Serikali isichezee Watanzania


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HALI inayoendelea katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ya kila mara wafanyakazi kulazimika kugoma ndipo wapate haki zao, ni mfano mzuri wa matokeo ya utendaji mbaya wa serikali.

TRL iliyotokana na uuzwaji wa hisa 51 za lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kampuni ya Kihindi ya RITES – Rail India Technical & Economical Service – inadhoofika kwa sababu ya menejimenti mbovu.

Sehemu kubwa ya viongozi wake katika menejimenti ni wageni wanaofanya kazi kwa kuzingatia zaidi matakwa na mitizamo ya wawekezaji hao.

Si ajabu basi kukuta utendaji wao unatajwa na wafanyakazi kuwa ni usiojali miundombinu ya kampuni na wafanyakazi wake. Kwao kitu muhimu ni faida na ziada tu japo hawajengi mazingira ya kupata hayo.

Ushahidi ni dhahiri. Kwa mara nyingine TRL imeonyesha kuwa kichwa ngumu baada ya kushindwa kulipa wafanyakazi wake mishahara ya Novemba.

Hali wakifahamu vizuri wajibu wao kimkataba, TRL hadi juzi Jumatatu, hawakulipa mishahara hiyo wala hawajatoa ahadi lini watalipa.

Cha kusikitisha ni kauli za kudhihaki watoazo, eti kampuni haina fedha. Lakini huduma hazijasimama, ingawa ni katika mazingira mabaya; na wafanyakazi kupitia chama chao, TRAWU, wanasema hakuna tatizo la fedha TRL.

Takwimu wanazotoa zinasema kufikia 22 Novemba, TRL ilikuwa na Sh. 3 bilioni na hadi 4 Desemba (Ijumaa iliyopita), tayari zilikuwa zimepatikana Sh. 600 milioni zikiwa mapato yanayotokana na huduma za usafiri na usafirishaji abiria na mizigo.

Tunakumbuka TRL ilishindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi hadi ikabebwa na serikali. Mara mbili serikali imetoa kiasi cha Sh. 7 bilioni kulipa wafanyakazi. Lengo lilikuwa ni kuepusha matatizo makubwa yatokanayo na migomo.

Malalamiko dhidi ya menejimenti ya TRL yamekuwepo kwa muda mrefu tangu mkataba wa kuwaingiza RITES kuendesha shirika uliposainiwa Oktoba Mosi 2007.

Inashangaza wawekezaji hawajaonyesha nia njema ya dhati kujenga TRC na wafanyakazi wake. Lakini inachefua zaidi kuona wanatoa visingizio ili kukwepa majukumu yao ya kimkataba.

Tunajiuliza kama wanavyojiuliza wafanyakazi wa TRL na Watanzania kwa ujumla: Tabia hii ya wawekezaji itakwisha lini?

Kwa nini serikali iendelee kubeba wawekezaji wabovu huku athari zikiwa ni pamoja na kuzorotesha huduma za reli inayotegemewa na sehemu kubwa ya wananchi?

Serikali inangoja nini iwapo wawekezaji wanashindwa kuheshimu mkataba? Serikali inaogopa nini kuuvunja mkataba wakati tayari wawekezaji walishauvunja?

Iwapo mazonge yote yaliyopo TRL hayajafikia wawekezaji kuvunja mkataba, maana yake nini? Uko wapi ushahidi mwanana wa kushindwa kwa mwekezaji na mwendeshaji kuliko kushindwa kulipa mishahara.

Huko ndiko kuvunja mkataba. Sharti serikali ichukue hatua. Irejeshe TRL mikononi mwa Watanzania.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: