Serikali yafichua kigogo wa Dowans


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version
Ni Mtanzania, kiongozi wa CCM
Hoseah kung'olewa TAKUKURU
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU), Dk. Edw

MAKAMPUNI ya kuzalisha umeme ya Richmond na Dowans yanamilikiwa na mtu mmoja, MwanaHALISI limegundua.

Vyanzo mbalimbali vya taarifa ndani ya serikali vimekiri pia kwamba hayo ni makampuni ya mfanyabiashara mmoja mashuhuri raia wa Tanzania.

Kupatikana kwa taarifa hizo kumefuta madai ya baadhi ya viongozi nchini waliokuwa wakisema kuwa Dowans ni kampuni iliyosajiliwa nchini Costa Rica, Marekani Kusini.

Lakini taarifa zinasema kuwa serikali imethibitishiwa na Mwanasheria Mkuu wa Costa Rica kwamba nchini humo hakuna kampuni inayofahamika kwa jina la Dowans.

Aidha, imefahamika kuwa akaunti za kampuni ya Dowans, ambayo mfanyabiashara Rostam Aziz amewahi kukiri kufahamiana kibiashara na maofisa wake, ziko Dubai, Falme za Nchi za Kiarabu.

Taarifa hizi zimeleta mshangao na maswali mengi, kwani wachunguzi wa mambo wanauliza, kama akaunti ziko Dubai, nani amekuwa akikusanya fedha kila mwezi kwenye dirisha la hazina.

Vyanzo vya habari vya gazeti hili vinasema wafanyakazi wa kampuni ya mfanyabiashara mmoja jijini Dar es Salaam ndio walikuwa wakikusanya fedha hizo.

"Ilifikia mahali kigogo mmoja wa Hazina akawasiliana kwa barua na Ikulu kueleza nani hasa alikuwa anaagiza au kukusanya fedha hizo, na wakati mwingine kuleta rabsha pale anapocheleweshewa malipo," vimeeleza vyanzo vya habari.

Kupatikana kwa taarifa kuhusu makampuni haya kunaondoa utata, siyo tu juu ya umiliki wake bali pia nani amekuwa akichota mamilioni ya shilingi kutoka hazina kugharimia mradi huu.

Kwa karibu miaka miwili sasa, mmiliki wa makampuni haya amekuwa akikinga Sh. 152 milioni kutoka Hazina kila mwezi kama gharama za mitambo bila kujali kama umeme umezalishwa au haukuzalishwa.

Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri unaoanza tarehe 10 mwezi ujao, unatarajia kuelezwa ugunduzi huu wa mmiliki wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakapokuwa anatoa taarifa ya serikali ya utekelezaji wa mapendekezo ya Ripoti ya Kamati ya Dk. Harrison Mwakyembe.

Ni katika mkutano huo wa Bunge, Pinda ataorodhesha hatua zilizokwishachukuliwa na serikali katika kutekeleza mapendekezo 23 ya Kamati ya Mwakyembe.

Moja ya hatua ambazo zinatarajiwa kutangazwa ni ile ya serikali kutekeleza maoni ya Kamati ya kumwajibisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah.

Taarifa kutoka serikalini zinasema Hoseah ataondolewa kwenye nafasi yake kabla ya Mkutano wa 12 wa Bunge kuanza mjini Dodoma.

Kamati ilipendekeza Hosea awajibishwe kwa sababu alilitia aibu taifa kwa kutoa taarifa potofu kuhusu mkataba kati ya serikali na Richmond.

TAKUKURU ilisema kwamba mkataba wa Richmond haukuwa na matatizo na kwamba serikasli ilikuwa haijapoteza lolote katika kuwa kwenye mkataba huo.

Mwingine ambaye anatarajiwa kung?olewa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Athur Mwakapungu ambaye anaponzwa na kushiriki kwake katika mchakato mzima wa kutoa zabuni kwa Richmond na kuficha ukweli kwa Kamati ya Mwakyembe.

Taarifa zinasema huenda Mwanasheria mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika akasalimika kutokana na mfumo wa utendaji ndani ya ofisi yake. Haikuelezwa zaidi.

Hata hivyo imefahamika kuwa baadhi ya watendaji katika ofisi hiyo watawajibishwa kutokana na kushiriki kwao katika mchakato mzima wa mkataba huo.

MwanaHALISI limedokezwa kwamba, kwa sasa serikali inafanya taratibu za kisheria kuona namna ya kusitisha malipo hayo ambayo tafsiri yake ni kuvunja mkataba na Dowans.

Uamuzi huo wa serikali umechochewa na taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Costa Rica kwa Kamati Teule ya Bunge kwamba nchini humo hakuna kampuni inayoitwa Dowans.

Dowans ambayo imekuwa inadaiwa kusajiliwa Costa Rica iliingiza ndani ya nchi mitambo kutokea Afrika Kusini huku akaunti zake zikiwa Dubai.

Katika uchunguzi wake, MwanaHALISI imebaini, serikali kwa kupitia Timu Maalumu (Task Force) iliyoundwa na waziri mkuu, pamoja na mambo mengine, ilipitia mkataba kwa kina na kuona namna ya kusitisha malipo kwa Dowans.

Tayari serikali imefungua akaunti maalum kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zingekuwa zinatiririkia kwenye mikono ya Dowans hadi "kieleweke."

Bunge la bajeti linatarajiwa kuanza Juni 10 huku joto la kisiasa nchini likiwa juu, kufuatia tuhuma mbalimbali za ufisadi na mawaziri kuendelea kujiuzulu kwa tuhuma hizo.

Katika mkutano wa 10, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na wenzake Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, walijiuzulu kutokana na mkataba wa kifisadi wa Richmond/Dowans.

Hata hivyo, waziri mkuu amethibitisha kuwa viongozi wote waliojiuzulu, wanafuatiliwa kwa makini ili kujua walivyohusika katika kashfa za ufisadi.

Pinda alikuwa akiongea na waandishi wa habari, juzi Jumatatu juu ya hatua za serikali katika kutekeleza mapendekezo ya kamati ya bunge. Alisema fikra za serikali ni kwamba "haitoshi kwa viongozi hao kujiuzulu."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: