Serikali yakosa uvumilivu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 22 July 2008

Printer-friendly version

HATUA ya polisi kuvamia ofisi za MwanaHALISI na kupekua kompyuta kwenye chumba cha habari na nyumbani kwa mtedaji mkuu wa gazeti hilo, ni ushahidi tosha kwamba sasa serikali imekosa uvumilivu.

Kisingizio ni kwamba kompyuta hizo zina taarifa za benki za baadhi ya akaunti za wateja.

Kama kwamba hiyo haitoshi, Mkurugenzi wa Upelelezi nchini Robert Manumba aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi iliyopita kwamba Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers, wachapishaji wa MwanaHALISI, Saed Kubenea anaweka taarifa hizo kwenye mtandao wa intaneti.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kukiri ujinga na kutokubali kujifunza katika suala hili. Wakati gazeti limechapisha taarifa, na gazeti hilo limesajiliwa kwenye mtandao wa intaneti, lazima taarifa zote zilizomo kwenye gazeti zitaonekana kwenye mtandao.

Hapa ndipo serikali inahitaji darasa. Magazeti yote makubwa ndani na nje ya nchi, na yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa yamejisajili kwenye intaneti.

Kila toleo likitoka, linawekwa pia kwenye intaneti. Kwa hiyo linaweza kusomwa mitaani au kwenye intaneti.

Wenye intaneti maofisini hawana haja ya kulinunua mitaani. Hatua ya polisi kupekua ofisi za MwanaHALISI, kwa hiyo, inadhihirisha kuwa ama serikali hawasomi gazeti hilo au kama wanalisoma basi "limewachosha" kwa taarifa za ndani zaidi ambazo zimekuwa mtindo wake.

Kwa mwaka huu peke yake MwanaHALISI limechapisha taarifa juu ya akaunti za makampuni ambayo yanadaiwa kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu na Wizara ya Fedha.

Aidha, gazeti hili limewahi kuchapisha baadhi ya akaunti za watu binafsi ambao wanahusishwa kwenye tuhuma za rushwa na ubadhilifu wa kiwango cha juu.

Hakuna ubishi, kama alivyosema Manumba, kwamba taarifa za akaunti ni siri kati ya mwenye akaunti na benki yake. Kama kuna malalamiko basi mwenye akaunti adai benki na benki ieleze jinsi ilivyotoa taarifa hizo.

Hapa basi hakuna nafasi ya polisi kupekua gazeti. Hata hivyo, akaunti inayoshukiwa kuwekwa mabilioni ya fedha za umma, siyo tena akaunti ya siri.

Hata mwenye akaunti hiyo anakuwa amepoteza hadhi ya siri zake kuhusiana na akaunti yake au akaunti zake, kama ana nyingi.

Pale ambapo zimeingia fedha za umma panaondolewa pazia ili zionekane zimekwenda huko vipi na kwa sababu gani.

Pale ambapo bado kuna tuhuma, akaunti zinaweza kutumika kujenga mashaka na hatimaye kuondoa mashaka hayo kuhusu upatikanaji wake. Lakini siri kati ya benki na mteja wake sharti ilindwe na hao wawili.

Gazeti la MwanaHALISI au gazeti lolote lile halina wajibu wa kulinda siri za akaunti ya mtu yeyote. Walinzi wa siri watakapokuwa wazembe na kinachoitwa siri kikavuja, hawapaswi kulalama wala kuajiri polisi kuwafanyia upelelezi.

Manumba anasema kuwa akaunti za watu binafsi zimeanikwa na yeye yuko kazini kutafuta mwenye taarifa. Hii haipaswi kuwa kazi ya polisi.

Bali hatua hii inaweza kusaidia kuibua hoja: Je, ni watu gani, wa hadhi gani wanaweza kuajiri polisi wa nchi hii kuwafanyia kazi? Hakuna akaunti ya mkulima wa Muleba au Tandahimba au Kiraracha ambayo imewahi kuanikwa na gazeti.

Hakuna akaunti ya mfanyabiashara asiyeshukiwa ambayo imewekwa hadharani na hakuna anayeihitaji.

Hakuna hata mwenye shauku ya kujua kiasi alichonacho mkulima au mfanyabiashara mlipa kodi.

Kwa msingi huu, kupekua gazeti kwa misingi ya kutaka kujua "taarifa za akaunti binafsi" za baadhi ya watu wenye uwezo wa kuajiri serikali kuwafanyia kazi, ni kuingilia haki ya gazeti au chombo chochote kukusanya, kupokea na kusambaza taarifa.

Katika lugha ya kawaida, upekuzi huu ni njia ya kusambaza vitisho; kutaka kuziba mdomo wa gazeti; kuua jicho la wananchi na kuziba sikio la umma.

Kama hivyo vyote visingekuwepo katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, kungekuwa na uelewa mdogo sana juu ya taifa hili linavyoangamizwa na wale waliopewa uongozi katika ngazi mbalimbali.

Kwa kipindi cha miezi 10 niliyokuwa mshauri wa MwanaHALISI, nimegundua uwezo wa gazeti hili kutafuta, kupata, kuchapisha na kuhifadhi baadhi ambazo zinasubiri "siku ya mvua."

Miongoni mwa viongozi wote wanaoshukiwa kushiriki ufisadi, hakika hakuna hata mmoja ambaye akaunti yake haitalifikia magazeti makini.

Magazeti na vyombo vingine vingi vya habari vina taarifa mbalimbali za akaunti, biashara au uhusiano miongoni watuhumiwa. Hili serikali inalijua. Polisi pia wanalijua.

Kwamba sasa wameanza kupekua MwanaHALISI, ni ishara kuwa wataendelea kupekua ofisi za magazeti na kanda za redio na televisheni.

Kila mwenye macho anaona kuwa kiama cha vyombo vya habari kimewadia. Katika hili la MwanaHALISI kuna mambo mengi ya kutilia mashaka.

Waliokwenda kupekua kompyuta hawakuwa na ushirikiano. Walikuwa na kichota taarifa kutoka kwenye kompyuta walichokuwa wakitumia kuchota taarifa ambacho hawakutaka kifunguliwe ili maofisa wa gazeti wajue kuna nini.

Katika mazingira ya "kutafuta mchawi," wahusika wanaweza kuwa wameacha chochote katika kompyuta wanazodai walikagua ili kuthibitisha kupatikana kwa kile ambacho walikuwa wanahitaji.

Vilevile katika mazingira ya kutatanisha, waliokuwa wakikagua waligeuka mbogo pale wapigapicha wa magazeti na televisheni walipoingia chumba cha habari na kuanza kazi zao.

Wapekuzi walidai kwamba wao hawapigwi picha na kwamba wangeombwa ruhusa.

Kitendo cha kukataa kupigwa picha kilionyesha jambo moja kubwa:
Kwamba huenda wataalam wao walikuwa wamekodishwa kutoka makampuni ya kutoa ushauri na kuwa wangeonekana wakifanyakazi chafu, basi taasisi zao zingetiliwa mashaka na biashara yao kuharibika.

Je, kama gazeti lingekuwa na uwezo wa kuwa na kamera za kupiga picha tangu mtu akiwa nje hadi anapokuwa ndani, kama ilivyo katika mabenki mengi, wangelalamika vipi kuwa hawapigwi picha? Je, hawana akaunti benki?

Wanapokwenda benki ambako wanachorwa na kamera tangu mwanzo hadi mwisho, mbona hawalalamikii kupigwa picha?

Nikiwa mshauri wa masuala ya taaluma ya habari wa gazeti hili, nimeambiwa wana mpango wa kuweka kamera hizo si muda mrefu kutoka sasa.

Si polisi wajue mapema basi, kwamba siku watakaporudi, ingawa hakika hawahitajiki, watakaribishwa na kamera kuanzia barabara kuu?

Upekuzi wa ofisi za magazeti, hapa nchini au katika nchi yoyote ile duniani, ni aina ya vitisho inayotumiwa na serikali kuingilia na hatimaye kuua uhuru wa watu wa kukusanya, kupokea na kutawanya taarifa na mawazo.

Hatima yake ni kuua hata uhuru wa kufikiri. Taifa lisilokuwa na uhuru wa kufikiri, huswagwa kama kondoo wanaochungwa na mchungaji wa kukodisha; hana uchungu, hathamini utu, anafanya mazingaombwe hata katika ofisi kuu ya nchi na hataki kurekodiwa kwa matendo yake.

Ni wazi sasa kwamba shinikizo la kupekua gazeti hili na baadaye vyombo vingine vya habari, linatokana na msimamo wa kufichua kashfa nyingi zinazokabili viongozi na serikali yenyewe.

Ufumbuzi si kutaka kuua MwanaHALISI. Ufumbuzi ni kupambana kuondoa madhila yaliyopo; kujenga uwajibikaji, uwazi na kuwa na utawala wenye maadili. Huko ndiko gazeti hili limekuwa likiisadia serikali kuelekea.

Vyovyote itakavyokuwa, MwanaHALISI linastahili shukrani kwa kazi nzuri ya kusaidia watawala kujiona walivyo na matatizo yanayowakabili, badala ya kufikiria kulizulia majanga na kutaka kuliua.

Anayefikiria kuua MwanaHALISI nikama anayeandaa mauaji ya halaiki. Hafai.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: