Serikali kikwazo vita vya ufisadi


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 06 May 2008

Printer-friendly version

WIKI iliyopita suala la kushamiri kwa ufisadi nchini limezungumzwa na watu watatu mashuhuri akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Ingawa wote hawa wametoa mitazamo tofauti, lakini wanakubaliana kitu kimoja - kwamba hali ya ufisadi ni mbaya mno kiasi cha kuhatarisha amani.

Akiwa mkoani Iringa, wakati wa sherehe za Mei Mosi, Pinda alisema kuwa ufisadi ni tatizo kubwa nchini lakini akaonya kwamba lisihusishwe moja kwa moja na chama chake-Chama Cha Mapinduzi (CCM) au serikali yake.

Alisema suala la ufisadi ni suala la mtu mmoja mmoja, ambapo katika asasi hizo wapo wachache. Alijitapa kwamba wengi wa waliopo katika taasisi hizo ni watu wasafi kabisa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, akilizungumzia suala hilo hilo katika mahojiano na gazeti la kila wiki kwa lugha ya Kiingereza la The African on Sunday, alisema kuwa itakuwa ni makosa iwapo vita yoyote dhidi ya ufisadi itakuwa inalengwa kwa mtu mmoja mmoja, na aliitaka ilenge katika kuiondoa hali nzima ya uozo huo katika jamii.

Akitoa mfano, alisema itakuwa kazi bure kumfuata mtu mmoja mmoja anyetuhumiwa, kwani hawa ni wengi mno, na badala yake vita ielekezwe kwa mfumo mzima unaoipandikiza na kuilea hali hiyo.

Mtu wa tatu aliyetoa maoni yake kuhusu ufisadi alikuwa ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sengodo Mvungi, ambaye, katika mahojiano yake na kituo kimoja cha Televisheni, hakutofautiana sana na Butiku. Dk. Mvungi, alisema tatizo ni mfumo, na siyo watu.

Mimi naheshimu maoni ya wote hao, na nakubali moja kwa moja kwamba hali ya uozo katika mfumo wa utawala ndiyo tatizo na ni lazima itokomezwe.

Lakini swali langu ni kwamba, wananchi watautokomezaje ufisadi? Au tuseme ni nani mwenye mamlaka ya kubeba wajibu wa kutokomeza ufisadi zaidi ya serikali?

Hii ni kwa sababu wananchi, kwa ujumla wao, wanaweza tu kuchangia hadi kiwango fulani kama vile kuwafichua mafisadi, au kutoa taarifa za vitendo vya ufisadi.

Baada ya hapo ni kazi ya serikali, kupeleka vita hiyo mbele. Ni kazi ya vyombo hivyo kupeleleza watuhumiwa, kuwafikisha mahakamani na kuhakikisha wanaopatikana na hatia wanahukumiwa kwa mujibu wa sheria.

Ni serikali pekee ndiyo yenye uwezo huo wa kutoa adhabu kwa wahusika na si wananchi. Lakini mara nyingi viongozi wetu, wakiwa katika majukwaa hupenda sana kusema "bila ya ushirikiano kutoka kwa wananchi, vita dhidi ya ufisadi haitafika popote." Wanataka wananchi kuwafichua, lakini serikali inaishia kusema "hawashitakiki."

Ukweli ni kwamba hadi sasa wananchi wameshafanya kazi ya kutosha katika kuwafichua mafisadi na ni sharti serikali iwape pongezi. Yaliyofichuliwa tayari ni mengi mno na yanatosha kuiwezesha serikali kufanya kazi yake.

Lakini hali inayojionyesha ni kinyume na matarajio ya wananchi. Serikali mbele ya macho ya wananchi inaishia kupiga danadana na mwisho inatoa visingizio vya ucheleweshaji wa kesi.

Isitoshe, vyombo vya serikali vinavyosimamia masuala haya, hasa taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), vinaonekana kuiangalia serikali kwanza katika kila hatua kwa ajili ya kupata maagizo, maelekezo au hata amri.

Bila shaka hii inatokana na ukweli kwamba kuna wakubwa fulani wanaotuhumiwa na ufisadi na hivyo wakuu wa TAKUKURU wanatarajia kupata malekezo kuhusu hao.

Na hii inatokana pia na ukweli kwamba pamoja na maelezo mengi, TAKUKURU imejikita katika Muhimili mmoja wa nchi - Muhimili wa Utawala (Executive Branch) na ambao ndiyo watuhumiwa wengi wa ufisadi wanapatikana.

Mtu anaweza kusema kwamba kwa ujumla, muhimili wa Utawala ndiyo unaoleta kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya ufisadi nchini.

Tumeona, katika sakata la Richmond, kwa mfano, jinsi muhimili wa Bunge (Legislature) ulivyofanya kazi yake. Lakini kwa upande wa serikali, hadi sasa haijachukua hatua zozote dhidi ya wale waliotuhumiwa, badala yake wananchi wanasikia maneno tu ambayo ni ishara ya danadana.

Muhimili mwingine mkuu wa nchi " Mahakama " hatujaona jinsi utakavyoshughulikia masuala haya, kwani hadi sasa haujapelekewa kesi yoyote. Kesi nyingi zimefungiwa katika makabati ya wakubwa serikalini.

Kuhusu kauli ya Pinda kwamba ufisadi usihusishwe moja kwa moja na CCM na serikali yake, ingawa nakubali kwamba mafisadi ni wachache, lakini ni lazima ifahamike kwamba hawa ni watu hatari sana kwa taifa.

Nguvu yao kubwa ni pesa walizopora. Pinda mwenyewe alilibaini hilo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Panda alisema si rahisi kuwashughulikia mafisadi kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Wanaweza kutumia fedha hizo kujikwamua katika kesi dhidi yao.

Pamoja na kwamba sikuridhishwa kabisa na kauli hii kutolewa na kiongozi mkuu wa serikali. Kwa tafsiri yoyote ile, kauli hiyo ni ya kukatisha tamaa. Ni kauli ambayo inatosha kuonyesha jinsi serikali inavyowavunja moyo wananchi wanaohangaika kuwasaka mafisadi.

Hata hivyo "mafisadi wachache" hao, kwa mujibu wa kauli ya Pinda, wanaweza kuinunua serikali. Tayari baadhi yao wameishika serikali mkononi.

Ni wazi kwamba kauli ya Butiku kwamba "ufisadi si tatizo la mtu mmoja" ingeweza kupata ufumbuzi iwapo nchi itapata kiongozi mwenye nia na dhamira thabiti ya kukabiliana na hali hiyo bila woga.

Karibu kila mtu anasema kwamba Rais Jakaya Kikwete hakuwa na ajenda yake mahsusi ya kuwaonyesha wananchi atawafanya nini wakati akiingia madarakani.

Matumaini makubwa ya wananchi waliokuwa nayo kwake katika kuwaondolea dhiki, hayajafanikiwa kwa kiwango kilichotarajiwa. Ikiwa sasa anakaribia kufikia nusu ya kipindi chake cha kwanza, hakuna kitu anachoweza kujivunia katika kutimiza matumaini ya wananchi wake.

Si hivyo tu, hata vitendo vya ufisadi vinavyoibuliwa kila kukicha anaonekana ameshindwa kukabiliana navyo. Ni dhahiri kwamba kushindwa huko kunaleta hisia nyingi dhidi yake pia.

Tatizo kubwa hapa ni kupata kiongozi ambaye kwanza awe mwenyewe ni msafi na asiye na tamaa ya mali, na pia awe na uwezo wa kujitolea kukabiliana na yoyote yule. Rais Kikwete si mtu mwenye ubavu huo.

Tayari rais, amenukuliwa akisema mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, aachwe apumzike. Mkapa anatajwa kuhusika moja kwa moja, ama kunyamazia vitendo vya ufiasdi vilivyofanywa wakati akiwa madarakani.

Mimi naamini kabisa yuko mtu au watu miongoni mwa jamii ambaye anaweza kuwa Thomas Sankara, Murtala Muhammed au Jerry Rawlings wetu na ambaye atakuwa tayari kujitolea mhanga kwa ajili ya mamilioni ya Watanzania masikini katika nchi hii yenye utajiri mkubwa.

Ni mtarajio ya wananchi kwamba iko siku Mwenyezi Mungu atakisikia kilio cha wananchi na kumleta mtu huyo kama kiongozi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: