Serikali inataka kutunyongea gizani, kimyakimya


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Gumzo

SERIKALI imeleta barazani pendekezo ambalo halikubaliki kuhusu umiliki wa vyombo vya habari. Likitekelezwa itakuwa kwa shuruti tu.

Pendekezo lenyewe ni hili: Kwamba mtu mmoja ataruhusiwa “kumiliki aina moja tu ya chombo cha habari, kama ni magazeti, au redio au televisheni, na siyo vyote kwa wakati mmoja.”

Serikali inapendekeza kuwa wenye aina zote tatu za vyombo vya habari – magazeti, redio na televisheni, wapewe “muda wa miaka mitano kuuza hisa” za vyombo vyao vya aina nyingine na kubaki na aina moja tu.

Hayo ndiyo mapendekezo ya serikali kwenye Sera ya Habari ya Mwaka 2003. Mwenye kudadisi haraka atajua kuwa serikali inamiliki magazeti, redio na televisheni.

Kwa mujibu wa muundo, kanuni na taratibu nchini, vinavyoitwa vyombo vya umma, hakika ni vyombo vya serikali. Uanzishwaji, uendeshaji, uwajibikaji na hata ugharimiaji wake, vyote ni kwa mfumo wa kumilikiwa na serikali na siyo “umma.”

Mateka wa kwanza basi sharti awe serikali ambayo kwa jina la “umma” inamiliki redio, televisheni na magazeti. Haitauza hisa zake, kama zipo. Huo ndio mgongano wa kwanza wa maslahi katika utekelezaji kwa upande wa serikali.

Kwa takribani miaka 24 sasa, baadhi yetu tumetaka serikali iachie vyombo vya habari inavyomiliki ili iandikwe na kutangazwa kama inavyoonekana na siyo kwa kurembwa, kuonewa haya au inavyotaka. Serikali imekataa.

Tumependekeza serikali iache kumiliki vyombo vya habari ndipo itapata hadhi na uhalali wa kuvisema na kuvikosoa, badala ya mtindo wa sasa ambapo serikali ni mshindani kama wengine lakini inatumia nafasi yake kukandamiza mshindani mwenzake. Na hapa kuna kipengele cha utovu wa utawala bora.

Serikali imekataa. Imebaki mmiliki wa vyombo vya habari; msajili wa vyombo vya habari, mtunga sera, msimamizi wa sera, mdhibiti wa vyombo vya habari na bado mshindani miongoni mwa wenye vyombo vya habari. Mgongano wa maslahi.

Mapendekezo ya serikali yanaonekana kulenga mtu mmoja au wawili wenye kumiliki aina nne za vyombo vya habari – redio, televisheni, magazeti na shirika la habari.

Hata hivyo, katika haraka ya serikali ya kudhibiti iliowalenga, haitaji Shirika la Habari kuwa aina nyingine ya chombo cha habari katika kifungu 2.3.2 kinachosomeka, “Maelekezo ya Sera.”

Haihitajiki busara ya nyongeza kuona kuwa mapendekezo yamelenga Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP na Media Solutions anayemiliki redio, televisheni na msululu wa magazeti.

Baadhi ya magazeti ya Mengi yamekuwa na msimamo mkali wa kukosoa utendaji serikalini na kuibua taarifa za rushwa na ufisadi.

Mwingine ni Anthony Diallo, mwenye aina tatu za vyombo vya habari ambaye anamiliki makampuni ya  Sahara Communications yenye redio, televisheni na gazeti moja.

Katika siku za hivi karibuni ni Reginald Mengi ambaye amelalamikiwa na serikali kwa kuipa nguvu hoja ya ufisadi nchini. Ameibuka na majina ya watu watano aliowaita “mafisadi papa.”

Hoja ya Mengi ilipojibiwa na mmoja wa waliotuhumiwa, Rostam Aziz, naye Waziri wa Habari George Mkuchika akaibuka na kudai kufunga mjadala huo kwa madai kuwa mjadala unataka “kuligawa taifa.”

Vyombo vya habari vya IPP na Media Solutions, hasa magazeti – This Day, KuliKoni na Nipashe – vimejizolea tuzo katika ushindani wa kuandika habari za uchunguzi katika rushwa na utawala bora.

Aidha, ni vyombo vya IPP, hasa televisheni, ambayo imemulika hata kelele za chinichini na mikwaruzo kati na baina ya wabunge na kutoa mwanya kwa wengi kujieleza, ambao bila chombo hicho, wangepotea kimyakimya kutoka jukwaa la siasa.

Mapendekezo ya serikali basi, yanalenga kuzima nguvu ya vyombo hivyo; mvumo na mfumo wake ratibishi na hatimaye kurejesha taifa katika usiku wa giza nene la upungufu na hata ukosefu wa taarifa ambazo, bila vyombo hivyo zisingepatikana.

Serikali inalenga kuua stadi na uwezo wa viwango ainaaina wa watumishi katika vyombo hivi; kwani pamoja na kupendekeza kuwa wenye aina zote tatu wauze hisa za aina nyingine mbili za vyombo vya habari, hakuna mwenye hakika ya vyombo vilivyouzwa kuendelea kukua, kushamiri na kutumika kwa malengo na manufaa yaliyotarajiwa.

Hapa kuna mkakati wa kuua ajira ya mamia, kama siyo maelfu, ya wafanyakazi wanaotegemea vyombo hivi na wengi wanaotegemea mafao yatokanayo na mishahara ya watumishi katika vyombo hivi.

Mapendekezo ya serikali katika sera yanalenga kuzima ujasiri katika uandishi wa habari za uchunguzi; ujasiri uliopatikana baada ya muda mrefu wa mafunzo darasani na kwa njia ya vitendo.

Haya ni mapendekezo maalum ya kuzima ushindani wa kibiashara kati ya vyombo vya habari vya serikali na vyombo binafsi na kurejesha wananchi katika mazingira ya kutokuwa na utashi juu ya chombo gani wanataka kiwape habari na taarifa.

Mapendekezo yanalenga kukatisha tamaa na kuogofya wale ambao tayari walikuwa wamehamasika na wanataka kuanzisha vyombo vingine vya habari.

Hatua ya serikali kupitia mapendekezo, inalenga kupunguza kiwango cha taarifa zilizokuwa zinawafikia wananchi. Hii ina maana ya kujenga mazingira ya uficho zaidi kwa serikali na watendaji wake. Uko wapi uwazi bila vyombo vingi vya kuuweka wazi?

Hatari kubwa ipo kwenye uhuru wa maoni. Hapo ndipo kuna janga. Kuwepo kwa vyombo vingi vya habari kunaweka mazingira ya wananchi wengi kutoa na kupata habari na taarifa; kubadilishana mawazo, kuelimishwa na kuelimishana na kuwa na maoni yao juu ya mambo mbalimbali.

Sauti nyingi za wananchi juu ya wanavyoona utawala na wanavyotaka uwe; juu ya furaha, huzuni, pongezi, malalamiko, vilio, shangwe na maafa, huweza kufika kwa wenzao na watawala kama kuna vyombo vingi vya habari.

Kupunguza idadi ya vyombo vya habari katika mazingira ya sasa, ni kutaka kuziba mifereji ya fikra na elimu; ni kutoa mwanya kwa uvumi na ujinga; ni kutaka wananchi wasikilize sauti moja kutoka kileleni; ni kuzika wananchi wakiwa hai katika mazingira ambamo hawatasikika wakipambana au wakilia na kuomba msaada.

Turudi darasani kidogo na kwenye uzoefu. Uhuru wa maoni kwa maana ya uhuru wa kujieleza, haukamiliki mpaka mtu aseme maoni yake – kwa kauli au vitendo.

Ni mpaka maoni yake yasikike kwa mwenzake, kundi au halaiki; au yachapishwe kwenye gazeti, au yatangazwe kwenye redio au televisheni. Vyombo vya habari ndivyo husaidia kukamilika kwa takwa la uhuru wa maoni na ndio maana vyombo hivyo ni sehemu ya uhuru wa kujieleza.

Sasa serikali inapendekeza wenye vyombo waviuze. Labda wanao wanunuzi. Wamuuzie nani ambaye ataviendesha kama vilivyokuwa vinaendeshwa. Mapendekezo haya ndiyo yanatarajiwa kuwa katika sheria mpya ya uhuru wa habari na uhuru wa kupata habari. Hii ni hatari.

Kama pendekezo la serikali litapitishwa na wadau, au litashinikizwa, sheria itakayotokana na sera hii itakuwa moja ya sheria za kishetani ambazo wadau wa habari wamepinga tangu 1985.

Bali kuna masomo mawili yanayopatikana hapa. Kwanza, pendekezo la serikali, ikiwa mdau katika huduma na biashara ya habari, linadhihirisha kuwa imeshindwa mbinu za ushindani na sasa imeamua kutumia mabavu kwa njia ya sera na sheria.

Pili, serikali imejipanga kuingilia uhuru wa wananchi wa kupata habari na kuwa na maoni. Itafanya hivyo kwa kuviondoa vyombo vya habari ambavyo tayari vilikuwa vimepenya jamii na vinakimbiliwa na wengi ili kutoa taarifa.

Mapendekezo ya serikali hayakubaliki na kila mwenye nia njema kwa taifa hili anaitaka serikali iyatupilie mbali. Inabidi hata walioyaleta wajue kuwa wao siyo wapangaji wa kudumu serikalini. Zimwi wanalojaribu kuumba watalikuta nje ya lango pindi wakiachishwa, wakifukuzwa kazi au wakistaafu.

Serikali ingejizolea heshima kwa kuhimiza watu binafsi na asasi mbambali kuanzisha magazeti mengi na vituo vingi vya redio na televisheni, bila kujali nani ana vyombo vya aina zipi. Kinachohitajika ni taifa linaloongea; na siyo la watu walionyang’anywa uwezo wa kuwa na maoni na vyombo vya kutolea maoni hayo.

Hivi kwa nini mtu akatae kujiandalia mazingira mazuri ya uhuru uliotamalaki na badala yake  ajiandalie mahabusi akingali madarakani? Tusikubali vipofu wajinyonge. Tuwanyang’anye vitanzi.

0
No votes yet