Serikali inalipiga Bunge teke


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

KUNA usanii mkubwa unaendelea nchini juu ya utekelezaji wa maagizo halali ya Bunge. Sasa ni miaka miwili na nusu imepita, tangu Bunge lipitishe azimio juu ya zabuni ya kufua umeme kutoka kampuni feki ya Richmond, serikali bado haijachukua hatua.

Pamoja na azimio hilo, bado yapo mambo mengi ambayo, hakika, hayaonyeshi nia ya kweli ya serikali kuyashughulikia.

Kwa mfano, hadi sasa hatma ya waliokuwa mawaziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake, Dk. Ibrahim Msabaha, ambao walitakiwa kufanyiwa uchunguzi kama walihusika katika vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa zabuni na utaratibu wa kufaulisha mkataba huo kwa Dowans, haujajulikana.

Kadhalika, umma haujaelezwa lolote juu ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambao kwa pamoja, walitakiwa kuwajibishwa kwa kuhusika, kwa njia moja au nyingine, katika suala la Richmond .

Pia wapo watendaji wengine wa serikali, waliotajwa katika azimio la Bunge ambao hawajachuliwa hatua. Lakini pia azimio lilitaka yafanyike marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA).  Hivyo na vingine vingi bado havijafanyika.

Kuna hata hili la mkataba wa kampuni ya Kupakua na Kupakia Mizigo Bandarini (TICTS). Bunge lilipitisha azimio la kuvunjwa kwa mkataba kutokana na TICTS kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Kuna habari ambazo si rasmi, kwamba serikali imeshikwa kigugumizi kuvunja mkataba wa TICTS kwa kile kinachodaiwa kuwa italazimika kulipa fidia ya Sh. 1 trilioni moja!

Tunajua kikatiba Bunge ndilo lenye dhima ya kuisimamia serikali, maagizo yake hayapingwi labda kama bunge lenyewe litatengue maamuzi yake. Hili liko wazi.

Kwa maana hiyo basi, serikali haina mbadala wa kutekeleza maamuzi ya bunge, labda kama itakuwa imeamua kutangaza mgogoro, kitu ambacho watawala makini hawapendi kukiona kinawatokea.

Tunafahamu kwamba muda ni rasilimali muhimu katika uzalishaji. Kadri siku, wiki, miezi na miaka inavyokwenda bila kuonekana kwa vitendo dhamira ya serikali ya kutekeleza maazimio hayo ya Bunge, kitu kimoja tu kinaweza kuelezwa katika hali hii.

Kwamba serikali haiko tayari kutekeleza maamuzi ya bunge, lakini haiwezi kusema hivyo, isipokuwa njia sahihi ni kuvuta muda.
 
Wanasheria wanasema haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa. Lakini pia kuna usemi kwamba muda unatibu (time heals). Kwa haya yote mawili yanawezekana ndiyo yanatokea.

Kwamba, serikali inavuta muda ikijua mwisho wa yote Bunge la sasa litafikia mwisho wake na kwa maana hiyo maazimio yake yanakwenda na maji.

Lakini la pili nalo ni sahihi. Baada ya kitambo, hasira, kiu au hamu ya wabunge kufuatilia masuala haya, mwisho wa yote vitakwisha kwa sababu jambo mambo yatakuwa yamepitwa na wakati. 

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Bunge kama taasisi, limeonekana likifanya kazi, hasa baada ya baadhi ya wabunge, ambao ni mawaziri kuonja hasira ya wananchi kutokana na kitendo chao cha kumfukuza bungeni mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kwa hoja ya mgodi wa Buzwagi.

Tangu Bunge lilipojiingiza katika ushabiki wa ovyo, na kumfukuza Zitto bila kujali na kutafakari kwa kina kile alichokuwa anazungumzia, badala yake ukereketwa wa itikadi za vyama ukawapofua kiasi cha kuchanganya mambo ya maslahi ya kitaifa na ukereketwa wa siasa za vyama, gharama yake imekuwa kubwa mno.

Baada ya machungu hayo, Bunge lilikuja kujipambanua katika hisia za kivyama na kujielekeza kwenye dhima yake muhimu ya kusimamia serikali. Kilele cha uwajibikaji wa Bunge kikiwa ni Februari 2007, Baraza la Mawaziri lilipoparaganyika.

Kwa mwendo huo, Bunge ambalo huko nyuma, hasa zama za serikali ya awamu ya tatu, lilipata kuwa chini sana kwenye kura ya maoni, lilijipambanua na kuwa mdomo wa wananchi.

Zile zama za wabunge kutishwa tu na rais aliye ikulu zikawa zimepitwa na wakati. La muhimu zaidi, kiongozi mkuu wa taasisi hiyo, yaani Spika, naye akijaribu kujenga Bunge lenye hadhi na nguvu za kuweza kuishurutisha serikali kufanya kazi.

Mafanikio haya ya Bunge, kwa vyovyote vile, hayajawafurahisha baadhi ya watawala, ambao wangependa kuendelea kutumia taasisi hiyo kama chombo chao cha kupitisha na kuhalalisha mambo yao, hata kama hayana maslahi na umma.

Msimamo huu mpya wa Bunge, kwa bahati mbaya, umejengewa hoja za kutafuta njia za kuudhoofisha. Ndiyo maana sasa kinachozungumzwa ni hisia za ovyo kabisa, kwamba nani kafanya nini bungeni lakini yu upande upi?

Bunge linataka kujengewa dhana kwamba ni chombo cha baadhi ya wabunge wasiotaka serikali ifanikiwe, wakiongozwa na Spika wake, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge wapambanaji, ili kuidhoofisha serikali.

Hoja za namna hii zinajengwa kwa fikra dhaifu, nyepesi, ambazo haziangalii kabisa mbele na kutafakari nafasi ya taasisi hii katika kuhakikisha kwamba watawala hawatumii ovyo madaraka waliyopewa na wapiga kura.

Kwa mfano, si jambo la kushangaza kukuta watu wakitumia baadhi ya waandishi wa habari kumwandama Spika Sitta na kundi fulani la wabunge wapambanaji, wasiokuwa tayari kutupiwa makombo ya uchafu wa watawala.

Juhudi hizi zimekuwa kubwa na za kutosha, kiasi kwamba wanaoendeleza ulimbukeni huu wanataka serikali iendelee tu kukaa kimya wakati wapo watu maisha yao yote yamekuwa ni kupora rasilimali za nchi hii.

Hawa wamejenga dhana, hadi baadhi ya watawala wamejawa na hofu, na wengine waliokuwa wanaonekana mahiri kabisa katika kukabiliana na vitendo vya kifisadi, sasa ama wamesalimu amri au wameamua kujiunga na kundi la walaji. Aibu tupu!

Kwa hiyo, umma unapoona kwamba maazimio ya Bunge, kama yanayohusu Richmond na TICTS, hayatekelezwi, wanajiuliza kulikoni? Mbona sasa ni miaka miwili na ushei suala la Richmond halionyeshi kufikia ukingoni?

Hili la TICTS nalo linaonekana kama serikali inafanya ujanja wa nataka sitaki. Mkataba hauvunjwi, kila kukicha habari mpya kuhusu kampuni hii, ambayo pasi na shaka yoyote, imeshindwa kutekeleza majukumu yake, achilia mbali mkataba tata ulioongezwa kinyemela na serikali ya awamu ya tatu wakati ikiondoka madarakani mwishoni mwa 2005.

Tafsiri ya mienendo yote hii ya serikali ni moja tu, kwamba maazimio ya Bunge hayatatekelezwa kwa sababu walaji, mafisadi na wahalifu sugu wameitisha na imetishika.

Sasa inatafuta njia za kukwepa utekelezaji wake ama kwa kuchelewesha muda au kwa kuvuta muda ili watu wasahau. Yote haya kama Bunge halitasimama imara, ni wazi mafisadi wamerejea kwa nguvu na kasi kubwa, tena wakiwa wameteka mateka wengi ndani ya mfumo wa dola. Tusubiri tuone.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: