Serikali kufanya usanii rada


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Yaweza kuwatema akina Chenge
Waokotwa ‘vijana wa Kariakoo’
Andrew Chenge

KESI ya "vigogo wa rada" imehamia kwa watu wadogo ikiacha watuhumiwa wakuu wa awali – Andrew Chenge, Tanil Sumaiya na Sailesh Vithal, imefahamika.

Taarifa zinasema serikali inaweza kuwafikisha mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

MwanaHALISI limeambiwa kwamba badala ya watuhumiwa waliokuwa wakitajwa kwa muda mrefu, akiwemo Dk. Idrissa Rashid wa TANESCO, washitakiwa wote watatu watakuwa wapya.

Waliofahamika kuwa miongoni mwa watuhumiwa wapya ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Salum Msoma.

Wengine wawili ni “watu wasio na majina” katika jamii na kwa mujibu wa mtoa habari, “inawezekana wamewachomoa Kariakoo.”

Katika kashfa hii, serikali ya Tanzania inadaiwa kununua rada ya kuongozea ndege za kiraia na za kivita kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa dola 40 milioni.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah, aliiambia MwanaHALISI kuwa anachofahamu ni kwamba upelelezi wa suala hilo bado unaendelea nchini Uingereza.

“Kwa upande wetu (Tanzania) tumemaliza uchunguzi kuhusiana na suala hilo. Kilichobaki sasa ni kwa wenzetu (Uingereza) kukamilisha sehemu ya uchunguzi. Wao wakikamilisha tunaweza kuwa tayari kushitaki lakini si kabla ya hapo,” alisema.

Juhudi za gazeti hili kupata Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) iliyoendesha uchunguzi wa kashfa hii kueleza walikofikia, hazikuzaa matunda.

Bali Hoseah alisema suala la rushwa ndani ya BAE linahusisha nchi nyingi ikiwamo Marekani, ambayo nayo ni mteja mkubwa wa kampuni hiyo, na kwamba uchunguzi unaoendelea kufanywa Uingereza utatengeneza sehemu muhimu ya ushahidi kwa watuhumiwa wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi amesema hafahamu chochote kuhusu kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wa kashfa ya rada.

“Mimi ninafanya kazi baada ya kuwa nimeletewa jalada na watu wa TAKUKURU na vyombo vingine. Ningeshauri uwaulize kwanza TAKUKURU kabla hujaongea na mimi,” alisema.

Hata hivyo alipoambiwa kuwa tayari gazeti limezungumza na TAKUKURU ambao wamethibitisha tayari kuwa upelelezi wa ndani umekamilika, Feleshi aliomba apewe muda kuona iwapo jalada la watuhumiwa liliishafikishwa ofisini kwake.

Alipopigiwa simu baadaye, Feleshi alisema bado ofisi yake haijapokea jalada la kesi hiyo kutoka TAKUKURU.

“Sijaliona faili la TAKUKURU ofisini kwangu. Without the file, I have no comment to make.” (Bila kuliona faili, sitakuwa na la kuzungumza).

Kashfa ya rada ilitendeka mwaka 1999, katika mazingira yaliyogubikwa na rushwa kwa watendaji serikalini ili waweze kulainisha watoa maamuzi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, Msoma atafikishwa mahakamani kutokana na nafasi aliyokuwa nayo serikalini wakati rada hiyo ikinunuliwa, lakini haijajulikana wengine wawili walihusika vipi.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na SFO ulibaini kwamba nchini Tanzania, watu wanne, Chenge, Somaiya, Vithlani na Rashid walihusika moja kwa moja kwenye sakata hilo.

Ununuzi wa rada hiyo ya kizamani, lakini iliyonunuliwa kwa bei ya juu, ulipingwa ndani na nje ya nchi, lakini serikali chini ya Rais Benjamin Mkapa, iliendelea na msimamo wake wa kuinunua.

Hatua ya serikali kuwafikisha mahakamani Msoma pamoja na watu wawili wengine wasiojulikana inaweza kuzua mjadala nchini hasa ikizingatiwa kwamba wengi walitaraji wangeshughulikiwa kwanza wale waliotajwa kwenye ripoti ya SFO.

Hivi karibuni, BAE Systems ilitangaza kukubali kwake kulipa faini ya dola 450 milioni ili kumaliza kesi mbalimbali zilizokuwa zinaikabili kutokana na udanganyifu katika kuuza zana za kujeshi kwa nchi kadhaa duniani ikiwamo Tanzania.

BAE Systems imeamua kulipa kiasi hicho cha fedha ili kumaliza kesi zilizofunguliwa dhidi yake na SFO pamoja na Wizara ya Sheria ya Marekani.

Kampuni hiyo inakiri kwamba kwa kuboronga katika uuzaji wa rada kwa Tanzania, inaridhia kulipa fidia ya pauni 30 milioni.

Kupitia barua iliyoandikwa 21 Machi 2008 na SFO kwenda kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, ofisi hiyo ilieleza jinsi watuhumiwa wakuu walivyohusika.

Barua hiyo ilieleza kwamba Vithlani, Somaiya, Chenge na Rashid, “wamefanya makosa ya ama kupokea au kutoa rushwa kinyume cha kifungu Na. 1 cha Sheria ya Uingereza ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1906.”

Vithlani na Somaiya wanadaiwa kuwa na nguvu za kufanya maamuzi ya kisheria ndani ya kampuni ya Envers Trading Corporation iliyofanya kazi ya udalali wakati wa mchakato wa kununua rada hiyo.

Katika ununuzi huo, Envers walipangiwa kupata kamisheni ya asilimia 30 ya mauzo ya rada.

Barua hiyo ilieleza kuwa Vithlani ndiye alikuwa akishawishi serikali ya Tanzania kununua rada hiyo iliyopitwa na wakati lakini kwa bei ya juu, ingawa “hakuwa mtaalamu wa rada wala mjuzi wa mambo ya biashara.”

SFO inaamini kutokana na nyaraka ilizonazo, kwamba mwanasheria mkuu wa zamani wa Tanzania, Andrew Chenge, alikuwa mmoja wa watu muhimu kwa Vithlani kutokana na umuhimu wa maamuzi na mapendekezo yao kwa serikali.

“Kwa mantiki hiyo, bila Mwanasheria Mkuu kukubali, malipo ya rada ambayo yalifanywa kupitia benki ya Barclays, yasingeweza kufanyika.

Ofisi ya mwanasheria mkuu ilitakiwa kutoa maoni yake na kisha kukubali malipo yafanyike au yakataliwe,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ilieleza pia kwamba kati ya 19 Juni 1997 na 17 Aprili 1998, taarifa zinaonyesha kwamba kupitia kampuni yake – Franton Investiment Ltd. – Chenge alipokea dola 1.5 za milioni katika akaunti ya kampuni hiyo iliyoko benki ya Barclays, tawi la Jersey.

Ni kwa barua hiyohiyo ilidhihirika kulikuwa na malipo ya dola 500,000 kutoka akaunti ya Chenge kwenda akaunti ya Dk. Rashid iliyoko Royal Bank of Scotland.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: