Serikali inapokwenda kwa ‘Babu Loliondo’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Babu wa Loliondo

SERIKALI imepata mbia katika ‘kupambana na maradhi.’ Imeruhusu mchungaji Ambilikile Mwasapile – Babu wa Loliondo – kuendelea kufanya tiba kwa kutumia dawa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka yoyote ya serikali.

Kuanzia wizarani, mkoani, wilayani, tarafani, hadi kijijini, serikali imebariki mchungaji Mwasapile kufanya kazi za kitabibu, huku yenyewe ikitumia muda mwingi kumtangaza.

Mkolezo wa hatua ya serikali unaongezwa na baadhi ya maaskofu na wachungaji ili kutoa ushuhuda. Baadhi ya walioajiriwa tayari wametoa ushuhuda, kwamba dawa inayotolewa inafanya kazi bila matatizo.

Kitendo cha serikali kutoa kibali kwa “Babu wa Loliondo,” na kutumia rasilimali za taifa na muda kutetea kinachotendeka, ni mkwamo wa aina yake.

Katika mazigira ya kawaida, serikali au chombo chochote kinachoshughulika na huduma za umma, kilipaswa kujiweka mbali na imani hizi.

Kwa mfano, serikali ingeweza kusema, “wanaotaka kwenda kwa mchungaji Loliondo ruhusa, bali “tiba ya ukimwi haijapatikana.” Haikufanya hivyo. Badala yake, imeruhusu taifa kurejea katika ujima.

Kushindwa kwa serikali kuingilia “tiba ya babu” kumetokana na mchoko wa kupigwa mbele, nyuma, kushoto na kulia. Hivyo imehofu kuonekana inapuuza wananchi.

Hata hivyo, hatua ya serikali kushabikia kile kinachoitwa “tiba ya imani,” ni sawa na kushindilia mwiba mwilini badala ya kuung’oa.

Mchungaji Mwasapile anasema dawa yake inayotokana na mizizi na magamba ya mti unaoitwa Muugamuryaga, kwa lugha ya kabila la Kisonjo, ambalo ndiyo wenyeji wa tarafa ya Sale, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, inatibu maradhi sugu ya kisukari, ukimwi, saratani na kifua kikuu.

Sasa serikali imejipa kazi ya ziada na iliyopo nje ya mipango yake ya bajeti. Kwanza, imetumia muda mwingi kutangaza kazi za “babu wa Loliondo” kuliko kutenda kazi zake.

Kwa muda wa wiki mzima mawaziri wa Kikwete, waziri wa afya na ustawi wa jamii, Dk. Haji Mponda na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (sera, uratibu na bunge) William Lukuvi, wamefanya kazi kubwa ya kumtangaza mchungaji.

Wakati Dk. Haji akitaka kusitishwa kwa muda kwa huduma zinazotolewa kwa kuwa dawa hiyo haijathibitishwa, Lukuvi alinukuliwa akisema serikali haiwezi kuingilia imani za dini za watu kwa kuwa si sera yake.

Hapa napo kuna tatizo la uelewa. Babu hajaongelea suala la dini. Anashughulika na imani. Ndiyo maana kila mwamini na muumini anayetishiwa na maradhi aliyotaja anakwenda kwake. Angehubiri dini asingekuwa na mtu.

Hata hivyo, Lukuvi alikiri kuwa serikali haifahamu lolote kama dawa inayotolewa ni salama kwa afya ya watu wake. Alisema kazi ya kuichunguza dawa hiyo inayofanywa na wataalamu wa serikali, bado haijakamilika.

Pili, serikali imelazimika kupeleka kwa “babu” manesi ili kusaidia kazi za kitabibu. Hawa si manesi kutoka hospitali binafsi – hao hawaamini katika yale yanayotendeka – ni manesi kutoka hospitali za umma. 

Tatu, nje ya mipango yake ya bajeti, serikali imepeleka askari polisi kuimarisha kazi ya ulinzi. Imegharimia usafiri wa watendaji na zana za kazi.

Lakini hatujaona serikali inayoamini dawa ya “Babu wa Loliondo” ikiondoa wagonjwa wa kansa waliojazana katika hospitali ya Ocean Road na kuwapeleka huko kupata matibabu. Wala hatujaona serikali ikichukua helikopta kumbeba “mtu wa Mungu” na kumpeleka Ocean Road akiwa na gudulia lake, kunywesha dawa wagonjwa.

Mkakati huu ungesaidia kupunguza msongamano Loliondo; ungesaidia  serikali kupunguza gharana za kuhudumia wagonjwa waliopo hospitali na ungeifanya serikali ifanye kazi nyingine muhimu za utawala. Kwa nini sasa hospitali zijae wagonjwa, wakati maji ya dawa yapo?

Serikali imeshindwa kumsajili babu ili iweze kupata mapato. Taarifa zinasema kila siku ya Mungu, “Babu wa Loliondo” anakusanya kati ya Sh. 5 milioni na Sh. 20 milioni. Kwa hesabu hii, serikali inapoteza karibu zaidi ya Sh. 2 milioni kwa siku.

Lakini kuna hili pia: Umuhimu wa habari za tiba ya Loliondo unachangiwa na habari za uvumi zinazoeleza mambo kadhaa bila uthibitisho. Kwa mfano, kuna taarifa kuwa baadhi ya vigogo serikalini wameishakwenda huko kupokea tiba; majina yao yanatajwa lakini hayaripotiwi kwenye vyombo vya habari.

Uvumi huu unanogesha soga na kuongeza hamasa ya kwenda Loliondo. Mpaka sasa hakuna mtu aliyepona na kujitokeza hadharani kutoa ushahidi juu ya tiba hiyo. Nyingi ya habari zinazotoka zinanukuu watu wengine wanaodaiwa kupona.

Ni kweli kwamba masuala ya imani yana mipaka isiyoweza kuvukwa na mtu yeyote asiyekubaliana na mambo ya imani, lakini kwa kuwa serikali nayo inaumwa, na kwa hiyo imeamua kwenda Loliondo kutibiwa, hatunabudi kuhoji hicho kinachotendeka.

Kimsingi mwitikio wa watu kuhusu tiba ya Loliondo unaashiria mambo mengi katika taifa. Kinachojitokeza wazi ni ukweli kuwa huduma za afya katika taifa ni mbaya mno.

Pamoja na mezoea kuwa huduma hizi ni mbaya kwa watu maskini na wa vijijini, lakini sasa imedhihirika kuwa ni mbaya kwa wengi zaidi. Taarifa zimetaja hata baadhi ya wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara wakubwa kuwa wanakwenda Loliondo.

Wenye fedha na nafasi ndani ya taifa, ambao walizoea kwenda Ulaya na India kupata tiba ya saratani, ukimwi, shinikizo la damu na kisukari, wengi wao wanaripotiwa kunywa dawa ya babu.

Fedha nyingi ambazo zingetumika kuboresha huduma za afya katika taifa, zimekuwa zinatumika kwenda nje ya nchi, lakini bado walewale waliozoea kukomba fedha za umma kwenda nje, wanamiminika Loliondo.

Wakati naandika makala hii, rafiki yangu mmoja alinitumia ujumbe wa simu ya mkononi, uliosheheni utani unaoweza kufanana na ukweli. Ulisema, “Usione kimya, niko kwenye foleni Loliondo toka Jumanne. Namba yangu ni 1561. Huku hakuna kuzamia. Ukizamia au kutoa rushwa hauponi.”

Anasema, “Nyuma yangu namwona mheshimiwa Ole Sendeka, Halima Mdee, Anne Kilango, Tundu Lissu na Rostam Aziz ambaye taarifa zinasema amekuja kuganga Dowans yake ili inunuliwe…Huwezi kuamini hata Mzee wa Upako yuko hapa. Naye ni mtu wa 1569.

“Mama Rwakatare ni wa 1621. Nitakuwa nakujuza kila kitu, ila network (mtandao) ni shida sana. Kwa mbali namwona Shibuda (John Shibuda), Mbowe (Freeman Mbowe), Samwel Sitta na Athony Diallo wamekamata kikombe. Tafadhali njoo na wewe.”

Ni utani. Utani mtupu unaoenea kwa kasi mitaani, lakini ni jambo linaloweza kutokea endapo serikali itaendelea kukumbatia mchungaji kutaka kuponyesha raia wake huku yenyewe ikishindwa kuchukua hatua za haraka kuboresha hospitali zake na vituo vyake vya afya.

Sasa serikali imeamua kukimbilia Loliondo kana kwamba Mchungaji Mwasapile anatibu ufisadi. Iliishatamkwa kuwa ufisadi hauna dini wala rangi na kwa hiyo, ufisadi hauna imani kwa Mungu.

Mchungaji Mwasapile anatibu kwa imani. Je, mafisadi wamepata imani lini ya kuweza kuponyeshwa na tiba ya Loliondo? Tusubiri tuone.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)