Serikali iwajibike 2010


editor's picture

Na editor - Imechapwa 06 January 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWAKA 2009 ulikumbwa na mjadala mizito. Mingi ilihusu tuhuma na shutuma kuhusu ufisadi serikalini na katika taasisi zake.

Rushwa na ufisadi vilitajwa pia katika mihimili mingine ya dola: Bunge na Mahakama. Tuseme basi hakuna mhimili uliosalimika katika kuhusishwa na maovu.

Hata pale serikali ilipojitoa ikakamata na kushitaki watuhumiwa wa ufisadi, maneno ya wengi yamekuwa “Waliokamatwa wamefanyiziwa tu bali wahusika wakuu hawajakamatwa.” Kauli ikakuzwa, “mafisadi wanaogopwa.”

Tunasema ni hatari inapotokea viongozi wanakosa ujasiri katika kupambana na maovu, na pale ulegevu na rushwa vinapotawala katika utendaji wa taasisi za dola zinazotegemewa kufuta fedheha hiyo.

Yamekuwepo malalamiko na shutuma kutoka kwa wananchi kwamba uongozi wa nchi umepotea njia. Kwamba mfumo wa utendaji kazi katika serikali yetu umeshindwa kuondoa watu katika umasikini.

Inathibitika sasa uchumi wa nchi haukui katika kiwango kilichotarajiwa na kuahidiwa na serikali yenyewe au kinacholingana na raslimali ambazo nchi imejaaliwa kuwa nazo.

Wanaonufaika na mfumo uliopo wa utendaji kazi serikalini, ni maofisa wachache wanaolindana huku sehemu kubwa ya wananchi wakiumia na kusaga mawe.

Pengo la masikini na matajiri linazidi kupanuka. Ndio kusema umasikini unachukua wengi zaidi kuliko wanavyoondokana nao. Takwimu za kiserikali haziendani na hali inayoonekana.

Kwa mfano, serikali inaeleza kuwa kwa miaka minne sasa, umasikini umekuwa ukipunguzwa kwa kiwango cha asilimia mbili kila mwaka. Hakitoshelezi.

Ni hali inayosikitisha hata wahisani wanaosaidia serikali. Chukua Umoja wa Ulaya ambao katika taarifa yao wakati wa kusaini makubaliano ya kuipatia Tanzania msaada wa Sh. 750 bilioni unaokwenda hadi mwaka 2014, wametoa indhari kuwa mambo hayaendi vizuri.

Wanalalamikia ulegevu wa serikali katika kukomesha rushwa hasa kubwa, upotevu wa fedha za serikali na raslimali zake nyingine. Wanalaumu mtindo wa wakosaji kulindwa na viongozi kucheza pamoja na mafisadi.

Ulaya wanasema wakati umasikini unaendelea kutishia Watanzania wengi, utekelezaji wa malengo ya milenia unakwama na mazingira ya kuwekeza nchini yanazidi kuwa mabaya.

Iko wapi Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya iliyoasisiwa na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anakampeni kutafuta urais?

Iwapi faida ya semina elekezi zilizohusisha viongozi na watendaji wa ngazi ya juu serikalini? Kila siku wananchi wanashangaa hawaoni maisha bora waliyoahidiwa.

Uvivu unaokithiri kwa serikali katika kutekeleza jukumu lake kuu la kuhudumia wananchi utaumiza zaidi Watanzania, hasahasa mkulima, mvuvi, mfugaji na mfanyakazi wa kada ya chini.

Tunapoingia mwaka 2010 tunatarajia wakuu wa serikali watoke na majibu ya maswali haya. Tunataka wabadilike kwa kujenga utumishi uliotukuka; ule utakaoondoa Watanzania kwenye maisha ya mashaka.

Watanzania hawawezi kuendelea na utumishi wa mazoea. Lazima wahudumiwe kifanisi. Shughuli zao ziende; uchumi wa nchi yao ukue inavyotakiwa na nchi ilingane na nyenzake zinazotabirika.

0
No votes yet