Serikali, sheria na meno ya plastiki


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version

KUNA Sheria tatu ambazo hazimlazimishi mtu kuzitii kwani kama ni meno basi ni yale ya utoto. Ipo Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 ambayo pamoja na mambo mengi imetajwa mara ya tatu sasa na Mkaguzi Mkuu kuwa inahitaji “meno.”

Ni sheria ya ajabu. Licha ya mazuri yote ambayo sheria hiyo inafunua, inabakia kuwa ni picha tu. Sheria hiyo, kama ilivyo sasa, hailazimishi mtendaji yoyote kuitii.

Inakuwaje vitabu vya hesabu vinaota miguu wakati wa ukaguzi na havipatikani, halafu mtu kesho yake bado anarudi kazini?

Inakuwaje kwenye idara moja kuna vitu vyenye thamani ya zaidi ya mamilioni vinatajwa vitabuni lakini havipo kihalisia; halafu mkuu wa idara hiyo bado anarudi kazini siku ya pili?

Inakuwaje mtu ananunua magari ya Sh. 400 milioni, wakati inajulikana magari hayo hayazidi million 30 halafu bado anajitokeza hadharani na rais au waziri fulani kana kwamba yeye ni kiongozi bora?

Sababu ni moja: Sheria ya manunuzi inapuuzwa kwa sababu haisimami kama dikteta wa mwisho. Ni kwa sababu hiyo, baadhi ya viongozi wanageuza idara za serikali kama kampuni binafsi na bado wanaendelea kubaki kazini na hakuna mtu aliyepiga kelele kama vile taifa lote limelishwa limbwata.

Hata hivyo, kwenye nchi yenye utawala wa sheria basi sheria ndiye dikteta mkuu (the law is the great dictator) na siyo mtu binafsi, hata awe rais au waziri mkuu.

Sheria nyingine ambazo nazo zimebakia kuwa kama mapendekezo ni ile ya Usalama wa Taifa ambayo ilitengenezwa kwa makusudi ya kufanya idara hiyo nyeti kuwa butu na badala yake kuwa ni chombo cha kisiasa zaidi.

Licha ya hotuba nzito iliyotolewa mwaka jana bungeni na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), CCM na wabunge wake hawaoni tatizo la idara hiyo.

Unaweza kuwa na Usalama wa Taifa ambao kisheria unakatazwa kukamata watu. Badala yake wamebakia kuwa wakusanyaji taarifa na wachambuzi?

Sheria nyingine ambayo nayo ni mfano wa mapendekezo, ni ile ya maadili ya viongozi wa umma. Walioiandika hawana maadili na sisi tulitarajia waandike kitu chenye maadili.

Sheria ambayo haimtiishi kiongozi wa umma kuwa muwazi, kufuata sheria na kutenda juu ya tuhuma yoyote, ni sheria ya kitoto.

Huwezi kuwa na sheria ya maadili wakati haina kichocheo chochote cha maadili. Kungekuwepo na sheria nzuri ya maadili, Basil Mramba na Andrew Chenge wasingeendelea kuwa mbunge.

Hata Benjamin Mkapa, tayari angefikishwa mahakamani. Edward Lowassa asingelipwa mafao kama waziri mkuu mstaafu; hata kaubunge kake kangekwishachukuliwa.

Hakika, watu kadhaa wa kadhaa wangekuwa wameondolewa kwenye utumishi wa umma. Lakini chini ya CCM, kutengeneza sheria yenye nguvu za namna hiyo, ni ndoto isiyoweza kutimilika.

Tunaweza kuzungushana na kutafuta kila aina ya udhuru,bali ukweli utabakia kuwa CCM na wabunge wake hawawezi kutengeneza sheria ambazo zitafanya wao kuwa waathirika wa kwanza.

Hawawezi kutengeneza sheria ambazo zitasababisha watu wake, hasa viongozi wake, kuaibika au kujikuta wanaswekwa lupango. Kwa kadiri tunavyowapa nguvu ya kutunga sheria, vivyo hivyo tusitarajie mabadiliko katika sheria zetu.

Wataendelea kutunga sheria zenye mfanano wa meno lakini ukichunguza kwa karibu utaona kuwa ni meno ya plastiki ambayo hata kumenya muwa hayawezi.

Hayo ndiyo matarajio yangu kwenye sheria yao ya wanasiasa kuchagua biashara au siasa. Hawawezi kutengeneza sheria ambayo itasababisha wafanyabiashara wasichague siasa.

Njia kubwa inayotumiwa na serikali na vyombo vyake katika kukwepa kuitii sheria, ni ile ya uundwaji wa tume.  Serikali imegundua (muda mrefu sasa) kuwa badala ya kutii sheria au kuacha sheria ifuate mkondo wake, viongozi wake hufanya hima kuunda Tume.

Na kwa vile Watanzania wanapenda mazingaombwe, basi wakisikia tume imeundwa basi wanafikiri sheria imefuatwa.

Tume huundwa kila wanaposhindwa kuifuata sheria au pale wanapojua kuwa sheria ikifuatwa hadi herufi yake ya mwisho, inaweza ikawatafuna wao wenyewe.  Tume zinatumika kama kiinimacho cha utawala wa sheria.

Isitafsiriwe kuwa hakuna haja ya kuunda tume au tume kwa asili yake ni mbaya wakati wote. La hasha.

Ninachosema ni kitu chepesi sana. Pale ambapo sheria iko wazi na imevunjwa, basi tusitumie uundwaji wa tume kuikwepa au kudhoofisha matumizi ya sheria hiyo.  

Pia tutambue kuwa tume inapofanya kazi yake sambamba na chombo chenye uwezo wa kufanya kazi hiyo, basi athari yake ni kukifanya chombo kilichoundwa kwa ajili hiyo kutokuwa na ulazima wa kuwepo.

Kwa mfano, kwanini tuwe na idara ya upelelezi ya polisi wakati tume inaweza kuchunguza kilichotokea Tabora? Kwa nini tuwe na nafasi ya DPP na kumpa madaraka makubwa wakati yale ambayo angeweza kufanya yanaweza kufanywa na Tume?

Binafsi siwalaumu CCM kwa kutotengeneza sheria ambazo kiukweli kabisa zingesababisha mabadiliko katika fikra za wananchi wetu kiasi kwamba watu waziogope.

Hadi pale sheria zitakapotungwa, ambapo wabunge wa CCM, kwa wingi wao, watazipinga basi ujue sheria hizo ni kali.

Ukiona sheria imepitishwa kwa urahisi basi ujue, ama haina athari kwa CCM na viongozi wake au inahusu mambo ambayo wanajua kabisa hayatawagusa wengi wao.

Hivyo, kama unasubiri itungwe sheria nzuri ya mambo ya fedha sharti usubiri hadi kiyama.

Kama unasubiri sheria ya madini ambayo itahakikisha Watanzania wananufaika na utajiri wa urithi wa nchi yao, utasubiri hadi miguu iote mizizi.

Kama unasbiri sheria itakayosababisha watendaji waogope kugusa hata shilingi moja ya fedha za umma, basi utasubiri hadi nywele ziote maua.

Na kama unasubiri sheria ya kuleta hadhi ya Usalama wa Taifa, basi utasubiri hadi uone mamba wakicheza “Mugongo… mugongo…”

Je, tunataka nchi yenye utawala wa sheria au yenye sheria ya watawalao?
Tusipoangalia tutafikia mahali ambapo sheria zinatumika kama hiari na hisani ya watawala.

0
No votes yet