Serikali ya CCM yajivunia silaha


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KAMA kuna kitu kimewachefua Watanzania wengi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuhodhi shughuli na sherehe zote za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.

Hata kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Ijumaa ya wiki iliyopita, wananchi waliishia kuona mbwembwe za vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama na kusikiliza hotuba ya rais badala ya kuona kumbukumbu halisi za miaka 50 ya uhuru.

Ni wazi basi, kwamba umoja wa taifa ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, haukuonekana kwenye sherehe za uhuru. Kilichoonekana machoni mwa wengi ni ubaguzi unaotokana na itikadi ya vyama vya siasa na hodhi ya kikundi cha watu wachache kumiliki mambo yanayowahusu wengi.

Dalili za CCM na serikali yake kuhodhi sherehe zilianza kuonekana mapema. Kwa mfano, wakati wote wa maandalizi ya sherehe za uhuru, hakuna hata kiongozi mmoja wa upinzani, aliyeshirikishwa katika vikao vya maandalizi.

Aidha, hakuna chama cha upinzani kilichoshirikishwa kwenye mipango ya kuandaa sherehe za uhuru. Wapo hata baadhi ya viongozi wake, walionyimwa mwaliko wa kuhudhuria sherehe hizo. Wachache walioalikwa walikwenda uwanjani hapo kama wageni wengine waliotoka nje ya nchi.

Kwa CCM na serikali yake, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani, ama ni adui au siyo sehemu ya Tanzania. Hili nalo ni janga.

Matokeo yake ni kwamba, ukiondoa shamrashamra zilizokuwapo uwanja wa Uhuru na matangazo machache kwenye vyombo vya habari, hakukuwa na jambo jingine kwenye maeneo mengine ya nchi, linalotambulisha kuwapo kwa sherehe za uhuru.

Hakukuwa na shamrashamra zozote mitaani. Hakukuwa na bendera zilizokuwa zinapepea. Hakukuwa na magari au pikipiki zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Tanganyika au nyingi za Muungano.

Kwenye barabara kuu, hakukuwa na mabango ya matangazo yanayoonyesha taifa liko kwenye sherehe za uhuru. Jijini Dar es Salaam, mabango ya matanganzo yalikuwa machache sana. Katika maeneo mengine ya wilaya na makao makuu ya mikoa, mabango hayo hayakupatikana kabisa.

Ni tofauti na inavyokuwa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa rais; mabango ya mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete yalitapakaa kila kona ya Jamhuri ya Muungano na hata kwenye vibanda vya nyasi ambavyo wakazi wake hawajawahi kumuona rais lakini wanajua wako Tanzania.

Kwa mgeni yeyote ambaye alikuwa ameingia nchini kwa mara ya kwanza, na ambaye hajabahatika kusilikiza televisheni, ilikuwa vigumu kufahamu kama nchi ilikuwa inasherehekea miaka 50 ya uhuru wake.

Hata wananchi waliokwenda uwanja wa taifa kufuatilia sherehe, ni wachache sana waliokwenda huko wakiwa na moyo wa kusema, “…katika miaka 50 angalau nimepata hiki.”

Kwa hiyo, miongoni mwa wengi jijini Dar es Salaam na hata mikoani, kile kinachoimbwa kila siku: “Tumethubutu, Tumeweza na Tunasonga mbele,” hakina sura na hakikupata umbo wakati wa sherehe.

Hii ni kwa kuwa kwanza, wananchi wanashuhudia umasikini wao ukiongezeka kila uchao. Ujinga unaongezeka kwa kukua kwa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika na wasiopata maarifa zaidi. Maradhi nayo yanaongezeka.

Wananchi wengi, hata wasipopata fursa ya kujieleza, lakini wanaona kuwa kaulimbiu za kuthubutu, kuweza na kusonga mbele ni tupu, kwani haifanani na maisha yao.

Ndio maana utasikia wengi wakisema shabaha kuu ya Mwalimu Nyerere ya kujenga taifa imara baada ya uhuru; taifa huru kwa watu huru; taifa huru lenye viongozi huru, viongozi huru wenye mawazo huru, imemomonyolewa na wale walioingia madarakani baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu au kuondoka duniani.

Wanaona na kushuhudia viongozi wakishindwa kulinda raslimali za taifa. Wanaona na kushuhudia baadhi ya viongozi wakitumia madaraka yao kujitajirisha binafsi, wao na familia zao.

Wananchi wanaona taifa lao lililokuwa linaelekea kujitegemea kutoka katika minyororo ya utumwa kisiasa na kiuchumi, limerudi kwa kasi katika utumwa huo.

Kwa mfano, Azimio la Arusha la mwaka 1967 lililokuwa kitovu cha mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii; lililolenga kujenga jamii ya kijamaa inayoheshimu demokrasia, haki, usawa na kupiga vita unyonyaji, lilibomelowa na viongozi haohao ambao Nyerere aliwachia madarakani.

Miaka 50 baada ya uhuru, sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliyohimiza wananchi kufanya kazi na kuchangia ustawi wa jamii; iliyopiga marufuku baadhi ya viongozi kuishi kwa jasho la wengine; sasa imegeuzwa mtaji na wale waliokabidhiwa madaraka.

Azimio lililoweka miiko ya uongozi iliyowafanya viongozi wasiweze kutumia madaraka ya umma kwa maslahi binafsi; lililoagiza kila kiongozi sharti awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki kwa njia yoyote ile katika ubepari; limefutwa na wale wanaojitapa kulinda uhuru.

Pili, miaka 50 baada ya uhuru, wananchi wanaona viongozi wao waliokuwa wanapigia chapuo taifa kuwa huru, wakiishi maisha ya anasa.

Baadhi yao wanamiliki makampuni makubwa ndani na nje ya nchi; wanamiliki hisa kwenye mabenki; wanalipwa mishahara minono ndani ya serikali na asasi za umma na wengine wameingia ubia na makampuni ya nje kupora rasimali za taifa.

Wananchi wanaona zaidi ya asilimia 35 ya wananchi wake hawawezi kumudu mlo mmoja kwa siku, wakati wengine wanaishi maisha ya anasa. Wanaona jinsi rushwa na ufisadi vilivyogeuka sehemu ya maisha ya kila siku ya baadhi ya viongozi.

Wanashuhudia jinsi wageni wanavyonufaika kwa mgongo wa uwekezaji; uongozi wa umma unavyonunuliwa kama bidhaa, huku wananchi wanyonge wakiporwa ardhi yao na kugeuzwa vibarua katika nchi yao.

Yote haya yamelikumba taifa hili linalosherehekea miaka 50 baada ya uhuru. Matendo ya baadhi ya viongozi yamepotosha shabaha thabiti ya kupigania uhuru wa taifa na hata kuwapo kwa sherehe zenyewe.

Kwa hiyo, ukichanganya yote hayo, wananchi wanakuwa hawana chaguo jingine, isipokuwa kubaki kwenye nyumba zao na familia zao. Sherehe zinabaki kwa walioshiba “matunda ya uhuru.”

Na wananchi hawakuhitaji sherehe. Miaka yote walikuwa wanafanyiwa nani sherehe? Wananchi walihitaji maadhimisho kwa kumbukumbu za kweli zinazoonyesha kupiga hatua za makusudi kwa maendeleo yao na siyo magwaride, ndege za kivita na hotuba kwa watawala wa nchi jirani na Tanzania.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: