Serikali yapora haki ya wanafunzi vyuoni


Stanislaus Kigosi's picture

Na Stanislaus Kigosi - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version

KWA lugha nyoofu, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haitaki upinzani wala wapinzani waliomo kwenye taasisi za elimu ya juu. Hii ni hofu ya kuondolewa.

Hofu hii ilianza tangu uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Miaka michache baadaye, serikali iliingilia kazi ya kupanga wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili kuzima mbegu za maarifa zilizochukuliwa na watawala kuwa ni upinzani dhidi ya CCM.

Baadhi ya wahadhiri walioonekana kuwa mwiba kwa serikali na waliokuwa wanawajuvya wanafunzi kuona udhalimu wa serikali, walipangiwa uhamisho.

Hata hivyo, wahadhiri hao wakiwemo Prof. Seith Chachage na Prof. Mwesiga Baregu walikataa uhamisho.

Mwaka jana serikali ilimkata maini Baregu kwa kusitisha kibarua chake UDSM kwa madai kuwa anajihusisha na “masuala ya siasa” wakati ni mtumishi wa umma.

Safari hii, serikali imefanya kituko kingine. Imehimiza wanafunzi wa elimu ya juu kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, lakini imewapora haki yao ya kupiga kura. Huu ndio uvunjaji wa haki za binadamu.

Wanafunzi walijiandikisha kupiga kura walipokuwa vyuoni lakini hawataweza kupiga kura kwa vile serikali imeamuru vyuo vyote vifunguliwe mara baada ya uchaguzi mkuu.

Hii ina maana kwamba zaidi ya wanafunzi 50,000 hawatapiga kura kwa vile watakuwa kwenye maeneo ambayo si vituo vyao vya kupigia kura.

Katika kufanikisha mkakati huu, serikali imeitumia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kusema kuwa bodi haina “fedha za kulipa wanafunzi mpaka uchaguzi utakapomalizika.”

Watu makini wanauliza je, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukopesha wanafunzi zimechukuliwa na serikali kwa ajili ya uchaguzi?

Au, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huu, wamekopa fedha za wanafunzi ili kufanikisha matakwa yao kisiasa? Je, hili linawezekana?

Hivi hizi fedha ambazo haziwezi kupatikana tarehe 25 Oktoba, zitatoka wapi kati ya tarehe 5 na 10 Novemba – muda ambao serikali inasema ndipo wanafunzi watatakiwa kurejea vyuoni?

Nani aliyebariki kitendo hiki cha kibabe na ambacho kimewafanya wanafunzi wa elimu ya juu nchini kukosa haki yao ya kikatiba ya kupigakura?

Jambo baya kuliko yote, ni pale bodi ya mikopo inapotoa vitisho kwa vyuo vikuu binafsi ambavyo vilitaka kufungua vyuo vyao kwa kufuata ratiba zake za kawaida.

Kiini cha yote haya ni utawala wa CCM kutafuta kila njia kupokonya haki ya wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na walimu wao.

Hata mwenyekiti wa taifa wa CCM, Jakaya Kikwete hajathubutu kwenda kuongea na wasomi wa taasisi hii. Ni kwa sababu, anatambua kuwa hakubaliki katika kundi la wasomi. Hana uwezo wa kutatua matatizo yao kwa sababu, haamini katika elimu.

Kwa sababu ya chuki dhidi ya wanamageuzi katika vyuo vikuu, serikali imesahau kwamba kuna baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu ambao ni wanachama wa CCM ambao nao wamepokonywa haki.

Serikali ya CCM haiamini kila mtu isipokuwa wateule wachache kutoka katika kundi la watoto wa vigogo. Ndiyo maana, kwa sasa, kuna mkakati kabambe wa kurithisha watoto wa vigogo nafasi za wazazi wao.

Wale ambao hawana nasaba ya wazazi katika chama, kila wanachosema hushushiwa shutuma, “Mmetumwa na CHADEMA; mmetumwa na upinzani?”

Viongozi wengi ndani ya CCM hawataki fikra mpya, bora zinazoweza kuleta maendeleo kwa taifa. Kimsingi hakuna kitendo cha kikatili na uvunjaji wa haki za kiraia kama hiki kilichofanywa na serikali – kuzuia haki za raia wake – wanafunzi wa elimu ya juu kupiga kura.

Lakini lazima ifahamike kwamba wanaotaka kurithisha madaraka watoto wao, watakabiliwa na wakati mgumu. Ni kwa sababu, wazazi waliokosa elimu moyoni mwao wana jambo – wameamka, wameamua kupeleka watoto wao shuleni na katika vyuo.

Serikali imejenga hofu na wasomi, inachukia upeo wao, kufaulu na kufika katika ngazi za juu kitaaluma. Kama hili ndilo kosa lao, basi serikali hii ni “genge” la watu waliojikusanya kukandamiza na kunyanyasa watu wake.

Katika mazingira haya serikali inapeleka vijana shuleni ili ionekane machoni mwa wengi kuwa inajali elimu, lakini ukweli ni kwamba haina dhamira njema na vijana.

Hii ndiyo maana hata shule ambazo wanazimwagia sifa wakidai wamevuka malengo ya milenia kwa uandikishaji kwa asilimia 95, hazifai kuitwa shule.

Haya ni makambi ya vijana kukulia. Huko inasomesha vijana isiowahitaji katika suala zima la kuamua kiongozi yupi anafaa kuongoza nchi.

Imefika mahali pabaya inaamua kusikiliza kauli za washirikina, kwamba rais alitupiwa jini na wapinzani wake kisiasa na wao watamlinda kwa maruhani; wakati wananchi wanalipa kodi kwa ajili ya ulinzi wa rais.

Serikali ya namna hii inalea ujinga. Pengine kazi kubwa inayopaswa kufanywa na wanafunzi wa elimu ya juu ambao wametapakaa nchi nzima ni kutoa elimu kwa wapiga kura wengine waiadhibu serikali.

Hapa kuna hoja kuu. Tume ya Uchaguzi inapaswa kuelekeza wanafunzi waliojiandikisha kupiga kura, kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waende kupigia wapi na wafuate utaratibu gani.

Ni kweli,wanafunzi watakuwa wameshindwa kumchangua yule waliyemlenga wakati wanajiandikisha; lakini angalau watatumia haki yao kumchagua waliyemwona na kumsikiliza kwa muda mfupi.

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu: Na. 0754 257 251/ 0714 801 893, au imeili: stanislaussenior@yahoo.com
0
No votes yet