Serikali yasubiri kuanguka


editor's picture

Na editor - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

ALICHOKIFANYA Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe bungeni mnamo wiki iliyopita, juu ya tuhuma za rada zinazomkabili Andrew Chenge ni udhalilishaji dhidi ya serikali na wananchi.

Eti kuliambia bunge serikali haina ushahidi wa kuwapeleka mahakamani waliobainika kulainishwa kwa hongo ili kuidhinisha ununuzi wa rada hiyo, ni mbinu za kudanganya umma.

Hatupati picha kila tunavyopima kauli ya Chikawe, ambayo inaonyesha aliiandaa mapema. Tunachoamini tu, sasa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imechagua kulinda wahalifu.

Suala la “rushwa ya rada” limefanyiwa uchunguzi wa kutosha na makachero wa Shirika la Upelelezi wa Makosa Makubwa (ya jinai) la Uingereza (SFO) tangu mwaka 2007.

Matokeo ya uchunguzi yamekabidhiwa serikali. Ushahidi upo. Barua ya SFO yenye Kumb. Na. SPCO/D/MC ya 21 Machi 2008, ambayo ilitumwa kwa mwanasheria mkuu ndiyo ushahidi mwanana katika suala hilo.

Barua ya SFO imesheni maelezo kila mshiriki na jinsi alivyolipwa mlungula wake.

Miongoni mwao ni raia wa Tanzania walioidhinisha ununuaji wa rada kwa dola 40 milioni (Sh. 70 bilioni). Miongoni mwao ni Andrew Chenge, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati huo.

SFO wamesema Chenge alitoa sehemu ya fedha alizolipwa kupitia akaunti yake iliyoko kisiwani Jersey, Uingereza kwa Dk. Idris Rashid, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya taifa (BoT).

Lakini, pamoja na ugunduzi huo unaohusisha viongozi waandamizi wa serikali nchini, serikali haikuendesha uchunguzi wowote kuthibitisha yaliyofichuliwa na SFO.

Ndipo tunapojiuliza, “Hivi iwapo SFO walibaini malipo haramu yaliyohusisha viongozi wa juu katika serikali ya Tanzania, kwanini kusifanywe uchunguzi ili kuthibitisha.”

Jibu rahisi: Serikali ililenga tangu mwanzo kulinda wezi.

Kwa kuwa uongozi wa juu serikalini ulijua kilichotendeka, na haukuagiza uchunguzi ili kuthibitisha waliyothibitishwa na SFO, haina hata sababu moja kueleza wananchi haina ushahidi wa kushitaki wezi.

Haina ushahidi kwa sababu haikutaka. Imeamua kuficha ufisadi. Na hicho ndicho kinachoendelea sasa ndani ya serikali.

Ndio msingi wa kauli ya Chikawe, “Serikali haina ushahidi.”

Kwa mwendo huu, serikali inaashiria mchoko. Haiwezi tena kulinda raslimali za taifa na kutetea maslahi ya umma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: