Serikali, TCRA wanajua simu hizi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), inajivunia usajili wa simu za mkononi uliokamilika yapata miezi mitatu iliyopita.

Serikali ilikuwa inadai kuwa simu za mkononi zinatumiwa kufanya uhalifu.

Uhalifu uliotajwa ni pamoja na kutukana, kupanga wizi na, au hujuma; kutoa vitisho kwa watu mbalimbali; kutoa taarifa za upotoshaji na wakati wote huo bila mhusika kufahamika.

Serikali ilidai simu zikisajiliwa, kazi yake ya “ulinzi wa amani” itakuwa imerahisishwa.

Simu zimesajiliwa. Wamiliki wamesajiliwa. Je, sasa serikali na TCRA wanaweza kutuambia simu Na. +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

Tangu Ijumaa wiki iliyopita, namba hizo za simu zimekuwa zikitema tuhuma dhidi ya Dk. Willibrod Slaa, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ujumbe wa simu unasema Dk. Slaa ni “mropokaji” anayelumbana na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi na kwamba anataka damu imwagike.

Kulumbana tu? Halafu damu inamwagika? Haya ni mazingara ya filamu za Nigeria.

Kwa waliosajili simu na wamiliki wake je, simu Na. +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

Nimepokea simu 79 zinazoulizia mwenye simu hiyo na shabaha yake. Bali karibu wote wamesema lazima utakuwa uzushi unaolenga kumdhoofisha Dk. Slaa.

Wamesema Dk. Slaa hana sababu wala muda wa kulumbana na majeshi – polisi, JW hata usalama wa taifa.

Aliyejitambulisha kuwa Moses Sebabili, kutoka Kabanga, Ngara amesema, “Dk. Slaa hana sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa kesho tu, atakuwa karibu sana nao na hata kuwaondolea matatizo ya miaka mingi.” Hiyo ni pindi akiingia ikulu.

Bali kwa waliosajili simu na wamiliki wake, namba hizi: +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

Sauti ya mwanamke iliyoita Jumamosi asubuhi, ilijitambulisha kuwa ni mwanamke wa Kimasai aliyeko Hanang. Alipokea ujumbe huo.

Je, waliotuma ujumbe walijua vipi namba ya simu ya mama wa Kimasai aliyeko kijijini Hanang? Labda waliosajili simu waweza kujua Na. +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani.

Kati ya watu 79 walioniita hadi Jumatatu usiku, 24 ni kutoka maeneo ya shamba na uwezekano wa simu zao kufahamika kwa aliyepeleka ujumbe, ni mdogo sana.

Nani ametoa namba za waungwana hawa kwa mwenye nia ya kutukana majeshi, kwamba akitokea mtu mmoja tu akalumbana nayo, basi yatamwaga damu? Nani?

Sasa majeshi na wananchi walioingiziwa ujumbe unaolalamikiwa, wanataka kujua: Hivi simu hizi, +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

Aliyeamuru simu na wamiliki wasajiliwe ni serikali. Aliyesimamia zoezi hilo ni TCRA. Waliotekeleza kazi hiyo ni mitandao ya simu nchini – tiGO, zain, vodacom, zantel, ttcl; nani mwingine?

Binafsi, namba yangu iko wazi gazetini. Je, wamepata wapi namba ya mama wa Kimasai wa Hanang; mchunga ng’ombe wa Ushirombo, Shinyanga; mkulima wa Namanyere, Rukwa, dereva teksi wa Tanga? Wamepata wapi?

Kauli za “wapinzani wakishinda damu itamwagika” zilisikika tangu miaka 15 iliyopita – pale mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa. Zilienezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwanza, baadhi ya watu wa shamba waliaminishwa, lakini baada ya miaka kupita, wakagundua ni ghiliba. Wakaona upinzani unawafumbua macho.

Mwaka huu, kwa mara ya kwanza tangu 1995, upinzani umekuja na hoja nzito zisizojibika kirahisi na ambazo zimekaba koo la CCM na wagombea wake.

Mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete – na mke wake Salma na watoto wao wawili, Ridhiwani na Miraji na jamaa zao, wanajua mzigo waliobeba.

Washauri wa karibu na hata wana-usalama, wanaelewa mzigo aliojitwisha; bali inawezekana hawajui kwamba wanaweza kuendelea kuwa walipo chini ya rais mwingine.

Katika mazingira haya ya mshikemshike, nani anaweza kuwa anajua simu Na. +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

Nani anaweza kuwa amezitumia, kwa kulenga kuchafua mmoja lakini akachafua wote; au amechafua yule ambaye hakutaka kuchafua? Nani?

Lakini wenye kujua wamiliki wa simu na namba zao ni serikali kupitia TCRA na wenye mitandao ya simu. Nani kati ya hao ameruhusu ofisi yake kupitisha “uchafu” dhidi ya jeshi na Dk. Slaa?

Niliwahi kuadika kupinga mradi wa kusajili simu. Nilisema huwezi kuondoa uhalifu kwa kusajili simu. Nilipendekeza utafutwe utaalam wa kukabiliana na uhalifu.

Sasa pamoja na usajili, hii chakachua iliyoleta Na. +3588976578 na +3588108226 imetoka wapi? Serikali haijui? TCRA haijui? Wenye mitandao hawajui? Udhibiti uliotakiwa uko wapi?

Kinachouma wengi ni, wamepataje namba za simu za wananchi ambazo hazijawahi kuchapishwa gazetini au kutangazwa redioni? Wametunga? Wamechukua kwenye mafaili ya TCRA?

Bali kinacholeta matumaini ni kwamba ujumbe wa simu Na. +3588976578 na +3588108226, unaosema Dk. Slaa ni mropokaji, haumpunguzii heshima; unamwongezea hadhi.

Mafisadi waliotajwa hadharani; wale wezi wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) na Hazina ambao aliwaanika; hawana jema la kusema juu ya Dk. Slaa.

Wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture, iliyokwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka BoT; wamiliki na wenye hisa katika Meremeta na Deep Green, makamapuni mengine ya kifisadi ambayo mgombea urais wa CHADEMA alianika, hawana neno jema kwake.

Wenye tamaa ya fisi, wanaosubiri mabonge ya dhahabu, almasi, tanzanite kutoka migodini ambako Dk. Slaa alishalikoroga kwa takwimu zisizopingika, watamwogopa na kumwita mropokaji.

Wananchi wanaoendelea kuwa maskini, katikati ya utajiri wa raslimali zao zilizoporwa na kikundi kidogo cha watu wa ndani na nje, wanahitaji “mropokaji.”

Wanaoitwa waropokaji ndio wenye uchungu na nchi yao. Wanahitajika wengi wengine. Ndio wawezao kuongoza katika kuleta mabadiliko kwa manufaa ya taifa.

Nimegundua kitu kimoja: Wananchi ambao wamefuatilia mwenendo wa Dk. Slaa kwa miaka 15 ya ubunge wake – ambapo ameadabisha serikali kwa kauli, takwimu na vidhibiti visivyopingika – hawatibuliwi na ujumbe wa simu.

Wanasubiri uchaguzi ili waandike historia ya mabadiliko vijijini, mijini, viwandani na maofisini; katika biashara, shuleni na vyuoni, ndani ya ikulu na katika majeshi ya ulinzi na usalama.

Kote huko wanasubiri mabadiliko. Lakini wanauliza, hizi namba za simu: +3588976578 na +3588108226 zenye ujumbe uliolenga kudhoofisha mwendo wa mabadiliko, ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki/wamiliki wake ni nani?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: