Serikali inatazamwa inavyookoa mafisadi


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 27 May 2008

Printer-friendly version
Kifo cha Ballali

BALLALI... Ballali... Ballali. Nadhani hakuna jina la mtu maarufu nchini, tukiliacha la Rais Jakaya Kikwete, linalotamkwa na kuandikwa magazetini mara nyingi katika muda mfupi chini ya mwaka mmoja sasa kama la Daud Ballali, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ambaye sasa ni marehemu.

Sidhani kama yupo anayepinga hili pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayeshangaa kwa vipi hali iwe hivyo.

Anashangaa kwa nini Ballali alitokea kuwa mtu "maarufu" nchini katika miezi michache iliyopita na "umaarufu" wake kuzidi hata baada ya kufariki. Labda Waziri Membe alitarajia baada ya kufa, Watanzania wanmsahau haraka.

Picha hii ndiyo inayopatikana kama mtu atachunguza kwa karibu kauli ya Waziri huyo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.

Akitaka wananchi wamwone Ballali kama Mtanzania mwingine yeyote aliyefia nchi za nje na kuzikwa huko, na yumkini alisema "wako wengi wa namna hiyo." Kwa bahati mbaya, Ballali yu tofauti.

Akitoa msimamo wa serikali kujibu minonong'ono inayoendelea, na hisia zinazojijenga kwamba serikali inapaswa kubeba mzigo, kwa namna moja au nyingine inahusika na kifo cha Ballali, alikanusha akisema serikali haihusiki kwa namna yoyote ile.

Pia alitoa changamoto kwa mtu yeyote mwenye ushahidi wa hoja hiyo ajitokeze kuutoa.

Watanzania wamezoea kusikia serikali ikitoa kauli hizo za kutaka "mwenye ushahidi autoe" na serikali ya awamu ya nne imetumia hilo kama chaka la kuficha uwajibikaji pale inapoandamwa kuhusu tuhuma mbalimbali.

Serikali inapenda kujitoa katika wajibu wa kueleza mambo kwa uwazi huku viongozi wake wakisema "jitihada zinaendelea kuchukuliwa" au tusubiri "uchunguzi ukamilike."

Na vyombo vinavyochunguza vimethibitisha udhaifu katika kutena kwa udhati na vimekosa majibu yanayolenga kutatua tatizo liliopo. Tuache hapo, bora turudi kwenye suala la Ballali.

Hisia za wananchi kwa serikali ni hizohizo na sababu yake kubwa ni danadana inazopiga. Kuhusika kwake kwa namna moja au nyingine na kifo cha Ballali hakuepukiki kama ambavyo ilibanwa kueleza tangu wakati wa ugonjwa wake iseme anaumwa nini na lini atarudishwa nchini.

Kilichochochea umma utake kufahamu taarifa zinazomhusu Ballali, ni kimoja tu: amekuwa akitajwa kama mtu muhimu katika tuhuma za ufisadi wa Sh. 133 bilioni zilizoibwa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na tuhuma za kupaishwa kwa gharama za ujenzi wa majengo pacha ya Benki hiyo, Makao Makuu.

Na tuhuma hizo si kwamba zilimhusu Ballali tu, watu wengine wakiwemo viongozi wa juu wa serikali na washirika (au maswahiba wao) wao kama walivyobainisha maodita wa Ernst&Young.

Katika masuala hayo, lazima kuna pande mbili kuu haiwezekani Ballali akawa ndiye "mhalifu" pekee kama ilivyobainishwa na ripoti ya wakaguzi hao ambayo ilichochea afukuzwe kazi na Rais 8 Januari, mwaka huu, wiki kadhaa baada ya kuvuja taarifa kuwa alishaomba kujiuzulu.

Lakini ushahidi wa nguvu kabisa wa kimazingira unaonyesha Ballali alikuwa mtu muhimu katika ushahidi wa kesi ambazo zingekuja kufunguliwa na serikali kuhusu ufisadi katika EPA.

Serikali haiwezi kusema ilikuwa na shauku hiyo, na upungufu huu unatokana na mwenendo wa uchunguzi unaofanywa na taasisi zake ikiwemo Timu aliyoiunda Rais chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.

Kisingizio cha serikali ni kwamba cha muhimu zaidi kwa hapo, ilikuwa kurudisha fedha zilizoibwa na baadaye ikasema urudishaji ulikuwa unakwenda vizuri. Lakini bado haikuona umuhimu kutaja wanaorudisha fedha hizo.

Wananchi wanahisi kwa vile urudishaji fedha unafanywa kwa siri kubwa, bila ya shaka wahusika wakuu watafichwa, ukiachia mbali wale waliotajwa katika ile "mikataba ya wizi" ya EPA, ambao ni watu wadogowadogo waliotumiwa na wahusika wakuu.

Masuala ya mahakamani yanaweza kuiumbua serikali kwani haitaweza tena kuzuia kitakachosemwa. Hata hivyo, serikali inajua fika katika masuala ya kesi za jinai, yenyewe ndiyo "mshitaki mkuu" kwa hivyo ndiyo iliyoshika mpini.

Ina uwezo wa kupeleka au kutopeleka kesi mahakamani, na pia ina uwezo wa kuifuta kesi yoyote itakayokuwa imefungua.

Kwa hivyo, utaona jinsi Ballali alivyokuwa anaikalia vibaya serikali - alikuwa kama mwiba kooni hasa iwapo angeweza kurejeshwa nchini kueleza anachokijua kuhusu ufisadi katika EPA.

Ajabu ni kwamba serikali haikuwa inaficha hili kamwe kwani kama wiki moja tu kabla ya kufariki kwa Ballali, ilitamka waziwazi haikuwa inamhitaji Ballali kwa wakati huu, maana kama ingekuwa inamtaka "ingempata" au "itampata tu."

Kauli hii ilishangaza wengi na kukasirisha wanaharakati wengi waliokuwa wanadhani serikali iko pamoja nao bega kwa bega katika suala la vita dhidi ya ufisadi, na kumbe sivyo.

Na kutangazwa kufa kwa Ballali siku chache tu baada ya kauli hii kulileta hisia kuwa serikali ilikuwa inajua ilichokuwa inakisema kwamba "haikuwa inamhitaji Ballali." Ilikuwa inajua kifo chake ki tayari.

Kama kuna upande "uliofaidika" na kifo cha Ballali, basi ni serikali na mafisadi ambao tunaambiwa wanapumua kwa kuamini ushahidi muhimu umetoweka naye.

Ni sawasa na suala la rada kwani serikali haitaki kumwona nchini Saileshi Vithlani shahidi mkuu katika dili hiyo iliyothibitishwa kujaa ufisadi. Lengo la kutomtaka huyo hapa nchini ni kuwaponesha jela wakuu wote wale waliopewa migao wa mlungula ktoka kampuni ya Uingereza ya BAE iliyoiuzia Tanzania mtambo huo.

Inapasa Membe atambuwe kwamba wananchi hawaoni matokeo yoyote ya vita dhidi ya ufisadi na badala yake wanaiangalia sana serikali na harakati zake za kuokoa "mafisadi."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: