Serikali yasalimu amri


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version

MUSWADA wa Sheria ya Mapitio ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, sasa utajadiliwa bila ya hati ya dharura, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za uhakika zilizofikia gazeti hili kutoka serikalini, zimesema serikali imekubaliana na hoja ya kutojadili muswada huo muhimu kwa hati ya dharura.

Tayari muswada umepokewa kwa malalamiko, shutuma, tuhuma na upinzani mkali kutoka kila upande wa nchi.

Muswada ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Jumatano iliyopita, chini ya hati ya dharura.

Hata hivyo, iliamuliwa baadaye kuwepo mijadala ya wazi ya wananchi ikiongozwa na kamati ya kudumu ya bunge ya Sheria, Katiba na Utawala.

Kabla na hata baada ya nakala ya muswada kuwa wazi, katika gazeti la serikali la 11 Machi mwaka huu, kumekuwa na upinzani mkubwa dhidi ya sheria ya kupitia/kurejea katiba badala ya kutunga sheria mpya.

Hata kabla serikali haijatangaza kupeleka muswada bungeni, chama cha wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) na asasi nyingine za kijamii, zilikuwa tayari zimeandaa kongamano la kuelekeza jinsi katiba mpya ya wananchi inavyopaswa kupatikana.

Katika kongamano hilo na jingine la Jumamosi ya tarehe 2 Aprili, wanataaluma na wanaharakati waliishauri serikali kutopora haki na mamlaka ya wananchi ya kutunga katiba ya kwanza ya wananchi tangu nchi ipate uhuru miaka 50 iliyopita.

Nje ya mijadala ya chuoni, vyama vya siasa, vikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadhi ya vyombo vya habari, vimeifafanulia serikali umuhimu wa katiba mpya ya wananchi.

Kilele cha upinzani kwa muswada wa serikali wa kupitia katiba, kilikuwa kwenye mijadala ya wazi Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar wiki iliyopita ambako wananchi wamekuwa wazi kwa serikali.

Asilimia kubwa ya walioongea wamesema muswada huo unalenga kunyamzisha wananchi, kuwapora haki ya kujadili mambo yanayowahusu na unalenga kuleta katiba inayolinda na kuendeleza maslahi ya watawala.

Hadi sasa vyama vikuu vya upinzani –  CHADEMA, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi vimeukataa muswada huo na kuishutumu serikali ya CCM kwa kuendesha mambo kidikteta.

Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary, alipokuwa akijadili muswada huo Ijumaa iliyopita mjini Zanzibar, alisema muswada huo “haufai.”

Alisema kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, jambo lolote linalogusa maslahi ya muungano linapaswa kufanywa kwa mashauriano ya pande mbili.

“Nasema serikali ya Zanzibar hatukushirikishwa. Muswada huu haufai. Uondoshwe kwenye meza ya Spika,” alisema na kuapa kuwa ataupinga na atashawishi wananchi wa Mgogoni waupinge.

Alipoulizwa msimamo wa serikali katika hili, alijibu kwa mkato, “Anayeweza kuzungumza hilo ni kiongozi wa serikali katika Baraza la Wawakilishi. “Mimi sina maoni. Hili ni jambo la kuzungumzwa na Kiongozi wa Serikali katika Baraza la Wawakilishi,” alisema.

Kiongozi wa Serikali katika Baraza ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idi ambaye jitihada za kumpata kwa simu hazikufanikiwa Jumatatu.

Balozi Seif ni mmoja wa viongozi waandamizi waliokuwa wakihudhuria vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma vilivyomalizika juzi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Masoud Othman amesema bunge la sasa la Muungano halina uwezo kisheria na kikatiba kutunga katiba, bali linaweza tu kurekebisha vifungu.

Amesema linalotakiwa kupitisha katiba ni Bunge Maalum lililoundwa rasmi kwa kazi hiyo.

Badala ya wachangiaji Zanzibar wametaka iitishwe kura ya maoni kuwauliza Wazanzibari kama wanataka Muungano.

Katika mazingira ambayo hayakutarajiwa, mwenyekiti wa jumuiya ya Maimamu zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed alichana muswada huo hadharani katika ukumbi wa shul;e ya sekondari ya haile Selassie.

Ahmed alisema wananchi wanakataa muswada huo na kwamba njia ya kuonyesha kuukataa kwa vitendo ni kama alivyofanya – kuuchana.

Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa sana, ni madaraka makubwa anayopewa rais juu ya uundaji wa tume, kuteua wajumbe wake pamoja na wajumbe wa sekretarieti.

Mengine ni rais kupokea ripoti ya tume, kuzuia wanasiasa kushiriki kufanya kampeni kabla ya kura ya maoni, kuzuia baadhi ya mambo kujadiliwa, na kutoa adhabu ya kifungo kwa wale watakaohoji utendaji wa Tume.

Wakitoka ukumbi wa mkutano mjini Zanzibar, wananchi walionyesha mabango. Baadhi yalisomeka: “Hatutaki Muungano jamani,” “Sanya na wabunge wenzako, rudini Zanzibar tudai talaka.”

Sanya (Ibrahim Mohammed) ni mbunge wa Mji Mkongwe, Zanzibar kupitia CUF.

Mtoa taarifa kwa gazeti hili amesema  ndani ya serikali kuna “muafaka fulani” kuwa muswada huo utarudishwa ili ufumuliwa na baadaye kujadiliwa kwa utaratibu ambao wananchi wanataka.

Kuondolewa kwa hati ya dharura katika kujadili na kupitisha muswada huo unaompa rais wa Jamhuri madaraka makubwa, ni moja ya madai ya wanasheria na asasi za kiraia.

Juzi, akitoa msimamo wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Rais wa chama hicho, Francis Stola, alisema ushauri wao kwa serikali ni kuondoa hati ya dharura inayoendana na muswada.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: