Serikali ya JK inacheza makidamakida


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Rais Jakaya Kikwete

KILA mkazi wa Dar es Salaam anaweza kusimulia alivyohangaika usiku wa Februari 16, 2011 baada ya mabomu kulipuka katika maghala ya silaha, Gongo la Mboto.

Japo naishi Chamazi, kilomita 10 hivi kutoka Gongo la Mboto, niliona kiama kimefika.

Watoto wangu walianza kulia. Nilipowaambia wasali, punde walinizunguka. “Baba mbona tunasali mabomu hayatulii?” alilia binti yangu wa umri wa miaka sita.

Nilijikuta nikifunga milango nikaanza safari na familia yangu kuelekea kusikojulikana. Nilipofika barabarani, mwanajeshi mmoja mstaafu aliyekuwa amelewa chakari alituketisha chini, akaanza kutufundisha tabia na aina za mabomu.

Tulitulia, tukabaki tukishuhudia miali ya moto ikienda juu na milipuko ya nguvu.

Watu walikuwa wanatukana ovyo, wakimsaka mchawi. “Serikali hii haifai, mara ya pili? Wakati ule tulifikiri bahati mbaya, safari hii je? Rais Kikwete hatuambii kitu,” alifoka bibi mmoja.

Walizungumza mengi; walisema Rais Jakaya Kikwete kapwaya kiuongozi, ameshindwa vita dhidi ya ufisadi na ameshindwa kuwajibisha wasaidizi goigoi hasa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi

Gongo la Mboto

Tukio la kwanza la milipuko ya mabomu katika jiji la Dar es Salaam lilikuwa mwaka mwaka 2005 kambi ya Gongo la Mboto.

Tukio lile dogo na lisilo na madhara lilikuwa linaizindua serikali kuwa silaha zote zilikuwa zinahitaji kufanyiwa uchunguzi ili ziharibiwe au kuhifadhiwa katika maeneo salama zaidi.

Serikali ikapiga usingizi. Aprili 29, 2009 ilizinduliwa baada ya maghala ya silaha Mbagala-Kizuiani kulipuka na kusababisha maafa makubwa.

Watu 25 walikufa, 300 wakajeruhiwa na yalisababisha uziwi kwa watoto wapatao 300; wengine kuwa yatima na maelfu ya wakazi kukosa makazi.

Serikali haraka iliunda Tume ya Uchunguzi ili kujua sababu za milipuko, na ikawaambia wananchi kuwa imeomba wataalamu kutoka nje ya nchi watumie vifaa vya kisasa kukusanya mabaki yoooote ya mabomu katika maeneo ya raia na kuyaharibu.

Kumbe ilikuwa geresha. Wiki mbili baadaye, bomu zito, walilookota watoto Kizuiani lililipuka na kuwaua Regina Chawala (6) na Rajab Said (6) na likajeruhi wengine wanne.

Wananchi walitoa rai, Rais Kikwete amwajibishe Dk. Mwinyi. Dk. Mwinyi alisema atajiuzulu ikiwa tume itachunguza na kuthibitisha kwamba milipuko ile ilitokana na uzembe.

Nini kilitokea? Serikali ikaficha ripoti ya uchunguzi.

Rais Kikwete kama kawaida yake alitoa ahadi kwamba serikali yake itafanya kila liwezekanalo kupitia maghala yote ya silaha ili tukio la Mbagala lisijirudie tena.

Wananchi walimwamini rais wao. Ikawa 2010, ikawa Januari 2011. Jumatano ya Februari 16, takriban miaka mitano tangu utokee mlipuko mdogo mwaka 2005, na takriban miaka miwili baada ya milipuko kambi ya Mbagala, mabomu ya Gongo la Mboto yakamwaibisha Rais Kikwete.

Maghala yote 23 yaliyokuwa na silaha za kutungulia ndege za adui, kuulia majeshi ya adui na kuhujumu vikosi vya adui, yalilipuka na kuua raia wema ambao wanaimba Tanzania ni kisiwa cha amani.

Watu zaidi 40 wamekufa na zaidi ya 300 kujeruhiwa maeneo ya Gongo la Mboto, Ulongoni, Mwisho wa Lami, Ulongoni, Majohe, Kinyerezi, Mwanagati, Kitunda, Pugu Steshini, Segerea. Wanajeshi na familia zao walisamilika.

Nani alaumiwe

Rais Kikwete hawezi kukwepa lawama. Serikali yake ilicheza makida makida, ikaficha ripoti ya uchunguzi wa Mbagala, ambayo ingetoa mwanga kama milipuko ile ilikuwa bahati mbaya, uzembe, hujuma au ujinga.

Kwa vile hakuna aliyewajibika kutokana na tukio lile, Rais Kikwete ana hiari ya kuendelea kumkumbatia Dk. Mwinyi na wasaidizi wengine wachovu ili hadhi yake iendelee kumomonyoka, au amtose na kuwawajibisha wazembe ajenge upya heshima ya uongozi wake.

0753 626 751
0
Your rating: None Average: 4.8 (6 votes)
Soma zaidi kuhusu: