Serikali inajenga mapinduzi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SHAHADA mara tatu. Lakini kampuni ya Kagoda Agriculture Limited imetajwa zaidi ya mara mia. Bado inaendelea kutajwa kama moja ya kampuni zilizonufaika na fedha zilizokwapuliwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Maodita, tangu wale wa awali – Delloite & Touche – waliofurushwa na serikali kwa sababu ya kugusa “mambo ya wakubwa” – wamethibitisha Kagoda pekee ilichota dola 30.8 milioni. Hii ni sawa na zaidi ya Sh. 40 bilioni.

Fedha zilizoibwa kwa jumla kutoka akaunti ya EPA zimetajwa na maodita kuwa ni Sh. 133 bilioni na kuhusishwa kampuni 22, ikiwemo Kagoda. Hivyo ndivyo ripoti ya maodita walioajiriwa mara ya pili – Ernst and Young inavyosema.

Kwa kiwango hicho cha wizi, na kulingana na taarifa ya ukaguzi wa akaunti hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2005/06, ina maana Kagoda walichota fedha nyingi zaidi.

Bado Kagoda i midomoni mwa utawala na umma. Kutuhumiwa na kutajwa kote huko wakati mwingine vyombo vya habari – na MwanaHALISI imeongoza kwa hili – vikianika ushahidi huu na ule unaoigusa kampuni hiyo, hakujasaidia serikali ijitambue.

Serikali na taasisi zake zinazoratibu na kusimamia uchunguzi, kukusanya ushahidi na kushitaki watuhumiwa mahakamani, kila siku wakiulizwa taarifa za Kagoda, hawana jipya, labda kujigongagonga tu.

Leo mtendaji wa taasisi hii anasema hili, kesho mtendaji wa taasisi nyingine anasema lile; na keshokutwa ofisa wa serikali kuu, kama vile waziri, anasema lake. Shaghalabaghala, songombingo na hadithi za abunuasi.

Ndio. Kauli zao hazijibu hoja kwanini wamiliki wa Kagoda hawajabanwa kisheria ili serikali ikatafuta kingine cha kutatua; labda umasikini uliokithiri mamilioni ya wananchi.

Binadamu lazima awe na ari (ajitambuwe); ajitahidi kuepuka lawama za kushindwa kuwajibika. Kwa serikali yetu, ni mwiko kuwajibika, bali zaidi kinachoonekana ni kuzidisha utata na manung’uniko.

Jambo moja ni dhahiri: Wananchi na hata nchi rafiki wanaendelea kujiuliza; “hivi Kagoda ni jini gani na kutoka ardhi ipi hata lisikunjwe likakunjika.”

MwanaHALISI katika namna mbalimbali limechapisha taarifa zinazotaja watu, tena wengine viongozi wakubwa tu serikalini na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioshiriki kuchora na kuidhinisha “sanaa ya ufisadi” huu wa EPA. Hadi sasa hakuna lolote.

Ni taarifa ninazoamini vyombo husika wamezisoma vizuri. Iwapo zingekuwa za uongo, serikali ninayoijua haitaki kuacha mwanya kubana waliofichua siri, ingepiga kelele na kukamata waendeshaji gazetini. Iliwakamata kwa jingine la kipuuzi tu, isingeshindwa hili.

Hakuna hatua ya maana iliyopigwa katika kubana waovu. Badala yake ni kuona “utatu mtakatifu.”

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba; Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah wanaendelea kuonesha ufundi wa kuzungumza.

Kama maneno matamu ni shibe, basi Watanzania hawana tena njaa.

Wiki iliyopita tu, DCI Manumba alinukuliwa na gazeti la kila siku la NIPASHE akisema bado jalada la Kagoda lipo mezani kwake na uchunguzi unaendelea.

Lakini sikiliza mwishoni. Anasema, “ukiniuliza lini upelelezi utakamilika nitakujibu sijui ni lini.”

Walishasikika DPP Feleshi na Hoseah wakizungumzia suala hilo na kutupiana mpira. Kwamba “jadala tulikuwa nalo lakini nimeshalipeleka kunakohusika.”

Hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mwishoni mwa mwaka, alipoulizwa kuhusu hilo na kuahidi uchunguzi na taarifa kutolewa huku akitamba “serikali haina cha kuogopa,” ninaamini sasa anajisikia maudhi kuuulizwa tena uchunguzi wa Kagoda umefikia wapi.

Kwa ujumla, serikali imeonesha udhaifu mkubwa katika suala hili. Imeshindwa kuthibitishia wananchi kuwa kweli imedhamiria kupambana na ufisadi mkubwa uliojikita nchini.

Wakati serikali ikijitapa kurudisha Sh. 70 bilioni na kupeleka “mawakala tu” wa ufisadi mzima mahakamani, inashangaza kusikia serikali hii imekosa mtu wa kutoa ushahidi mahakamani hadi kusababisha kesi kuhairishwa.

Tayari viongozi walishasema “hatuwezi kukamata watu na kuwapeleka mahakamani wakati hakuna ushahidi wa kutosha. Wakishinda watadai fedha nyingi.”

Lakini ni ukweli usioa na shaka kwamba wahusika ni watu wenye nguvu ya pesa nyongi. Ndiyo maana serikali inawaogopa.

Hata Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema aliwahi kusema “kuwakamata inahitaji uwe umechunguza sana hadi nje ya nchi. Maana ukikosea utabomoa nchi.”

Kweli bwana, kwa kisingizio cha kutopata “ushahidi wa kutosha,” watuhumiwa wakuu wakiwemo waliotajwa kuwa waliita na kuajiri mawakili mashuhuri na kuwapa nyaraka za mikataba ya kuchotea fedha za EPA, wangali huru na wanakula raha mjini.

Si ajabu kutokea mtu akataja majina ya anaowaita “mafisadi papa.” Kitendo chake cha kijasiri ni ishara ya hisia kali walizonazo wananchi wengi za kukata tamaa baada ya kuona mwenendo uliojaa malengelenge wa viongozi wa serikali katika kupambana na ufisadi.

Hapa kuna hatari. Mwenendo wa serikali unakataa utawala bora. Haustawishi utamaduni wa uwajibikaji na utendaji wa uwazi na kwa usawa.

Anapotokea kiongozi wa serikali ya CCM akasimama na kusema “Tumejidhatiti kupambana na ufisadi” anazungumzia mapambano yanayobagua waovu. Wengine washughulikiwe hadi mahakamani na wengine wasiguswe kamwe.

Hii ndio hatari ninayoieleza: katika taifa letu sasa sheria inatumika kubana baadhi tu ya Watanzania. Kwa raia wengine haina nafasi. Uongozi wa namna hii unakosa uongozi. Uongozi unastawisha “bora utawala” badala ya “utawala bora.” Ni uongozi muflis.

Penye uongozi wasiojali panapandikizwa chuki miongoni mwa wananchi. Hapo wananchi wanajengwa moyo wa kuamini serikali imewachukia na kuwakandamiza. Hali ya amani na utengamano inapotea. Ni vema serikali isitufikishe huko.

Nchini Somalia hakuna utawala tangu alipoangushwa Mohamed Siad Barre na utawala wake mwaka 1991 maana hakuna Msomali aliyefanikiwa kuunganisha Wasomali ili kujenga nchi yao.

Kilichotokea ni kuibuka kwa makundi ya “mabwana wa vita” ambao kwa kutumia silaha walizopora, wanaendeleza mikakati ya kujitajirisha na kutumikia mabwana zao.

Kwa sababu mataifa yenye utajiri yananufaika na mchafukoge huo inayoendelea katika nchi hii ya Pembe ya Afrika, itachukua muda mrefu kupatikana utulivu wa kweli Somalia.

Kadhalika, itachukua miongo mingi Tanzania kufika hapo. Lakini ukweli ni kwamba amani huchafuka siku moja tu na huwa ni hitimisho la kuvunda kwa dalili zilizoanza kujitokeza miaka mingi nyuma na kidogokidogo.

Unapokuwa na serikali inayobagua watu, hasa waovu, na ikawa inawanyenyekea hata wengine kuwatumia kama sehemu ya maamuzi ya kisera na kiutawala, jua hapo wananchi wanachochewa wakasirike.

Watu waliojaa hasira kutokana na tabia mbaya ya serikali yao, siku moja watatamani kujiachia ili kupambana na wanaoamini ni waovu wanaolindwa na utawala. Hayo ni mapinduzi.

Utawala usipotenda kwa haki, ukishamiri kudhalilisha raia, usipojali haki za binadamu kwa usawa na ukatumia vibaya raslimali, hakika unajenga hisia za kimapinduzi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: