Serikali yachekelea ‘unga’


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI inafanya mzaha kwa namna inavyoshughulikia tatizo kubwa la biashara na matumizi ya madawa ya kulevya nchini. Hatua inazochukua ni dhaifu zinazolea badala ya kukomesha tatizo.

Wakati viongozi wakihutubia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupiga vita madawa ya kulevya, mitaani askari wanakamata watu ovyo. Wakishawafikisha vituoni na kuchagua ni nani wamshitaki, huwaachia waliobaki. Wengine hupelekwa mahakama ya jiji.

Palepale kwenye vyumba vya waendesha mashitaka, waliokamatwa huulizwa, “Una kiasi gani.” Au mtu huulizwa, “Unayo elfu kumi (Sh. 10,000)?” Akiwanayo, anaachiwa. Asiyenayo anashitakiwa kwa uzembe na uzururaji katika mahakama ya jiji.

Haya yamefanyika Kinondoni, mkoani Dar es Salaam wiki iliyopita. Mara kadhaa tumeshuhudia askari wa Kituo cha Oysterbay wakiendesha operesheni zembe namna hii.

Yawezekana operesheni hizi hufanyika maeneo mengine ya mkoa na nchini, lakini kwa jumla, kumekuwa na mwenendo wa ovyo nchini kuhusu vile serikali inavyoendesha vita dhidi ya biashara na matumizi ya madawa. Kumejaa mzaha na vituko.

Aliposhika tu madaraka mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete alionya wafanyabiashara wa madawa ya kulevya wajirekebishe kwani anawajua. Kilichofuata baadaye ni wananchi kutakiwa watoe taarifa za watu wanaoshiriki biashara hiyo ili wakamatwe na kushitakiwa.

Baadhi ya waliothubutu kufuatilia alikuwa Amina Chifupa (sasa ni marehemu), mbunge kijana katika bunge la nane aliyesema bungeni kuwa anayo orodha ya watu wakubwa wanaofanya biashara hiyo na yupo tayari kuikabidhi polisi.

Haikuchukua muda, alitangazwa amefariki dunia kwa ugonjwa uliozua utata mkubwa hata kwa familia yake.

Tangu hapo, kinachoonekana ni matukio ya kukamatwa vijana wanaomeza madawa hayo wakitokea nchi za mbali na kuingia nchini.

Sasa serikali inajinasibu kuongeza kiasi cha madawa yanayokamatwa, japo viongozi wanajua fika wanaokamatwa, ni walalahoi wanaotumwa na matajiri wa madawa ya kulevya.

Rais, yuleyule aliyeapa kuwakomesha, leo anatuhumu viongozi wa dini kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na kuwataka waache. Mzaha tu.

Ni tofauti na inavyofanywa na nchi nyingi kama vile Colombia ambako dola inaonekana ikisimama kidete kuvunjavunja mitandao ya wauza madawa. Nchini Tanzania, vishindo kama vile hutokea pale serikali inaposakama wanasiasa wa upinzani.

Ni mpaka pale viongozi wenye maamuzi watakapoamua kuacha ufisadi wa kuchumia matumbo, ndipo kazi ya kukomesha biashara na matumizi ya madawa ya kulevya itafanywa kitaalamu na kwa ufanisi. Ni lini tutafika hapo? Viongozi wanalo jibu.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)