Serikali inataka kuleta vita


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Vurugu uchaguzi wa Kenya 2007

KATIKA nchi jirani – Kenya, Tume ya Uchaguzi iliacha kazi yake ya kusimamia uchaguzi na badala yake ikafanya kazi ya kuteua rais.

Hiyo ilikuwa mwaka 2007, wakati wa uchaguzi mkuu. Kilichofuatia ni kutoaminiana, kushutumiana, kupigana na kuuana.

Mwaka huu, nchini Tanzania – hasa wiki iliyopita – serikali iliacha shughuli zake za kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira huru na kujiingiza katika uteuzi wa rais.

Kupitia gazeti lake linalotolewa kwa lugha ya Kiingereza, Daily News, serikali ilisema kupitia safu ya maoni, kuwa mgombea urais anayechachafya rais aliyemaliza muda wake, hawezi kushinda.

Serikali imesema, “…Na ukweli ni kwamba Dk. Willibrod Slaa hatakuwa rais wa tano wa Tanzania…”

Kwa kauli hiyo, serikali inajua, na huenda bila mashaka yoyote, nani atakuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kauli hiyo, serikali imemaliza “uteuzi” wake wa rais ajaye na imejiandaa kuiambia tume ya uchaguzi, kutangaza jina la yule ambaye imeona anastahili.

Kama ilivyokuwa Kenya, upande mmoja wa washindani unaweza kuomba, kubembeleza, kutishia na hata kulazimisha Tume kutangaza yule ambaye unataka awe rais.

Katika mazingira ambamo mgombea wa chama chenye serikali amekabwa koo katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea, uamuzi wa serikali kutangaza aliyeshindwa, una maana ya kujitangaza mshindi.

Kauli ya serikali, siku 36 kabla ya kupiga kura, una maana ya kuingilia kazi za Tume na kuandaa mazingira ya ushindani nje ya vituo vya kupigia kura.

Kitendo cha serikali kinaonyesha mengi zaidi. Kinaonyesha kuwa serikali imejiandaa kwa kila hali, kuingia katika ushindani na vyama na kutwaa ushindi kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Gazeti la Daily News halihitaji kunukuu msemaji mwingine wa serikali, kwani lenyewe ndilo chombo teule cha kueleza maoni, utashi, amri na matarajio ya serikali.

Huwezi kutegemea gazeti la serikali kusema zaidi ya haya. Hapa limemaliza kazi yake. Linatoa msimamo wa mwisho wa serikali na linasisitiza, “…na hivyo ndivyo itakavyokuwa na kwa hili, vyombo vya habari vinavyomuunga mkono kasisi huyo wa zamani, vinaweza kutunukuu.”

Katika tafsiri ya kawaida, gazeti la Daily News limepandikiza shaka, woga, ghadhabu, hasira, chuki, mifarakano; na hasa limejenga mazingira ya kukwaruzana na hata kupigana.

Serikali imefanya kazi ya Tume, lakini imeifanya kabla muda wake haujatimia. Bado tume inafanya usimamizi – inaandaa taratibu na kutekeleza kanuni muhimu kuelekea uchaguzi mkuu.

Tume inajua kuwa muda wa kutangaza aliyeshindwa au aliyeshinda, siyo leo wala kesho. Ni baada ya uchaguzi wa 31 Oktoba.

Hii ina maana kwamba serikali imeingilia kazi ya Tume. Imevuruga kazi ya Tume. Ama inataka Tume isusie kazi hii na serikali iendelee kuwa madarakani, au inataka Tume itishike na kufanya kama serikali inavyotaka.
Serikali imejenga mazingira yanayoweza kufanya vyama vya siasa kususia uchaguzi na kutaka kuanza upya. Au inataka vyama vingine viungane nayo katika kuangamiza Chadema.

Hili likifanyika, serikali itakuwa imefaulu kuchora mipaka ya ushawishi na kuunda mashabiki kwa nia ya kujihami kuangamiza wale ambao wanaona wanakaba koo mama (baba) yao – CCM.

Ni hatua hii ambayo imezingatiwa hapo juu, kwamba inapandikiza ghadhabu, inajenga makundi na kuyachochea hasira; inakaribisha maafa katika nchi.

Serikali imepata wapi mshindi kabla ya uchaguzi? Kauli ya kushinda na kushindwa ikitamkwa na chama, hakika inaweza kueleweka; na vyama vimekuwa vikiitoa.

Lakini kwa serikali kutamka aliyeshindwa, mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, ni kutaka kusimamisha mchakato wa uchaguzi na kuleta vita nchini.

Nani aiadabishe serikali? Tume ya Uchaguzi? Je, Tume yenyewe inatambua kuwa dude hili linaloitwa serikali limeingia katika mbuga zake na kutenda uhalifu?

Je, Tume inajua kiwango cha uharibifu kilicholetwa na serikali? Inajua madhara ya serikali ndani ya nyoyo za wapigakura? Inajua wapigakura hivi sasa wanapanga nini?

Unafahamu kitendo cha serikali kimeelekeza nini ndani ya wanaopigania mabadiliko?

Ni kweli kwamba Tume imeundwa na serikali. Lakini inaongozwa na watu binafsi wenye akili nzuri na wanaojitegemea katika kufikiri na kutenda. Sasa wafikiri na kutenda kama jamii inavyowatarajia.

Ni juzi tu Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amejiigiza katika kazi ya Tume na kutetea uvunjaji kanuni za uchaguzi uliofanywa na mgombea urais wa CCM. Inaonekana huu ulikuwa mwanzo wa serikali kutenda uhalifu.

Kwa njia hii na kwa kauli na vitendo vya sasa, Watanzania wanaweza kuanza kuelewa kuwa mengi, makubwa, machafu na hatari yanakuja.

Matendo haya ni maandalizi ya vurugu ambayo bahati mbaya chanzo chake ni serikali inayoogopa kushindana; lakini inayoteseka kila ikifikiria kushindwa.

Kauli ya serikali ni ishara ya maandalizi machafu na katili pindi matakwa yake yatakapokuwa tofauti na matokeo.

Yawezekana kuna maandalizi makubwa zaidi, hata magwaride ya siri na kimyakimya. Mwaka 1995 yalianikwa mengi – virungu na mabomu mapya ya machozi yenye sumu kali zaidi yaliyonunuliwa kutoka Ulaya.

Woga umetamalaki. Waliotawala kwa miaka 50 wanaanza kukosa pumzi. Wanafyatuka kwa kauli zinazofichua siri zao. Bali waliyotenda hayasameheki kwa kuwa yanalenga kuleta uhasama na hata vita.

Serikali imewakosea wananchi wapigakura. Sharti ikiri kufanya makosa. Iungame kwa wananchi iliowaelekezea vitisho. Iahidi kutotenda uhalifu wa aina hii tena.

Tangu mwaka 1985, waandishi wenye uelewa mpana wameishauri serikali kuachana na miliki ya vyombo vya habari ambavyo imetumia kujiremba na hata kushambulia wengine.

Serikali imetumia vyombo vyake kugawa wanataaluma kiasi kwamba kumekuwa na uandishi wa habari wa aina ya serikali na ule wa vyombo vinavyomilikiwa na makampuni binafsi.

Ni miliki hii inayofanya serikali ikose uadilifu. Huku inafanya biashara ya habari huku inatunga sheria za kuumiza na hata kuua vyombo vya habari vya binafsi – mgongano wa maslahi.

Huenda hata hili la leo lisingetokea kama sio kwa vijimbweneleni katika taaluma na ndani ya serikali visingekuwa vinatafuta kujitutumia na kupalilia uteuzi katika utukufu wa kisiasa.

Serikali iombe radhi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: