Serikali yafadhili kampeni za CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Msemaji ikulu agoma kuongea
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu

MABILIONI ya shilingi yatachotwa kutoka serikalini kugharamia kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.

Fedha hizo zitagharamia utengenezaji picha zitakazotumiwa na CCM na mgombea wake, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza 20 Agosti 2010.

Kampuni iliyomo kwenye mradi huu imefahamika kuwa ni Mediapix International Limited kutoka nchini Canada.

Kwa mujibu wa mawasiliano kati ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu, mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za CCM, Abdallahaman Kinana, na wawakilishi wa kampuni hiyo, William Sarakikya na Zahur Ramji, mkataba kati ya CCM, serikali na Mediapix ulifungwa 22 Juni 2010.

CCM na serikali wamejifunga kuilipa Mediapix kiasi cha dola za Marekani 1.5 milioni (sawa na Sh. 2.17 bilioni).

Kwa mujibu wa mkataba huo, serikali ilipaswa kufanya malipo ya dola za Marekani 750,000 ifikapo 24 Juni 2010.

Malipo ya mwisho ambayo ni asilimia 50 ya gharama ya kazi, yalipaswa kufanywa 7 Julai 2010.

Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, unahusu utengenezaji wa picha za mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika saizi tofauti.

Nyaraka zinaonyesha kampuni hiyo ndiyo itakayotengeneza picha zitakazotumika kwenye mabango makubwa (billboards) ambazo zitasambazwa kote nchini.

Katika hili, mkataba unasema ubunifu huo wa picha utakuwa na haki miliki ambayo itabaki kuwa mali ya Ramji, ambaye hafahamiki uraia wake.

Ankara mbili za malipo zenye Namba. MPX/CCM-TZGOV 2010/2713 na MPX/CCM-TZGOV 2010/2717 zilitumwa kwa serikali na CCM, 22 Juni 2010.

Nyaraka zinaonyesha kuwa ankara hizo za malipo ni kwa ajili ya utengenezaji wa picha 600,000 zenye ukubwa wa A3, zikitokea katika kivuli cha kijani.

Aidha, zitatengenezwa picha nyingine 200,000 za Rais Kikwete zenye ukubwa wa A4 na ambazo zitatokea katika kivuli cha njano.

Picha nyingine 200,000 zenye ukubwa wa A4 zinatakiwa kutokea katika kivuli cha kijani.

Kwa mujibu wa mkataba, mabilioni hayo ya shilingi yalipaswa kuwekwa katika Akaunti iliyopo Royal Bank of Canda.

Benki hiyo ipo Mtaa Na. 571 Sandhulst Circle, Scarbourgh, Ontario MIV 1V2, Simu: 416 292-6701.

Taarifa ambazo gazeti hili limepata zinasema mkatana huu umeikosesha serikali kodi mbalimbali ikiwamo kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Fedha hizo za VAT zilipaswa kulipwa nchini Canada na hivyo vifaa hivyo kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru wa VAT.

Mkataba unasema kwamba iwapo wenye mkataba wanataka kuongeza idadi ya bidhaa zaidi ya hizo zilizoagiwa, vifaa vipya vitaingizwa kutokana na mabadiliko ya bei na gharama za usafirishaji za wakati huo.

Aidha, mnunuzi atawajibika kulipa gharama zote kwa kila shehena itakayokuwa inaingia nchini.

Kuhusu malipo, taarifa za mawasiliano kati ya Salva na wenye mkataba zinaonyesha kuwa yatafanywa kwa Mediapix International Ltd kabla ya hatua yoyote ya kutumia picha nchini.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa ingawa vifaa hivyo vimeagizwa kwa anwani za Canada, vinatengenezwa nchini China na vinatarajiwa kuingizwa nchini katikati ya mwezi huu.

Hii ni mara ya pili kwa CCM na serikali yake kutuhumiwa kutumia fedha za walipakodi kugharimia shughuli zake za uchaguzi.

Mwaka 2005, CCM ilituhumiwa kutumia baadhi ya viongozi wake waandamizi kukwapua mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kulipia gharama zake za uchaguzi.

Moja ya makampuni yanayotuhumiwa kukwapua mabilioni hayo ya shilingi, ni Kagoda Agriculture Limited.

Kwa mujibu wa mawasiliano ya barua pepe iliyoandikwa na Ramji, Jumapili ya Julai 4 mwaka huu, saa moja na dakika 55 asubuhi, kwenda kwa Salva, Mediapix ilikubali kazi ya kutengeneza picha za kutumika kwenye mabango.

“Kwa mujibu wa makubaliano yetu ya Juni 22 mwaka huu, Pro-forma Invoice Na. MPX-CCM/GOVTTZ-2010.619, tutawatumia picha kwa ajili ya matumizi ya kwenye mabango. Tunaomba picha hizo zitumike kwa ajili hiyo tu na si vinginevyo,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Kabla ya hapo, Sarakikya alikuwa amemwandikia Salva, Jumamosi ya Julai 3 mwaka huu, saa nane na dakika 20 na sekunde 11, akisema kwamba picha zilizotumwa awali na Mediapix kwa ajili ya mabango ni ndogo na zisingefaa kwa ajili hiyo.

“Kwa mabango, tunahitaji picha zenye saizi isiyopungua 300dpi na ukubwa wa 50Mb. Picha tuliyoletewa ina ukubwa wa 216Kb na haitafaa kwa kazi hiyo,” inasema sehemu ya barua pepe hiyo.

Katika barua hiyo, Sarakikya alimwambia Salva kuwa inabidi picha zenye saizi inayotakiwa zitumwe haraka kwa vile muda uliobaki ni mdogo.

Siku hiyo hiyo, saa 12 na dakika nane na sekunde 46, Salva alimwandikia baruapepe Sarakikya kumhakikishia kwamba ombi lake litatimizwa haraka iwezekanavyo.

“Tayari nimezungumza na mwenyekiti wetu, mzee Kinana (Abdulrahman Kinana ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM) na mpiga picha Ramji kuhusu suala lako. Amekubali hilo lakini kwa masharti yafuatayo:

“Kwamba kwanza utatumia picha hiyo kwa ajili ya mabango pekee na si kwa ajili ya kitu kingine chochote…na mazungumzo haya yataendelea kuwa siri kati yetu,” ilisema barua hiyo ya Salva.

Katika barua pepe hiyo, Salva anamtaja Kinana kama “mwenyekiti wetu” wakati yeye (Salva) si mwajiriwa wala mtumishi wa CCM ambayo ndiyo itakayonufaika na matumizi ya picha hizo.

Mkataba baina ya CCM, serikali na Mediapix ulisainiwa 22 Juni mwaka huu na ulisimamiwa na kampuni ya wanasheria ya Jane Barvey Associates Lawyers, yenye ofisi zake katika mtaa wa 300 Borough, Toronto, Canada.

Hata hivyo, pamoja na kusimamiwa na kampuni hiyo ya Canada, mkataba huo umeeleza kuwa utafuata sheria na taratibu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndani ya mkataba huo, Mediapix imepewa haki ya kuteua kampuni yoyote itakayotaka kuchapa picha hizo kwenye kofia au fulana.

Mkataba huo unaonyesha kwamba CCM imeamua kuchapa kofia na fulana zake nchini China, na Mediapix imepewa haki hiyo kuhakikisha ubora wa picha zake hauharibiwi na kampuni itakayozitumia kwenye kofia na fulana.

Alipoulizwa Salva juu ya ikulu kuhusika katika mpango huo, awali alisema, “Aah…nipigie baadaye kidogo.” Alitafutwa tena, lakini hakupatikana.

Hata hivyo, baada ya muda kupita, Salva alipiga simu na kutaka kukutana na mwandishi wa MwanaHALISI katika hoteli ya Southern Sun iliyopo karibu na Ikulu ya Dar es Salaam.

Mwandishi alipomfuata, Salva aligoma kuzungumza akitaka kuonyeshwa kwanza nyaraka ya kile ambacho alidai gazeti inalo. Alisema angeweza kuongea lolote baada ya kupatiwa nyaraka hizo.

Gazeti lilimkatalia kumuonyesha nyaraka ilizonazo na hivyo naye akasisitiza kuwa hayuko tayari kueleza ushiriki wake.

Hata hivyo, nyaraka zinaonyesha Salva alifanya mawasiliano mara kadhaa na Sarakikya, Kinana na Ramji jinsi ya kufanikisha “mpango huo.”

Katika mawasiliano hayo Salva anasema, “Nakushukuru sana kwa kikao tulichofanya Jumamosi hii asubuhi (3 Julai 2010) na kufanikiwa kubadilisha imeili zetu kuhusiana na suala la picha za kampeni.”

Akiandika kwa msisitizo, Salva anasema, “Wote wana matumaini kuwa shehena italetwa haraka… makubaliano rasmi yatatiwa saini Jumatatu…”

Mawasiliano hayo ya imeili yalinakiriwa kwa Januari Makamba, Sarakikya, Kinana na Ramji.

MwanaHALISI lilipomtafuta Sarakikya ambaye kwa mujibu wa nyaraka zilizopo anatoka kampuni ya A1 Outdoor ya Dar es Salaam, kueleza kuufahamu mpango wa ikulu alisema, “mimi si msemaji wa kampuni.”

Alipong’ang’anizwa kwamba ametajwa katika mawasiliano ya Salva, Kinana na Ramji, Sarakikya alisema, “Sifahamu lolote katika hilo.”

Jitihada za kupata maelezo ya Ramji hazikufanikiwa baada ya gazeti hili kutojibiwa ujumbe aliotumiwa kupitia anuani yake ya barua pepe: zahur@hotmail.com

Naye, Yusuf Makamba hakupatikana, pamoja na juhudi kubwa za kumtafuta kwa simu yake ya mkononi. Kwa upande wa Kinana, simu yake ilikuwa inaita bila kujibiwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: