Serikali ya umoja haiepukiki Bara


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MATOKEO ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita nchini yamekiondolea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukiritimba baada ya vyama vya upinzani hususani Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupata matokeo mazuri kwenye uchaguzi huo.

Kuna uwezekano mkubwa wa bunge lijalo la Tanzania kuwa na wabunge wanaokaribia 100 kutoka kambi ya upinzani. Hii itakuwa ni idadi kubwa ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya nchi hii.

Matokeo ya uchaguzi huu si tu kwamba yanaweza kubadili mwelekeo wa nchi katika uendeshaji wa bunge na serikali, lakini unatoa picha ya huko tuendako katika siku za usoni.

Ni wazi, serikali zote zijazo, kuanzia hii itakayoapishwa baada ya uchaguzi huu, zitakuwa na kazi ya kuhakikisha vyama vyote vinashiriki katika mchakato mzima wa kuendesha nchi na si kile tawala pekee.

Hivi ndivyo wenzetu katika nchi zilizoendelea wanavyofanya. Chama tawala huwa kinatumia bongo kutoka katika vyama vya upinzani, watu binafsi na sekta binafsi kufanikisha malengo ya kitaifa.

Kwa mfano, mara baada ya Barack Obama kushinda kiti cha urais nchini Marekani, miaka miwili iliyopita, tukio la kwanza alilofanya lilikuwa kumbakiza Robert Gates, kuwa waziri wa ulinzi wa nchi hiyo.

Gates ni mfuasi wa chama cha Republican wakati serikali ya Obama ni ya chama cha Democrat. Wizara aliyopewa Gates ni miongoni mwa wizara nyeti kabisa katika serikali hiyo. Obama aliamua kumwacha Gates aendelee na wadhifa huo aliopewa tangu enzi za George W. Bush kwa vile alikuwa kiongozi makini na madhubuti.

Alifanya hivyo kwa sababu pamoja na tofauti zao kubwa kiitikadi, Gates alifanya kazi nzuri kama waziri wa ulinzi. Ukizingatia kwamba Marekani bado iko vitani Afghanistan, Pakistan na Irak, hakukuwapo sababu ya kumtoa mtu anayejua vizuri mambo.

Kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita, rais ajaye wa Tanzania ni muhimu akaamua kufuata utaratibu wa wenzetu wa kutoangalia chama chake bali kwingineko na kusikiliza sauti za wale waliochagua vyama vingine. 

Wamarekani wana vita katika ugaidi na kulinda maslahi yao. Tanzania ina vita vya kupambana na maadui wakuu watatu tangu enzi za uhuru; ujinga, maradhi na umasikini.

Kama Marekani inaweka tofauti za kiitikadi pembeni ili wapate ushindi katika mstari wa mapambano, ni wazi Tanzania ina kila sababu ya kufanya hivyo ili kushinda vita dhidi ya maadui hao watatu.

Hata hivyo, kuna tofauti kubwa moja baina ya Tanzania na Marekani ambayo ni muhimu kuieleza mapema. Ni tofauti inayoweza kutumiwa kwa faida ya nchi hii.

Nchini Marekani, mtu anaruhusiwa kikatiba kuwania nafasi yoyote ya uongozi, hata kama hana chama cha siasa. Ndiyo maana, Ross Perot aliwahi kuwania urais wa Marekani enzi za Bill Clinton akiwa mgombea binafsi.

Nchini Tanzania, hilo haliwezekani. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa katiba, mtu haruhusiwi kuwania nafasi yoyote ya uongozi ya kisiasa bila ya kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Tanzania yenye watu milioni 40.4, ina wanachama wa vyama vya siasa wasiozidi milioni 10. Hii maana yake ni kuwa zaidi ya robo tatu ya wananchi hawana vyama vya siasa.

Kwa hiyo, asilimia hiyo kumi ya wenye vyama vya siasa ndio wanaopewa nafasi za uongozi. Na wanabadilishana haohao kiasi kwamba uongozi unaonekana ni suala la kurithishana na kufahamiana.

Miongoni mwa mambo yanayoifanya Tanzania izidi kubaki nyuma katika vita yake dhidi ya maadui hao watatu ni suala hili la kuacha robo tatu ya watu nje ya uongozi.

Kuna watu wengi walio nje ya vyama vya siasa ambao wangeweza kuifanyia nchi makubwa lakini hawawezi kwa sababu hawataki kujihusisha na kile kinachoitwa mchezo mchafu wa siasa.

Kuna kundi jingine la watu walio nje ya vyama hivyo ambao wangeweza kuwa na mchango mkubwa kwa nchi, lakini wanashindwa kufanya lolote kwa sababu vyama vyao haviko madarakani.

Kwa hiyo iwapo mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, atashinda ni vema akamua kuwatumia watu kama Dk. Willibrod Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba, ingawa hawapo katika chama chake.

Aidha, ikiwa Dk. Slaa atashinda au Prof. Ibrahim Lipumba ni vema wakatimiza ahadi zao za kuwatumia watu kutoka vyama tofauti na maeneo tofauti ya fani kwa lengo la kuongeza nguvu katika mikakati ya kujiletea maendeleo na mapambano dhidi ya maadui watatu.

Hivi ndivyo itakavyofanyika Zanzibar. Kwamba baada ya vyama viwili vikuu vya CCM na CUF kufikia maridhiano na kuwekwa ndani ya katiba, mawaziri na watendaji wakuu serikali watateuliwa kuzingatia kwa uwiano wa vyama.

Kama Zanzibar wamefikia uamuzi wa kuunda serikali ya pamoja baina ya vyama hasimu vya CCM na CUF, hakuna sababu kwa nini isiwezekane Tanzania Bara. Hapa kuna haja ya kuunganisha nguvu bila ya kujali itikadi za vyama katika wakati ambapo nchi ina vita ya kupiganwa.

Dunia nzima, kwa sasa, suala la serikali inayoundwa na chama zaidi ya kimoja ni la kawaida kabisa. Mbali ya Marekani, Ujerumani inafanya hivyo na Uingereza hivi sasa kuna serikali inayoundwa na vyama viwili; Conservative na Liberal Democrat.

Wakati mwingine, kuwa na watu wanaofikiri tofauti katika uendeshaji wa serikali ni suala muhimu kuliko kuwa na watu wenye fikra na mtazamo wa aina moja na wanaofikiri kuhusu itikadi zao kuliko kitu kingine.

Hata kiongozi mashuhuri wa China, Mao Ze Dong, alipata kusema ni muhimu kwa watu kuacha aina tofauti za maua 100 yakue kwa pamoja badala ya kuwa na ua moja zuri.

Ni muhimu kwa chama kilichoshinda kipewe fursa ya kuunda serikali. Lakini, Watanzania watakapokuwa wamekipa fursa hiyo ya kuongoza, watakuwa pia wameweka maisha yao na mustakabali wa vizazi vijavyo kwenye mikono ya chama hicho.

Ni jukumu la chama tawala kijacho kufahamu kazi hiyo kubwa iliyo mbele yao. Na ni wazi, kazi hiyo itafanyika iwapo kila mwenye uwezo atashirikishwa bila ya kujali itikadi zake.

0
No votes yet