Serikali ya CCM si sikivu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version

KATIKA kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, mawaziri wanajitahidi sana kusema ‘Serikali ya Chama Cha Mapinduzi’, CCM ni sikivu sana.

Tumeshuhudia akisema hivyo Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anawasihi viongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) wasitishe mgomo uliopangwa kufanyika nchi nzima kuanzia Mei 5, mwaka huu.

Tumemsikia pia akisema Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk John Magufuli alipokuwa anaitoa miswada miwili kuhusu ufugaji wa kisasa baada ya wabunge kuikataa.
Tumewasikia hata wabunge wakati wakichangia hoja katika mijadala mbalimbali. Lengo lao ni kutaka watu wote tuamini uongo na uzushi huo.

Mathalani, Jumatatu iliyopita mbunge mmoja wa CCM alisimama kupongeza msafara wa waziri mkuu kutembelea jimbo lake na akataka salamu hizo ziwafikie wahusika.

Tunajua kwamba hizi ni kampeni na zinafanywa kwa gharama ya woga wetu wa kutohoji, kutojua sheria na kutojua mamlaka tuliyonayo dhidi yao. Wasiojua mamlaka tuliyonayo wasubiri miezi ya kampeni ifike.

Kwa hiyo, mawaziri na wabunge wa CCM wanatumia kila mbinu na hila kuwapumbaza wananchi wadhani serikali ya CCM ni sikivu, hivyo inawajali.

Lakini kwa kuzingatia malalamiko ya wananchi, sisi tunasema kwamba serikali ya CCM imeziba masikio ya kusikia kero za wananchi imefungua masikio ya kusikia mlio wa hela za mafisadi, mabepari na wahujumu wanchi.

Kama serikali ya CCM ingekuwa sikivu, isingewachezesha kwata walimu miaka nenda rudi wakidai haki yao.

Serikali ya CCM ingekuwa sikivu ingetekeleza maombi ya TUCTA inayopigania haki za wanachama wake. Badala yake wanasomewa hotuba iliyojaa vitisho wasidai haki yao.

Kama kweli ingekuwa sikivu kwa nini imewatosa wananchi wa Ngorongoro badala yake ikamkumbatia mwekezaji?

Ripoti iliyotolewa na Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC) mwaka 2008 ilipendekeza ama mgodi wa North Mara ulioko wilaya ya Tarime ufungwe au wakazi wa Nyamongo wahamishwe.

Ripoti ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo ilitolewa mwaka juzi inaonyesha madhara makubwa wanayopata wakazi kutokana na maji ya sumu ya cyanide na kemikali ya paf kutoka mgodini. Kama kweli serikali ya CCM ni sikivu, kwa nini imeacha kutekeleza mapendekezo hayo?

Mijadala mikubwa iliyoibuka miaka ya hivi karibuni bungeni kama vile mkataba wa kuipa kampuni ya Richmond kufua umeme wa dharura nk imeisha bila hatua za maana kuchukuliwa.

Kama serikali ya CCM ina uchungu kweli na raslimali za wananchi, kwa nini haikuwachukulia hatua. Wala rushwa za rada, ndege na mikataba ya madini wanatamba mitaani.

Je, si serikali hii ya CCM inayouza nchi na raslimali kwa mabepari ambao leo wamepewa jina la wawekezaji?

Kwa ujumla serikali ya CCM si sikivu na wananchi watakapokuja kugundua wamenyanyaswa kiasi cha kutosha, wamepuuzwa kiasi cha kutosha na wamenyonywa kiasi cha kutosha itawekwa serikali sikivu kwa maslahi ya wananchi wote.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: