Serikali ya Kikwete kama Mnara wa Babeli


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

WAKRISTO wanafahamu habari na juhudi za wanadamu waliotaka kujenga Mnara wa Babeli ili wamfikie Mungu. Kwa kuwa walikuwa wamekwisha kupotoka, Mungu hakuwa na sababu yoyote ya kugombana nao, ila aliwavuruga kwa lugha tu. Kila mmoja akawa anasema lake.

Kwa vile hayakuwepo tena mawasiliano, kazi ya ujenzi haikuwezekana; kila mmoja akawa anafanya kivyake, matokeo yake mnara wao uliporomoka. Mawasiliano yanayoongozwa na utaratibu maalum uliokubalika, ni kielelezo mojawapo kuashiria mafanikio kwa kila jambo.

Suala hili ni muhimu zaidi jeshini, amri ikitolewa hakuna kuijadili bali kuitekeleza kwanza kisha kuuliza baadaye. Ndiyo maana jeshi linafanikiwa katika mambo mengi.

Nimekumbuka suala la kuwasiliana kila ninapoitazama serikali na jinsi inavyozungumzia suala la ugonjwa wa mtumishi wake au mwenzao, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Yaani ni kama wale waliokuwa wanajenga mnara wa Babeli. Kila mmoja na lugha yake. Nitafafanua.

Baada ya kimya kirefu sana cha kukataa kusema lolote juu ya afya ya waziri huyu, kunzia alipoanza kuumwa ugonjwa wa ajabu wa kuvimba mwili, ngozi kubabuka na kisha kukimbizwa hospitalini India baada ya tiba za hapa nchini kushindikana, hatimaye serikali kwa nyakati tofauti imethibitisha jinsi ilivyo na ndimi nyingi juu jambo moja linalomhusu Dk. Mwakyembe.

Ulimi wa kwanza kuzungumzia juu ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe, ulikuwa wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye hakutafuna maneno ila alisema wazi kuwa anachougua Dk. Mwakyembe kina uhusiano mkubwa na kulishwa sumu. Sitta alisema wazi, kuwa Dk. Mwakyembe kalishwa sumu.

Baada ya kauli ya Sitta si jeshi la polisi lililotaka kusema lolote, mbali tu ya kumtaka apeleke ushahidi wa hicho anachosema. Lakini mwishowe, Waziri mwenzake, wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye busara ilimwelekeza cha kusema akiwa mkoani Mbeya, akasema “polisi wanachunguza suala la Mwakyembe kulishwa sumu.”

Lakini akawa mwepesi wa kuweka wazi pia kuwa hata kama uchunguzi huo ukikamilika, hawatautoa hadharani kwani suala la ugonjwa wa mtu ni siri yake. Alitaka Mwakyembe mwenyewe aseme anaumwa nini.

Hata hivyo, wiki iliyopita Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alijitokeza na kusema kuwa kadri anavyojua yeye na kwa mujibu wa taarifa walizopata kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu. Kauli hiyo imeamsha taharuki kubwa nchini, watu wamehoji na kudadisi kama si sumu ni nini?

Lakini Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda, akajiweka mbali na taarifa ya Manumba akisema haijui na wala hajui alikoipata. Amewataka wote wanaofutilia suala hilo, wamuulize DCI Manumba ameipata wapi.

Kwa maneno mepesi ni kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo inalipia gharama za matibabu ya Dk. Mwakyembe katika hospitali ya Apollo, India, haijazungumza na polisi juu ya ugonjwa wa Naibu waziri huyo, lakini pia nayo haitaki kusema lolote juu ya ugonjwa huo.

Ingawa Waziri Mponda amekimbiza ubawa wake katika suala la Dk. Mwakyembe, akiomba kabisa wizara yake kutokuhusishwa na lolote kwa kuwa haijui chochote, na wala haijapokea taarifa yoyote, mgonjwa mwenyewe, Dk. Mwakyambe amemwakia Manumba kwa kuibuka na kauli za kushangaza kwamba hajalishwa sumu.

Dk. Mwakyembe amemtuhumu Manumba kwamba alichokisema hakijui na wala hajui amepata wapi taarifa hizo, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi kutomhoji yeye wala kuzungumza na madaktari wake. Zaidi alisema uchunguzi wa afya yake bado unaendelea, hivyo ni vigumu kujua hasa nini kimesababisha matatizo yaliyoko kwenye uboho (bone marrow) wake.

Ugonjwa wa Dk. Mwakyembe, kwa mara nyingine, umethibitisha udhaifu mkubwa wa serikali. Kama mawaziri watatu wa serikali hiyo hiyo wanaweza kuwa na kauli tofauti juu ya jambo moja, ikiongezewa nguvu na kauli tofauti ya Manumba, basi tunajenga Mnara wa Babeli na muda si mrefu utaporomoka.

Kuna nini ndani ya serikali? Sitta anaapa na miungu ya kwao kwamba Dk. Mwakyembe kalishwa sumu; Nahodha anakwepa kuingia kwa undani juu ya kinachomsibu mbali tu ya kusema wanachunguza na hata wakimaliza uchunguzi hawatasema hadharani; Ofisa Mwandamizi ndani ya Wizara yake, DCI Manumba, anasema tena kwa kujiamini: “Si sumu, si sumu.”

Anatamka mara mbili mbele ya waandishi wa habari. Anajishika na Wizara ya Afya na Utawi wa Jamii kwamba ndiyo imempa taarifa hizo, wizara inasema haina taarifa hizo, inataka aulizwe vizuri Manumba alikopata taarifa zake kwani kimsingi ana vyanzo vingi kama kiongozi wa Jeshi la polisi. Dk. Mwakyembe naye anamkana Manumba. Sasa mgogoro wote huu unaeleza nini kwa tafsiri ya kina ya fikra pevu.

Hali hii inawezekana tu kuelezwa katika aina ya utendaji kazi wa serikali inayojenga Mnara wa Babeli tu. Ikumbukwe kwamba tangu ameugua Dk. Mwakyembe mwaka jana mwishoni, umma umetaka kuelezwa kiongozi wao anaumwa nini? Dk. Mwakyembe si sawa na Mbasha Asenga anayeganga tu njaa kwa kuendesha shughuli zake, huyu ni kiongozi wa umma, ofisi yake inaendeshwa kwa kodi za wananchi, majukumu yake ni kuwatumikia wananchi; huyu ni mbunge wa Kyela, amechaguliwa na wananchi.

Si siha njema kisiasa na kiutawala kuacha uvumi tu mitaani juu ya kinachomsumbua kiongozi kama huyu, hasa pale maneno ya kuweko mkono wa mtu yanapokuwa yametumbukizwa humo.

Serikali inayofumbia macho hali kama hiyo ikiendelea huku ikijua ina wajibu wa kuweka mambo sawa, haiwezi kujivua lawama za kujitakia na hukumu ya umma kwamba imeparaganyika kimawasiliano. Ni vema kujiuliza swali, hivi Nahodha, Sitta na Mponda wanahudhuria Baraza la Mawaziri hilo hilo moja chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete? Hapana shaka jibu ni ndiyo. Katika mazingira kama hayo, je, wanazungumza je? Je, kiongozi wao anawaangaliaje?

Watu wanaweza kudhani kuwa suala la mawasiliano ni dogo sana ndani ya mfumo mkubwa kama serikali, lakini kwa hakika kama mawasiliano hayapo ni dhahiri serikali hiyo haipo pamoja. Ni mapande ya serikali, kinachowaunganisha ni kupeperusha bendera ya serikali na kuendeshwa kwenye magari ya serikali na kuhudumiwa kwa kodi za wananchi, lakini utendaji wao na unyenyekevu wao hauko kwa serikali hiyo wala kwa wananchi.

Hali hii hamkani haitaiacha serikali ikiwa imesimama, ni lazima iwe kama Mnara wa Babeli tu; kinachosubiriwa ni wakati.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: