Serikali inaihujumu TANESCO kwa ajili ya Dowans?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Gumzo
Dowans Power Plant

KWA mara nyingine, serikali, kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), imetangaza mgawo wa umeme ambao utaathiri mikoa yote inayopata umeme kupitia gridi ya taifa.

Kwa mujibu wa tangazo la serikali lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, mgawo huo umetokana na kile kinachoitwa, “Kupugua kwa kina cha maji kwenye vituo vya kuzalisha umeme vya Kihansi na Pangani na kuharibika kwa mtambo wa kuzalisha umeme wa Pangani, Hale na Songas.”

Mitambo iliyoharibika ina uwezo wa kuzalisha megawati 65 tu za umeme.

Hii si mara ya kwanza kwa TANESCO kutangaza mgawo wa umeme kwa kisingizio kile kile cha kupungua kwa maji au kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Dk. Rashidi ndiye alikaripia Bunge kwa jazba na ghadhabu, akisema TANESCO ingejiondoa katika mjadala wa ununuzi wa mitambo yenye utata ya kampuni ya Dowans Holding (Tanzania) Limited, na kwamba asilaumiwe iwapo nchi itaingia gizani.

Tishio la Dk. Rashid lilikuja baada ya Bunge kupitia Kamati ya Nishati na Madini, kugoma kubariki ununuzi wa mitambo ya Dowans, huku Bunge likiitaka serikali kununua mitambo yake.

Hata hivyo, si serikali, wala Bodi ya wakurugenzi ya TANESCO iliyokemea Dk. Rashid kwa kauli yake hiyo.

Haikuchukua muda, TANESCO ilitangaza mgawo mkubwa wa umeme nchi nzima kutokana na kile ilichoita, “kuharibika kwa mtambo wa kuzalisha umeme wa Songas.”

Hata hivyo, kinachotia shaka sasa ni mgawo huu kuja miezi 10 tu baada ya serikali kuahidi wananchi kuimarisha vyanzo vya umeme na kutafuta vyanzo vipya ikiwa pamoja na kununua “mtambo mpya wa kuzalisha wa megawati 200.”

Ukifuatilia kwa makini tatizo la mgao wa umeme utagundua kuwa kuna tatizo kubwa la uongozi ndani ya TANESCO na serikali kwa jumla.

Mtendaji mkuu aliyekabidhiwa jukumu la kuongoza shirika hili tayari amethibitisha kwamba si mtu mwenye uwezo wa kuongoza shirika na hana sifa za kuweza kuaminiwa.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, Katibu Mkuu, Arthur Mwakapungi na Kamishina wa Nishati nao wameshindwa kazi.

Kama si hivyo, ziko wapi ahadi za serikali za kukabiliana na tishio la Dk. Rashid la nchi kuingia gizani?

Je, baada ya Dk. Rashidi kutishia kuwa lazima nchi itagubikwa na mgawo wa umeme ifikapo Septemba au Oktoba mwaka huu, watendaji hawa walifanya nini kuokoa taifa na dhahama hiyo?

Je, tahadhari ambayo wizara ilichukua ili kauli ya Dk. Rashidi isitekelezeke ni ipi?

Kuna haja ya serikali kuwaeleza wananchi hatua zilizochukuliwa, hasa kwa kuwa ni serikali yenye jukumu la kuhakikisha umeme unapatikana na nchi haitumbukii katika giza.

Ni jukumu la serikali kusimamia shughuli zote katika sekta ya umeme. Hii ni pamoja na kusimamia kazi zinazofanya na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na menejimenti yake.

Moja ya kazi kubwa ambayo bodi hiyo inapaswa kuwa nayo ni mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa upatikanaji wa umeme nchini.

Tunajua kwamba serikali inaweza kuja na majibu rahisi tu, kwamba tangu mwaka 1990 imebuni miradi mikubwa ya umeme.

Haitasita kutaja miradi ya IPTL, Songas, Aggreko, Richmond/Dowans, Alstom, Tegeta, Wartsila, Ubungo na Kihansi ambayo imesaidia kupunguza matatizo kwenye mfumo wa umeme nchini.

Lakini ni serikali, iliyotangazia umma Septemba 2006 kuwa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu yamekauka. Serikali ilisema kutokana na hali ilivyo bwawa la Mtera lingejaa baada ya miaka mitatu.

Hata hivyo, bwawa hilo liliwaaibisha likajaa katika muda mfupi baada ya kauli ya serikali, likafurika hadi uongozi ukamuru kumwaga maji ili maji hayo yasilibomoe.

Ni kisingizio hiki cha nchi kuingia katika gizani kulikodaiwa kungetokana na kukauka kwa mabwawa ya Mtera na Kidatu, ndiko kulikosababisha vigogo serikalini kutumbukiza nchi katika mkataba wa kitapeli wa kampuni ya Richmond/ Dowans.

Haikuchukua muda ukweli ukadhihirika, kwamba uwongo ule ulikuwa na shabaha moja tu: Kutengeneza ulaji wa wajanja wachache waliomwaga mabilioni kuchangia kampeni za uais wa CCM katika uchaguzi, ambao baadhi yao ndio wanaotajwa kuwa wahusika wa Richmond.

Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba hatua zilizochukuliwa hazitoshi. Kigezo cha kutokutosha ni pale panapotokea upungufu kidogo wa maji kwenye baadhi ya vituo vya kuzalishia umeme, ama mitambo kuharibika (na mitambo ya SONGAS kuharibika mara kwa mara) mara moja nchi inatumbukia katika mgawo.

Ndiyo maana mgawo wa sasa unatia aibu. Je, nchi huru iliyojitawala kwa miaka 48 inawezaje kuingia katika giza kwa kukosekana kwa megawati 65 tu za umeme? Je, hatuna mikakati endelevu ya kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme?

Machi 2008 mkutano wa wataalamu ulikubali kuwa endapo mahitaji ya umeme yangeongezeka kwa kasi, TANESCO ingefanya marekebisho ya mikataba yake na makampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans (100 MW), Aggreko (40 MW) na Alstom ya Mwanza (MW 40) ili kuongeza mikataba kutoka mwaka 2009 hadi 2012.

Hata hivyo, 30 Juni 2008, Dk. Rashidi alitangaza kuvunja mkataba na Dowans. Kwa kujiamini alisema, "Kwanza hatuhitaji umeme wao (Dowans), tunao mwingi...kuna mitambo ya megawati 100 ya Ubungo (ex-Wartsila ya Finland ). Mitambo hiyo ilizinduliwa 14 Novemba 2008 na Rais Jakaya Kikwete.

Tarehe 25 Oktoba 2008, Dk. Rashid alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuelezea upatikanaji wa umeme kwenye gridi ya taifa.

Katika taarifa yake Dk. Rashid hakusema kwamba kujiondoa kwa serikali katika mkataba wa Dowans kungeifanya TANESCO ishindwe kutimiza wajibu wake wa kuwapa wananchi umeme.

Hata hivyo, haikuchukua muda Dk. Rashidi huyo huyo asikika akiomba Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuruhusu TANESCO kununua mitambo ya Dowans.

Hadi sasa, Dk. Rashid hajasema nini kilibadilisha uamuzi wake wa awali. Aliahidiwa nini na nani?

Katika matukio haya, ni upi msimamamo wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO chini ya uongozi wa Peter Ngumbullu? Mbona inavyoelekea Dk. Rashidi anaongoza shirika hilo kama mali yake binafsi?

Hii ni kwa sababu haijawahi kusikia Bodi ya TANESCO ikitoa kauli kuhusu masuala yanayotia shaka ndani ya shirika. Kilichowahi kusikika kwa Bodi ni pongezi, kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Dk. Rashidi amefanya kazi nzuri.

Mfano uliotolewa na Bodi ni jinsi utawala wa Dk. Rashid ulivyoweza kupunguza madeni ya shirika lililokuwa linadaiwa.

Hata hivyo, jambo moja lililo wazi ni kwamba Bodi haikusema madeni haya hayakulipwa kutokana na ubunifu wa ongezeko la mapato au ukusanyaji wa madeni ama kupungua kwa gharama za matumizi yasiyo ya lazima uliobuniwa na Dk. Rashid.

Madeni ya TANESCO yaliweza kupunguza kutokana na fedha zilizokopwa (Sh. 280 bilioni) na serikali katika benki mbalimbali nchini zikiwamo Stanbic, EXIM na CRDB.

Kingine ambacho Bodi ya Ngumbulu ilisahau ni kuwa kazi ya Bodi si kutazama mapato na matumizi tu. Bodi inajukumu la kusimamia masuala ya kiutendaji. Na katika hilo, Dk. Rashidi hana sifa zozote za kubeba.

Tangu ameingia TANESCO, Dk. Rashid ameshindwa kupunguza bei za umeme, ameshindwa kuboresha huduma kwa wateja na sasa ameingiza nchi katika mgawo wa umeme.

Kimsingi Dk. Rashid ameshindwa kazi. Kinachotakiwa ni serikali kuchukua hatua sasa. Haipaswi kusubiri mtu huyu amalize mkataba wake.

Kuondoka kwake kunaweza kujenga uwezo kwa TANESCO kufanikisha dhamira ya serikali kuleta wawekezaji kutoka nje. Dhamira hii (ya Rais Kikwete) haiwezi kutekelezeka katika nchi ambayo umeme unakatika kila wakati na mgao kuwa jambo la kawaida!

Wakati nchi za wenzetu zinasonga mbele kwenye maendeleo kutokana na kutilia mkazo sekta ya umeme, sisi kama taifa tumebaki nyuma.

Ni asilimia 13 tu ya Wanzania wanaopata umeme wa uhakika, ukilinganisha na asilimia 80 katika nchi ya Afrika Kusini.

Mahitaji yetu ya umeme nchini ni kati ya megawati 700 na 900 tu, wakati Afrika Kusini yamefikia megawati 40,000. Je, maendeleo ya sekta hii yanaweza kuletwa na viongozi aina hii tuliona sasa?

Inawezekanaje TANESCO ishindwe kuwa na mipango ya kunusuru nchi pale mitambo jirani ya SONGAS inapo haribika harafu ukasema hapa kuna uongozi?

Tangu mwaka 2006, kila mitambo ya SONGAS ilipoharibika, TANESCO inatangaza mgawo wa umeme.

Tatizo lingine ni kuwa kwenye mgao wa umeme wa mwaka 2006, TANESCO ilipata hasara kubwa kwa kushindwa kupata mapato yanayotokana na kuuza umeme.

Uongozi wa shirika ulilalamika kuwa linapoteza mapato ya karibu bilioni tisa hadi 11 kwa mwezi, kwa kushindwa kuuza uniti za umeme.

Ikiwa hivyo ndivyo, TANESCO imeshindwaje wakati wa neema kutafuta fedha za kununulia mitambo ili kuepuka majanga ya mgao wa umeme? Au kwa maoni ya Dk. Rashidi, ni lazima tu kununua mitambo ya Dowans, hata kama imejaa lundo la utata?

Kwanini Dk. Rashidi hakuwa ametoa hoja kwa Serikali izungumze na makampuni Aggreko na Alstom, ambayo yalikuwa na nia ya mkataba kuongezwa muda, badala yake ameng’ang’ania Dowans pekee?

Ndiyo utendaji huu ambao unazua maswali mengi kutoka kwa wananchi. Kwa mfano, mitambo hii ya Kihansi na Hale iliharibika lini? Gharama zake kiasi gain?

Kipi kilichosababisha serikali na TANESCO ishindwe kuifanyia matengenezo hadi kutaka nchi kuigia gizani?

Je, akitokea mtu leo hii na kusema kwamba hapa kuna hujuma inayotendwa ili kuhalalisha ununuzi wa Dowans, Dk. Rashid atakataa?

Wala hakuna mashaka kwamba Dk. Rashid anaendesha shirika kwa hisia na bila kufanya utafiti. Ni mtu wa kukurupuka na asiyeweza kuaminika katika jamii.

Tuhuma za sasa ndani ya TANESCO na zile za kale katika ununuzi wa rada, unamuondolea sifa ya kuwa mtendaji wa shirika hili nyeti la umma.

Angalau mkataba wake unakaribia ukingoni, mungu anaweza kusaidia TANESCO ikapata mtu mwenye uwezo na hadhi ya kuongoza shirika hili.

Ni ukweli usiopingika kwamba serikali ilikabidhi TANESCO kwa mtu asiye na uchungu na shirika wala wateja wake. Ndiyo maana kwake suala la kutangaza mgao wa umeme ni kitu cha kawaida.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: