Serikali kuua raia, lazima yawepo maswali


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Mazishi waliouliwa Arusha

KUNA watu wanataka kutupa pendekezo la hatari na wanataka tulikubali bila kuhoji. Pendekezo hilo ni lile linalotaka wananchi wanapofia mikononi mwa serikali basi watu wasiulize maswali na wasiibane serikali kuwajibika.

Kuruhusu kukubali pendekezo hili ni hatari kwani litatoa kibali kwa watawala kufanya wapendavyo.

Mauaji ya wananchi yaliyotokea jijini Arusha kwenye maandamano na yale ya Mbarali, mkoani Mbeya yanaacha maswali ambano yanahitaji majibu.

Lakini pamoja na maswali hayo kuna hali ya baadhi ya watu kututaka tukubali tu kuwa wananchi wamefia mikononi mwa polisi basi yaishe. Miongoni mwa wanaotaka tukubali pendekezo hili, ni polisi wenyewe.

Yaani, watu wafie mikononi mwa polisi halatu tukubali polisi watoe kauli ya mwisho na kisha tuipokee kama kanuni ya imani. Haiwezekani! Hili ni pendekezo la hatari.

Wananchi hawatakiwi kufa katika mikono ya serikali yao isipokuwa kwa mazingira makubwa ya aina mbili tu: Kwanza ni wakati serikali inatekeleza hukumu halali ya kifo iliyotolewa kulingana na tararibu za haki na sheria za nchi.

Hapa sizungumzii maadili ya hukumu ya kifo; nazungumzia mahali ambapo hukumu hiyo ipo na umewekwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa mtu anayehukumiwa adhabu hiyo kweli anastahili.

Pili, ni pale ambapo ambapo katika mazingira ya kulinda maslahi makubwa zaidi ya jamii, serikali inaona upo uhalali wa kutumia nguvu ambayo yaweza kusababisha kifo.

Hili linatokea pale ambapo vyombo vya dola vinapoamua kutumia nguvu dhidi ya wananchi na sehemu ya nguvu hiyo huweza kusababisha kifo.

Serikali kwa kutumia maafisa wake wa vyombo vya usalama huweza kutumia nguvu katika kulinda na kutetea maslahi ya wananchi wengine au sheria. Hivyo, polisi anaweza akajikuta analazimika kuua kwa sababu hakukuwa na njia nyingine yoyote ya kuondokana na tishio lililokuwepo.

Sote tunajua kuwa mauaji yaliyotokea Arusha na yale ya Mbarali hayakutokea kwa sababu hiyo ya kwanza – kutekeleza hukumu halali ya mahakama.

Hivyo, sababu pekee ambayo inatajwa ni kuwa wananchi waliouawa jijini Arusha na Mbarali ilitokana na polisi kutumia nguvu kukabiliana na wananchi. Hii haihalalishi mauaji kufanyika.

Kwa mfano, jijini Arusha bado hawajakubaliana kama vifo vilivyotokeaa vilitokana na CHADEMA hatositisha maandamano au kwa sababu wale waliouawa walikuwa wanajaribu kuvamia kituo cha polisi.

Kule Mbarali kuna hilo nalo, kwamba vifo vimetokana na wananchi kuwawazidi nguvu polisi au la. Mjadala huu ungeweza kuzima kwa kauli moja ya polisi, “Kuomba radhi Watanzania na kusema basi yaishe.”

Bahati mbaya msimamo huu wa serikali inaweza kuua raia wake bila kuhojiwa unaungwa mkoano na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa dini.

Kwamba, tukihoji mauaji hayo maana yake tunapingana na “mamlaka halali.”Kwamba, tukitaka maelezo ili tujue kuwa wananchi wameuawa katika mazingira ambayo yangeweza kukubalika, “Tunaonekana hatujali polisi.”

Tatizo ni kuwa serikali duniani hasa zenye mwelekeo wa vitendo vya kifisadi au vya kidekteta huanza kwa kuua wananchi wake pasipo kuulizwa na mtu.

Idi Amin alianza hivyo hivyo na huyu jamaa aliyetimuliwa huko Tunisia naye ni hivyo hivyo. Tawala za kimabavu kama iliyowahi kuwapo Afrika Kusini nayo ilitawala hivyo.

Wananchi wanauawa, lakini hakuna maswali na wale wanaothubutu kuhoji wanaonekana wanataka kuchochea vurugu au kufanya watu “waichukie” serikali.

Hata wakati wa sheria za kibaguzi za nchini Marekani, wananchi walikuwa wanauawa na tawala za chini. Na pale wananchi walipojaribu kuhoji, wakati mwingine “walipotea” kiana. Haturajii sisi kufika huko.

Kutokana na uelewa mkubwa ambao serikal inayo na nyezo ambazo ziko mikononi mwake, nchi zenye kufuata demokrasia ya kweli zimeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha wananchi wanapokuwa mikononi mwa vyombo vya dola wanakuwa salama.

Lengo ni kuzuia watawala kutumia kifo kama silaha ya kulazimisha watu waipende serikali au kutii mamlaka yake.

Maana serikali ikianza kutumia kifo kama silaha, maana yake watu wataanza kuogopa kuhoji, wataogopa kujitokeza kupinga serikali yao na wataogopa hata kutoa maoni yao.

Hivyo wenzetu walioendelea wameweka utaratibu unaotumika wakati ambapo wananchi wanauawa mikononi mwa polisi.

Karibu vikosi vyote vya polisi nchini Marekani wanapoua raia, askari waliohusika husimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa ndani ili kuhalalisha matumizi ya nguvu kubwa namna hiyo.

Baadhi ya mamlaka za pPolisi zimeweka utaratibu kuwa wakati wowote polisi wanatumia risasi na kuua basi wale polisi waliohusika wanatakiwa kutoa maelezo ya kuhalalisha matumizi hayo ya nguvu.

Katika maelezo yao, wanatakiwa waeleze ni kwanini walitumia nguvu hiyo na si nyingine; na kama walikuwa wamefuata agizo, basi ni agizo la nani. Wanaeleza iwapo waliamini agizo walilopewa lilikuwa halali au la.

Lengo ni kuhakikisha kuwa polisi hawaui halafu yakaisha Hili la mwisho ndilo ambalo maofisa wa polisi na baadhi ya watu wanataka tukubali kwamba wananchi wamekufa mikononi mwa polisi basi yaishe.

Tukilikubali, basi tujue tumekubali kuwapa kibali cha kutuchinja wapendavyo. Kama wameuawa safari hii na wote tukataa kimya, kesho wakiuawa 10 itakuwaje, na kesho kutwa itakuwaje wakiuawa 50?

Kwa sababu tukikubali kwamba polisi wanaweza kuua halafu wao wenyewe wakaja kutuambia kuwa wameua kwa sababu “walizidiwa” ama “hakukuwa na njia nyingine,” na sisi tukakubali, basi tutakaribisha utawala wa kidikteta.

Ninachosema ni hiki: Mauaji ya Arusha na Mbarali na mauaji mengine yoyote ya wananchi mikononi mwa polisi yanahitaji hayawezi kukubalika. Polisi wananyenzo tena nyingi za kukabiliana na wahalifu. Wazitumie badala ya kutumia silaha za moto.

Inahitajika maelezo na yenye kukubalika na ushahidi wa wazi kuhalalisha matumizi ya silaha za moto kwa raia. Katu huwezi kuhalalisha hilo kwa kauli zisizo na mashiko za viongozi wa polisi.

Na ili tuweze kuyapata majibu sahihi haiwezekani wahusika polisi wenyewe ndiyo watoe maelezo hayo. Inspekta Jenerali ndiye aliyezuia maandamano, na yeye mwenyewe ndiye baadaye anatueleza kuwa mauaji yalikuwa halali? Kwanini tumuamini?

Sasa nakubaliana na wale wanaotaka uchunguzi huru ufanyike. Lakini, ninajiuliza hivi kweli hakuna utaratibu uliokubalika kutumika wakati polisi wanaua wananchi kwa sababu yeyote ile?

Je, Tume ya Haki za Binadamu haijahusishwa katika mazingira kama hayo? Hivi kweli tutaendelea kusubiri wananchi wangapi wafe ndio tupate akili za kuweka utaratibu kama huo?

Kwa sababu ukiniuliza mimi sitaki kuwa na Polisi ambaye ameua na amerudi kazini kesho yake! Vinginevyo, tunaweza kukuta watu wanaanza kufurahia hiyo nguvu ya uhai na kifo.

Na sisi kama taifa tusiikubali watu wafe mikononi mwa serikali bila kuhoji. Vinginevyo, sisi wenyewe tutaletewa misiba na tutashindwa kujua pa kuanzia.

Tuungane kuhoji na kupinga bila kujali dini zetu, vyeo vyetu, vyama vyetu, hali zetu za maisha na mambo mengineyo kama hayo.

Ni lazima iwe ngumu sana kwa serikali au vyombo vyake kuua wananchi raia wake. Hadi hivi sasa, polisi wamepoteza haki ya kufafanua mauaji ya Arusha na jinsi walivyojichanganya ninaamini uchunguzi huru utahitajika.

Taarifa tulizopewa aidha hazikuwa sahihi au kwa makusudi zimepotoshwa. Tunataka wa kutuambia ukweli. Serikali haiwezi kufanya hivyo, wala polisi hawawezi kufanya hivyo.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: