Serikali yachelewesha mgombea binafsi


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imeshatangaza mchakato wa maandalizi ya kupata wagombea wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Ubunge la Tarime, mkoani Mara ili kuziba nafasi iliyotokana na kifo cha Chacha Zakayo Wangwe.

Wangwe alikuwa mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Uchaguzi huu unakuja katika mazingira mapya.

Kuna uamuzi wa jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu uliotolewa tarehe 5 Mei 2006 uliobaini kuwepo kwa ibara zinazokinzana katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kufuatia “Marekebisho ya Kumi na Moja” yaliyozuia raia wa Tanzania kugombea nafasi za urais na ubunge bila kupitia vyama halali vya siasa.

Jopo hilo la aliyekuwa Jaji Kiongozi Amir Manento, Jaji Salum Massati (sasa ndiye Jaji Kiongozi) na Jaji Thomas Mihayo, lilibainisha haki ya mgombea binafsi katika jitihada za kupanua demokrasia.

Raia yeyote mwenye sifa zinazohitajika, anaruhusiwa kugombea nafasi hizo bila kupitia chama cha siasa na hivyo kuhalalisha nafasi ya mgombea binafsi. Hapo mahakama ilitoa maelekezo kwa serikali kuweka utaratibu wa kisheria ili fursa hiyo iwepo kabla ya uchaguzi mkuu ujao (2010).

Maneno “kabla ya uchaguzi mkuu ujao” yana maana kwamba iwapo amri ya mahakama ingetekelezwa ipasavyo au mara moja, wagombea binafsi wangeanza kushiriki chaguzi kuziba nafasi zinazojitokeza hivi sasa, ikiwemo hii ya Tarime.

Tafiti nyingi za wanasayansi ya siasa tayari zimeonyesha kuwa, pamoja na sera nzuri ya chama cha siasa, watu kwa kawaida, huvutiwa zaidi na wagombea wenyewe binafsi.

Kama wagombea binafsi wangekuwa wameruhusiwa, yawezekana wangejitokeza katika uchaguzi wa sasa huko Tarime. Lakini kwa nini serikali haijatekeleza amri ya Mahakama Kuu?

Hii imetokana na serikali yenyewe kuamua kupinga uamuzi huo wa mahakama kwa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kwa Shauri la Rufaa Na. 20 la 2007. Hapa ndipo palizaa mnyukano.

Mawakili wa wajibu rufaa, walipinga maombi ya mawakili wa serikali, ya kufungua rufaa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Mroso, Rutakangwa na Kileo, wakakubali pingamizi hilo.

Majaji waliamua “kuiondoa” na sio “kuitupa” rufaa hiyo, ikimaanisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza kuiwasilisha tena kwa utaratibu unaofaa.

Kwa hiyo uamuzi wa mgombea binafsi mpaka sasa unabaki uleule uliotolewa na Mahakama Kuu kwani Mahakama ya Rufaa bado haijapokea rufaa, kuisikiliza na kutamka lolote. 

Historia inaonyesha kwamba uamuzi kama huo uliwahi kutolewa na mahakama lakini serikali ikaupuuza kiasi cha kumsikitisha sana hata Mwalimu Julius Nyerere.

Kilichofanyika ni kwamba baada ya uamuzi wa kuruhusu wagombea binafsi uliofanywa na Jaji Kahwa Lugakingira katika Shauri la Madai Na. 5 la 1993, serikali ilipeleka bungeni haraka muswada wa sheria Na. 34 ya 1994 iliyorekebisha vifungu vya 21 (1), 39 (1) (c) na 67 (1) (b) vya Katiba ili kuondoa kabisa haki hiyo.

Kwa mfano, awali Ibara ya 21 (1) ya Katiba ilisomeka, “Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”

Ibara hiyo sasa inasomeka kama ifuatavyo, “Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 39, ya 47 na ya 67 ya Katiba hii na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za  utawala wa nchi kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”

Hoja inajengwa kuwa maneno “BILA KUATHIRI MASHARTI YA IBARA YA 39, ya 47 na ya 67” ndiyo yaliyowanyima Watanzania haki ya “mgombea binafsi katika urais na ubunge,” kwani ibara zinazotajwa zinaeleza masharti ya kugombea urais na ubunge, yakiwemo ya kuwa mwanachama wa “chama chochote halali cha siasa.”

Masharti hayo yapo pia kwa wagombea udiwani kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa ambayo, Katiba katika kibwagizo cha Ibara hiyo 21 (1) inasema, “…Kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”

Hayo ni baadhi ya matatizo ya Katiba yetu ambayo wanazuoni wa masuala ya katiba na haki za binadamu wanasema ni katiba inayotoa haki na kunyang’anya haki hizo.

Hii inadhihirishwa na kuwepo ibara zinazokinzana na ibara zingine katika Katiba, hususani zile za haki na wajibu; kuanzia Ibara ya 12 hadi 29 na matamko au mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.

Kwa mfano, Ibara ya 20 (2) ya Katiba inakataza kumlazimisha mtu kujiunga na chama chochote. Lakini Ibara za 39 na 67 zinasema ili Mtanzania agombee urais au ubunge anapaswa awe “ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.”

Huo ndio mgongano ndani ya Katiba. Usingekuwepo, Tarime ungekuwa uwanja wa kwanza wa wagombea binafsi tangu haki hiuyo ilipopokonywa na mfumo wa chama kimoja mwaka 1965.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: