Serikali ishitaki RITES kwa kuhujumu TRL


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

“WA moja havai mbili hata akivaa humdondoka” ni msemo ambao aghalabu hutumiwa na watu mitaani hasa pale wanapotambiana juu ya nafasi zao katika jamii. Msemo huo hutumiwa kama jibu la kukata ngebe za watu wanaokinzana, yawezekana kwa sababu za kuoneana choyo au kijicho katika ustawi wa maisha.

Ingawa misemo kama hii ni maarufu zaidi kwa akina mama hasa wanapoumbuana mitaani, wiki hii nimetafakari nikafikiri kwamba unafaa kabisa kutumiwa kitaifa. Kwamba sisi kama taifa ni wa kuvaa moja, hata kama tukibahatisha tukapata mbili, hatuwezi kuimudu itatudondoka tu. Kwa maneno mengine sisi ni watu wa kubakia tulivyo tu. Tumebaki kuwa watu wa kuliwa, kuibiwa, kurubuniwa hata tufanye nini. Hiyo ndiyo Tanzania yetu.

Mwishoni mwa wiki Baraza la Mawaziri lilitoa maamuzi juu ya mustakabali wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL). Taarifa hiyo ambayo ilikuwa fupi sana kama zilivyo taarifa nyeti za serikali kwa umma ambazo hazipendi kuzungumza kwa kina hali ilivyo, ilikuwa hivi:

“Baraza la Mawaziri leo, Ijumaa, Machi 12, 2010, katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam, chini ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limejadili hali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kufanya maamuzi ya msingi kwa kukubaliana kama ifuatavyo:

  1. Kwamba Serikali ianze mara moja kujadiliana na RITES, mbia wa Serikali katika kampuni ya TRL, kwa lengo la Serikali kununua hisa 51 za RITES katika kampuni hiyo. Kwa sasa RITES inamiliki asilimia 51 na Serikali inamiliki asilimia 49 katika TRL.
  2. Kwamba baada ya hapo, Serikali itafanya matayarisho ya msingi ikiwa ni pamoja na kurekebisha kasoro na kuangalia mustakabali wa TRL, na kuiandaa kampuni hiyo kwa ajili ya kutafutiwa mbia mwingine wa kushirikiana na Serikali katika kuendesha TRL.

Kinachozungumzwa kwenye taarifa ya serikali ambayo ilisainiwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri, Philemon Luhanjo, ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi, ni kuvunjwa kwa mkataba wa serikali na RITES katika kuendesha TRL, lakini wakati huo huo serikali kujipanga kununua hisa asilimia 51 za TRL!

Serikali imefikia hatua hiyo kwa sasa baada ya kuwepo kilio cha muda mrefu juu ya uwezo wa RITES; kilio hiki kimetoka katika makundi mbalimbali.

Wapo wananchi wa kawaida, wapo wafanyakazi wa TRL wenyewe ambao wamefichua vitendo vingi vya hujuma vilivyokuwa vikifanywa ndani ya shirika hilo, lakini kubwa zaidi hata wabunge walifikia hatua ya kutoa azimio lililotokana na hoja binafsi ya mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi juu ya kudorora kwa huduma za TRL.

Kumekuwa na kurushiana mpira kwa muda mrefu mno juu ya uendeshaji wa TRL huku serikali ikijaribu kukwepa wajibu wake muhimu wa kutambua kama kweli mbia aliyepatikana yaani RITES ndiye aliyekuwa anafaa kwa ajili ya kazi hiyo au zilikuwa harakati nyingine za kuingia mikataba kichwachwa kama ambavyo imekuwa ni jadi yetu.

Tangu siku ya kwanza ya mkataba huu kufikiwa kulikuwa na kila dalili kwamba taifa lilikuwa limeliwa kama ambavyo lililiwa kwenye mikataba mingine yote ama ya kubinafsha au kuingia ubia katika uendeshaji wa mashirika ya umma. Tulifanyiwa hivyo hivyo NBC, TBL, TTCL, ATCL na kwa ujumla uuzaji au ukodishaji wa hoteli zote zilizokuwa zinasimamiwa na bodi ya utalii nchini.

Hatuna nafuu hata moja, kila mkataba tuliliwa, tumeendelea kuliwa tangu awamu ya pili, ikaja awamu tatu na sasa awamu ya nne; hakuna tulikopona. Sisi ni wa kuvaa moja, tukipewa au kuokota ya pili itatudondoka tu!

Huo ndio ukweli. Lakini katikati ya ukweli huu tunapata fadhaa kubwa eti “Kwamba Serikali ianze mara moja kujadiliana na RITES, mbia wa Serikali katika kampuni ya TRL, kwa lengo la Serikali kununua hisa 51 za RITES katika kampuni hiyo. Kwa sasa RITES inamiliki asilimia 51 na Serikali inamiliki asilimia 49 katika TRL” tunashindwa kujua kwamba inataka kununua nini?

Katika vitu ambavyo vimeifikisha TRL hapo ilipo leo ni kushindwa kabisa kwa mbia kuwekeza chochote katika kampuni hii, RITES hawajalipa fedha yoyote ya kupewa hisa asilimia 51 mpaka leo; kama kuna sehemu RITES walilipa umma unataka uelezwe, lakini hadi sasa taarifa za ndani ya TRL zinasema kwamba hakuna mahali popote ambapo RITES walilipa fedha, hakuna senti moja iliyolipwa!

La pili na lenye umuhimu kama hilo, ni ukweli kwamba hakuna mahali ambapo RITES wamewekeza kwenye TRL kwa maana ya uwekezaji; kilichotokea ni kujaribu kuleta mabehewa yaliyochakaa ya mwaka 47 baada ya kuyakarabati yakiwa ni sawa tu na uchafu usiohitajika tena huko India, lakini wakati huo wakiyafanyia hujuma mabehewa ya TRC yaliyokuwako miaka mingi; hawakutaka kuyakarabati; walikataa kukarabati hata injini za treni zilizokuwako na badala yake wakawa wanaleta vichwa vya treni ambavyo havina uwezo wa kuvuta mabehewa hapa nchini.

Kwa muda wote TRL chini ya menejimenti ya RITES ilishindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi, wafanyakazi hawa walikuwa wakiishi kwa ruzuku ya kodi ya wananchi wote, hizi ni fedha za wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara; ni fedha za kila avujaye jasho na kulipa kodi. RITES hawakuleta ufanisi wowote TRL, hawakuweza kurithisha tekinolojia yoyote TRL, wafanyakazi waliamua kuasi na kujituma kwa nguvu kukarabati mabehewa ambayo RITES hawakutaka yakarabatiwe kwa kuwa walitaka kujenga soko la mabehewa makukuu ya kwao kutoka India .

Katika hali kama hii kauli ya ‘kununua hisa’ inapotamkwa na Baraza la Mawaziri, umma unapata fadhaa. Unashindwa kujua ni lini hasa tutapona ugonjwa huu wa kuibiwa na wasimamizi wa wizi huu wakiwa ni watu waliopewa dhamana? Nani asiyejua kwamba mkataba wa TRL ulisainiwa wakati wa serikali ya awamu ya nne, tena wakati huo Waziri wa Miundombinu alikuwa Andrew Chenge, ambaye aliuthibitishia umma kwamba walikuwa wamechukua hadhari zote kabla ya kufikiwa kwa mkataba huu, sasa kwa nini RITES imeshindwa kutekeleza majukumu yake, tuseme nini sasa?

Nilifikiri Tanzania ingechukua maamuzi mazito kuhusu RITES, kwanza kuvunja mkataba na kuishitaki mahakamani kwa kuhujumu TRL hadi kufikia hapo ilipo sasa; nafikiri kama taifa sasa tunataka kulipwa hasara hizi ambazo watawala wetu wala hawashtuki, kuumia wala kuona ni kitu kila tunapoliwa katika mikataba hii ya ovyo ovyo ambayo tunatumbukia mwaka baada ya mwaka, awamu baada ya awamu.

Ninasema kwa kinywa kipana sasa tukatae kuwa kwenye kundi la mvaa moja havai mbili, ili kujikomboa na madhila ya kuwa watu wa kutumiwa na kuachwa kama tulivyo.

Mwisho nikumbushe kitu kimoja, kwamba katika kutumiwa kwetu Celtel ambayo baadaye ilikuja kuwa Zain ilianzishwa kwa fedha za TTCL, niseme tena kwamba Indol ya Afrika Kusini iliyonunua TBL na majumba yake kupewa bure, iliyauza majumba hayo na kupata fedha za kuwekeza; NBC ilitolewa bure kwa ABSA baada ya kutakiwa kulipa Sh. bilioni 15 ambazo ilizidai kwa MNB na kudai eti ndiyo malipo yake kwa serikali katika ununuzi wa NBC; sasa TRL imeachwa mkiwa kama si marehemu, hatujui ni kwa kiasi gani RITES imevuna humo ndani.

Itoshe tu kwa leo kusema kwamba kuna haja ya kuchochea uasi wa umma dhidi ya madhila haya ili tuondokane na laana ya mvaa moja havai mbili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: