Serikali ya CCM bado inacheza na muswada


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 April 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA mkutano uliopita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Spika Anne Makinda alitoa kauli inayohitaji ufafanuzi kuhusu hatima ya muswada wa serikali wa kuunda Tume ya Kukusanya Maoni ya marejeo ya katiba ya Tanzania.

Ufafanuzi huo unahitajika sasa ili ijulikane aliuondoa muswada huo au aliuongezea muda wa kupata maoni ya wananchi nchi nzima.

Wengi wanaelewa kwamba muswada huo uliokataliwa na wananchi na hata wabunge katika mikutano ya hadhara, uliondolewa ukarejeshwa serikalini.

Lakini matukio ya hivi karibuni yanaonyesha kwamba muswada huo haujaondolewa ila umeongezwa muda ndiyo maana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imejiandaa kuendelea kukusanya maoni ukiwa na maudhui yaleyale.

Tunajiuliza, kamati inatarajia kupata nini kipya kwa wananchi ikiwa wananchi wa vituo vilivyoteuliwa awali —Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma wakiwemo wabunge wenyewe—wameukataa?

Kwa uelewa wetu, wananchi wamepinga mambo mawili makubwa. Kwanza muswada kujadiliwa chini ya hati ya dharura, na pili walikataa maudhui yake.

Kisheria, muswada wowote ukikataliwa na wabunge  unarudishwa serikali ili iufanyie marekebisho au iandae upya.

Makosa yaliyomo katika muswada ule kama ya kupuuza ushiriki wa Rais wa Zanzibar, kuzuia muungano kujadiliwa, Rais wa muungano kuwa na sauti ya mwisho katika mchakato huu, hayarekebishiki kwa kupata maoni mbadala mikoani
Ndiyo maana inashangaza kuona Kamati ya Bunge inajipanga kufanya safari nchi nzima.

Spika wa Bunge awaeleze wabunge na wananchi maigizo haya ya safari za wabunge wa kamati hiyo mikoani yanafanyika kwa maslahi ya nani?

Dalili kwamba muswada huo hauwezi kukubaliwa na wananchi na hata vyama vya siasa zilijionyesha wazi katika mijadala miwili ya wazi iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa). Walitoa makosa zaidi ya 100.

Moto ule uliowashwa na Udasa ndio ulipokewa na wananchi Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar ambako miswada ilichanwa na kuchomwa moto.

Kwa nini serikali inagharimia safari ya wabunge wa kamati hii badala ya kutumia fedha hizo kuandika upya au kufanyia marekebisho ya nguvu? Nani mwenye maslahi, wananchi waliokataa au serikali ya CCM inayoshikiza upite kama ulivyo?

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: