kuwa endapo siku za usoni, kama sasa 2010, kutatokea migogoro kati ya maslahi ya wafugaji na mifugo kwa upande mmoja, na maslahi ya wanyamapori na utalii kwa upande mwingine, wafugaji wapewe kipaumbele.

Lakini mwaka 1975 serikali iliwafukuza kikatili wafugaji kutoka katika kreta (shimo) katika hifadhi hii. Mbali na kreta hiyo kuna maeneo mengine makubwa ambayo leo wafugaji wamepoteza ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

Mhifadhi mkuu, Bernard Murunya anatamba kuwa wafugaji zaidi ya 550 wamehamishwa Ngorongoro tangu mwaka 2005.

Sasa serikali ya Rais Kikwete inaanda muswada utakaopelekea sheria mpya ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Muswada huu utateketeza fedha za umma bila sababu. Kwa nini Serikali isitangeze tu kuwa sasa Ngorongoro ni moja ya hifadhi 14 za taifa?

Kwa hatua hii, serikali imevunja katiba kwa kuhamisha wananchi mahali ambapo wanapamiliki kisheria. Kinachoweza kusaidia ni kule ibara ya 46(2) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupiga marufuku kumshitaki rais.

Mwandishi wa makala hii, ni mwanaharakati wa haki za binadamu na anatoka jamii ya wafugaji. Anapatikana kwa simu Na. 0786 453 194
0
No votes yet