Serikali yaua TTCL


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version
Kila kitu chakombwa na Celtel

MWEKEZAJI ambaye alipaswa kuimarisha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), sasa anaizamisha, MwanaHALISI limeelezwa.

Kampuni ya MSI/Detecon iliyokubaliwa na serikali kuwa mbia wa TTCL tangu kusainiwa kwa mkataba 21 Februari 2001, haijamaliza hata kulipa hisa zake.

Kwa mujibu wa mkataba, MSI/Detecon ilikuwa inachukua hisa 35 kwa gharama ya dola 120 milioni (sawa na Sh. 150 bilioni), lakini 'hadi inaondoka mwaka 2007, ililipa dola 60 milioni tu ambazo ni nusu ya gharama,' ameeleza mtoa taarifa ndani ya TTCL.

'Miaka saba tangu waingie TTCL, hawajalipa nusu ya pili, lakini wamechuma karibu shilingi 4 bilioni kila mwaka tangu 2001 hadi Septemba 2005,' ameeleza.

Kwa mujibu wa habari za ndani ya TTCL, hakuna ripoti za ukaguzi wa hesabu zilizothibitishwa na kutangazwa, wala taratibu za manunuzi kama zinavyotakiwa na Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004.

MSI/Detecon – ushirika wa kampuni ya Mobile Systems International ya Uholanzi na DETECON ya Ujerumani – imeshindwa au imekataa kulipia nusu ya hisa zake wakati ilipaswa kulipa fedha zote (dola 120 milioni) mara moja; na serikali imekaa kimya kuhusu hilo.

Kampuni hiyo iliahidi kuwaendeleza ajira ya wafanyakazi wote wa TTCL na kuongeza wengine; lakini kufikia sasa imewapunguza wapatao 1,800. Hili nalo serikali imelinyamazia.

MSI/Detecon iliahidi kuongeza njia 800,100 za simu. Haikufanya hivyo. Badala yake, chini ya uongozi wake, njia 160,000 zilizokuwepo, zimepungua hadi kuwa 100,000.

Kama kwamba hiyo haitoshi, MSI/Detecon badala ya kuendeleza kampuni ya simu za mkononi iliyokuwa imebuniwa na TTCL kwa jina la CELNET; ilitelekeza mradi huo na kuanzisha kampuni tanzu ya CELTEL.

Kinachosumbua akili za wengi katika TTCL kwa sasa ni vipi Celtel, iliyoanzishwa kama kampuni tanzu, ilichomolewa na kufanywa kampuni binafsi inayojitegemea, nje ya TTCL.

Juhudi zaidi za kuitenga Celtel na TTCL zilikamilika pale Celtel ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel International miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.

Kuja kwa MSI/Detecon, kukaidi kwa kampuni hiyo kutekeleza masharti na ahadi zake, kuanzishwa kwa Celtel ndani ya TTCL na baadaye kunyofolewa; kuanzishwa kwa Celtel International kumefanya TTCL 'ibaki kasha tupu.'

Leo hii, mitambo ya simu ya TTCL ndiyo inatumiwa na Celtel International kuunganisha nchi saba za Afrika Mashari na Kati.

Msemaji wa TTCL hakuweza kupatikana kutoa maelezo kamili juzi Jumatatu wakati gazeti likienda mitamboni kutokana na kuwa sikukuu. Juhudi za kupata hata simu ya mkononi ya Mkurugenzi hazikufanikiwa.

Leo hii, kwa mujibu wa kutoka ndani za TTCL, Celtel International, ambayo sasa iko chini ya MSI, inahodhi njia ya setilaiti kwa ajili ya kurushia mawimbi ya sauti kutoka Dar es Salaam hadi Ngara.

Kutoka Ngara, Celtel imejenga mtandao wa waya hadi Uganda na kutoka hapo, imejenga mtandao wa njia za usambazaji (multiplex) kwenda Kenya na nchi nyingine za Magharibi mwa Afrika. Tanzania ndio chimbuko.

Ndani ya Tanzania, Celtel, inatumia mitambo ya TTCL ya Voice Satellite (VSAT) iliyoko Kigoma, Bukoba na Mtwara kuendeshea mtandao wake.

'Kinachosikitisha katika biashara hii ni kwamba TTCL inaendelea kugharimia mitambo hiyo na Celtel inaendelea kuitumia bila ya malipo yoyote,' kimeeleza chanzo cha habari hizi.

Kwa mfano, TTCL ililipa, angalau hadi Machi 2006, dola 100,000 kugharimia mitambo hiyo ambayo Celtel inatumia bure.

Imefahamika kuwa wafanyakazi wa TTCL ndio wanaohudumia mitambo ya kampuni hiyo ambayo inatumiwa na Celtel International. Mishahara yao inatoka TTCL.

Mkataba wa MSI/Detecon na serikali umezaa madhara makubwa kwa TTCL ingawa serikali imekaa kimya.

Chuo cha Posta ambacho kilikuwa kinahudumia nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, kimedhoofika na kufutika kitaaluma; na mitambo yake kuhamishiwa mikoani kuhimili mtandao wa Celtel.

Mitambo ya aina ya GS 5000 kutoka Canada, Niax kutoka Japan, DTS A1100 kutoka Korea na Sys 12 kutoka Ubelgiji, yote ya TTCL, imehamishiwa Manyoni, Tabora na Rufiji.

Kuna taarifa kwamba ni mitambo hiyo ya TTCL iliyochukuliwa Dar es Salaam ambayo uongozi wa Celtel unadai uliinunua kwa Sh. 2.1 bilioni.

Pia imefahamika kuwa baada ya Celtel kujichomoa TTCL, iliondoka na wateja wakubwa kwa mtindo wa 'lipa baada ya kutumia' ambao ulichukua wengi.

Walipokuwa wanajiandaa kumaliza kazi, MSI/Detecon walipendekeza kampuni ya SASKATEL ya Canada kuendesha TTCL.

Cha kushangaza ni kwamba SASKATEL, iliyokuwa muuza vifaa kwa MSI/Detecon, ndiyo ilipendekezwa na kukubaliwa na serikali bila ya hata kufuata mtiririko kama unavyoainishwa na sheria ya manunuzi ya mwaka 2004 ukielekeza kuitishwa zabuni.

Saskatel ilikuwa katika kundi la makampuni matatu yaliyoshindania zabuni ya TTCL mwaka 2001.

TTCL ya sasa imebakia mifupa, anasema mmoja wa wafanyakazi kwa sauti ya huzuni. 'Wafanyakazi wamegawanyika – upande mmoja ni wanaopenda menejimenti na upande mwingine ni wanaopigania haki yao na maslahi ya umma,' anasema.

Haina tena kiwanda; mitambo yake imenyofolewa; ufundi na mafundi waliowika kusini mwa Afrika wametawanyika na taifa kwa ujumla limepoteza utaalam.

'Ufundi wa kompyuta, kwa mfano, na ule wa Switchboard taaluma zilizokuwa zinafundishwa chuoni pale, vimetoweka na kampuni imebaki muflis,' ameeleza.

Msiba mkubwa kwa TTCL ni mali zake zisizohamishika: ardhi na majengo. MSI/Detecon ilichukua nyumba na viwanja vyote vya kampuni.

Mtandao wa TTCL ulikuwa katika kila wilaya. sasa ulipofika, palikuwa na viwanja, nyumba na mitambo yake. Vyote vimechukuliwa au vinadhibitiwa na Celtel.

Wakati hayo yote bado yanaendelezwa na Saskatel, mrithi wa MSI/Detecon aliyeingia kwa mlango wa uwani, serikali inaendeleza kimya chake.

0
No votes yet