Serikali yaleta muswada kinyemela


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version

SERIKALI imetoa kimyakimya toleo jingine la Muswada wa Marekebisho ya Katiba, MwanaHALISI limegundua.

Katika toleo jipya, linaloweza kuitwa muswada mpya kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa, mambo yote ambayo awali yalitajwa kuwa ni nyeti na yasijadiliwe, sasa yanajadiliwa.

Mambo hayo ni pamoja na Muungano wa Tanzania, taasisi ya urais, Bunge, Mahakama na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.

Kifungu cha 9 cha muswada ambao MwanaHALISI imefanikiwa kuupata juzi, kinatamka kuwa mambo yote hayo sasa ni ruhusa kwani yajadilika.

Toleo la kwanza la muswada lilikosolewa sana na hata kupingwa na wasomi, asasi za kijamii, majaji wastaafu, watu mashuhuri nchini na wananchi katika makundi tofauti na mtu mmojammoja.

Kasoro kubwa zilizoibuliwa zilihusu namna ya kupata maoni, mchakato wa kupitisha katiba ulioegemea upande wa serikali na kutokuwepo utaratibu wa kura ya maoni ili kuidhinisha katiba.

Kasoro nyingine zilihusu kumpa rais mamlaka makubwa katika kuamua jinsi ya wa kupata katiba; kushindwa kwa muswada kuweka nafasi ya Zanzibar katika mchakato huu na muswada kuwa katika lugha ya Kiingereza.

Katika toleo la sasa lililochapishwa Mei mwaka huu, kuna mabadiliko hasa pale serikali na viongozi wa Zanzibar wanapotajwa.

Kwa mujibu wa toleo hili, kutakuwa na kura ya maoni itakayosimamiwa na kuendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kama asilimia 65 ya watakaopiga kura Tanzania Bara na asilimia ya 65 ya watakaopiga kura upande wa Zanzibar wataikubali katiba mpya, basi itapata uhalali.

Muswada huu sasa umechapishwa katika lugha mbili – Kiswahili na Kiingereza, na unatarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa kusomwa kwa mara ya pili.

Toleo la kwanza la muswada lilisomwa bungeni kwa mara ya kwanza Aprili 5, mwaka huu.

Tayari kuna mazingira ya kuibuka kwa utata wa kisheria ambao unaweza kuikumba serikali kuhusu muswada kuwasilishwa bungeni kwa mara ya pili.

Hoja zinasema je, huu si ni muswada uleule wa awali ambao ulikuwa katika Kiingereza?

Hapa kuna kinachoonekana kuwa muswada mpya na wenye mambo mengi mapya na katika lugha ya taifa – Kiswahili.

Kwa hiyo, muswada unapaswa kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni, kwani ule uliosomwa Aprili uliondolewa bungeni, siyo kwa masahihisho madogo bali kwa kuwa haukukidhi matakwa ya katiba mpya au mabadiliko ya katiba.

Hili hata serikali yenyewe ilikiri ndipo ikaridhia kuondoa muswada.

Aidha, toleo la awali lilikuwa halieleweki kwa wananchi wengi wasiojua Kiingereza.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji, amesema muswada “…unapaswa sasa kusomwa kwa mara ya kwanza” kwa kuwa ni tofauti na muswada wa awali ulioondolewa bungeni.

Mtaalamu mwingine wa sheria ya katiba, Profesa Hamudi Majamba wa Chuo Kikuu cha Dar es Saaam (UDSM), amekuja na msimamo huohuo.

Anasema muswada huo una mambo mengi mapya; hivyo utakaposomwa bungeni, hakika maudhui yake yatakuwa yanasomwa kwa mara ya kwanza na siyo ya pili.

Maprofesa Shivji na Majamba walikuwa wakifundisha wanasheria na waandishi wa habari misingi na namna ya kutunga katiba, katika semina iliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Hata hivyo, pamoja na ukweli unaoelezwa na magwiji wa sheria, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaweza kukaidi hekima hiyo na kuendelea kuupeleka bungeni na kuusoma kwa mara ya pili.

“Hapa tatizo litakuwa serikali kutaka kuonyesha ubabe na kutokiri kuwa muswada wa awali ulipingwa na kukataliwa hadi kuondolewa bungeni,” ameeleza kiongozi mwandamizi serikalini ambaye hakutaka kutwajwa jina.

Katika toleo la sasa la muswada, maneno “marekebisho ya katiba” yamebakishwa ili kusisitiza kuwa serikali haina nia ya kuwa na katiba mpya bali iliyorekebishwa tu.

Hata hivyo, kuna mabadiliko makubwa katika toleo hilo jipya, yanayojibu hoja na malalamiko ya uongozi wa Zanzibar.

Kwa mfano, sasa imetamkwa kuwa mbali na ushauri, itabidi mpaka mamlaka ya nchi Zanzibar ikubali ndipo jambo lolote litendeke chini ya muswada huu.

Kwa maana hiyo, sasa hakuna jambo lolote litakalofanywa na Rais wa Jamhuri kuhusiana na suala la marekebisho ya katiba, kwa mujibu wa muswada huu, ambalo Rais wa Zanzibar hatatakiwa kutoa ushauri na kuafiki.

Kwa mfano, kifungu cha 5 cha muswada huo kinampa Rais wa Jamhuri mamlaka ya kuunda Tume ya Marekebisho ya Katiba baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar.

Hilo litafanyika baada ya marais hao wawili kushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kifungu cha 6 kinatamka kuwa rais atashauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba.

Katika kifungu cha 8, rais anapewa mamlaka ya kuunda hadidu za rejea za Tume baada ya kushauriwa na kukubaliana na Rais wa Zanzibar.

Kifungu cha 9 cha muswada kinaitaka Tume kuzingatia maadili na “utamaduni wa Kitanzania” katika kushughulikia mambo kwa “misingi ya muungano wetu.”

Utamaduni unaoainishwa ni pamoja na kuwepo taasisi za Urais, Bunge na Mahakama, aina ya utawala ambapo Tanzania ni Jamhuri, kuwepo kwa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, umoja, amani, utulivu na utengamano, uchaguzi wa mara kwa mara, ulinzi wa haki za binadamu na nchi kutokuwa na dini.

Safari hii muswada unaitaka Tume ikishamaliza kazi, ikabidhi nakala mbili za ripoti yake – moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na nyingine kwa Rais wa Zanzibar.

Katika toleo la awali la muswada wa marekebisho ya katiba, serikali ilipendekeza kuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba ikabidhi ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ambaye angempa nakala Rais wa Zanzibar.

Jambo hili lilizua manung’uniko upande wa Zanzibar kwamba kiongozi wao huyo amedharauliwa kwa kufanywa mtu wa kuulizwa tu ushauri.

Aidha, Kifungu cha 20 cha muswada kinampa mamlaka rais, kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, kuteua wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Marais watakuwa wameshauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Profesa Shivji ameelezea wasiwasi kuhusu uwezekano wa watawala kutumia mwanya huo kuingiza wabunge wa sasa wa Bunge la Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

“Ikitokea hivyo, wananchi watakuwa wamenyimwa haki yao ya kushiriki kutunga katiba yao ambayo wangeipa uhalali wa kisheria na wa kisiasa,” amesema Pofesa Shivji.

Anachokihofia profesa kiliwahi kutokea mwaka 1962 wakati wa kutunga Katiba ya Jamhuri ambapo bunge la kawaida lilijibadili na kuwa Bunge la Katiba; na mwaka 1977 wakati wa kutunga Katiba ya sasa ambapo Mwalimu Nyerere aliwateua wabunge wote waliokuwa bungeni kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba.

Muswada unawataja moja kwa moja, wanasheria wakuu wa Tanzania na Zanzibar, kuwa wajumbe wa Bunge hilo maalum la katiba.

Pia, Katibu wa Bunge la Jamhuri anatajwa kuwa atakuwa Katibu wa Bunge la Katiba na Katibu wa Baraza la Wawakilishi atakuwa Naibu wake.

Kifungu cha 22(3) cha muswada kinampa uwezo Katibu wa Bunge la Katiba, kwa kushauriana na Naibu wake, kuteua baadhi ya wafanyakazi kutoka Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuwa wafanyakazi wa Bunge Maalum la Katiba.

Muswada unazipa NEC na ZEC – tume ambazo zimekuwa zikilalamikiwa sana kwa kutokuwa huru na kutumiwa kupendelea CCM – mamlaka ya kusimamia na kuendesha kura ya maoni juu ya katiba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: