Sh. 300 bilioni kufukia migodi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

SERIKALI huenda ikatumia Sh. 330 bilioni za walipakodi kufukia mashimo na kukarabati mazingira ya migodi baada ya madini kumalizika.

Habari zilizoifikia MwanaHALISI zimeeleza kuwa hadi sasa hakuna kampuni hata moja ya uchimbaji madini nchini iliyoweka dhamana ya fedha kwa ajili ya kukarabati mazingira hayo.

Dhamana hiyo inawekwa ili kuhakikisha kuwa endapo kampuni husika ya uchimbaji madini itashindwa kukarabati mazingira baada ya mgodi kufungwa, fedha hizo zitumike kufanya kazi hiyo badala ya kuchota fedha za walipa kodi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini (TMAA), Paul Masanja amethibitisha kuwa migodi yote mikubwa haijaweka dhamana ya ukarabati wa mazingira hadi sasa.

“Migodi yote inatakiwa kuweka dhamana ya jumla ya dola za Marekani 210 milioni, na hii ipo katika taarifa zao; lakini hawajaweka fedha hizo,” amesema alipozungumza na MwanaHALISI kwa simu mwishoni mwa wiki.

Amesema katika ukaguzi wake, wakala umebaini kuwa wawekezaji katika sekta ya uchimbaji madini hawatekelezi mpango huo, jambo ambalo ni ukiukaji wa masharti ya leseni.

Alipoulizwa wamefanya nini kurekebisha hali hiyo, alisema TMAA inaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya serikali hususan Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuhakikisha kasoro walizobaini zinarekebishwa.

Miongoni mwa mambo aliyosema wamefanya, ni serikali kuteua kamati ya watu saba ya ushauri wa madini, inayoongozwa na Richard Kasesera, ambayo itapitia mikataba na kushauri jinsi gani na benki ipi itumike kwa kampuni hizo kuweka dhamana hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Masanja kwa serikali, nchi nyingi duniani zinakabiliwa na changamoto ya kuwapo kwa migodi iliyofungwa na, au kutelekezwa na wamiliki wake bila ya mazingira ya maeneo ya uchimbaji kurekebishwa.

TMAA iliyoundwa 2 Novemba 2009 ndiyo imefanya utafiti wa kubaini aina na viwango vya dhamana ya ukarabati wa mazingira, vinavyotumika duniani ili kuishauri serikali ni aina ipi ya dhamana inayofaa kuwekwa na njia ipi itumike kukadiria kiwango chake.

“Utafiti huu ni muhimu kwani ulilenga kuhakikisha kwamba jukumu la ukarabati wa mazingira ya migodi linabakia kuwa la wamiliki wa migodi na sio la serikali,” amesema Masanja katika taarifa hiyo.

Masanja amesema matokeo ya utafiti huo yamesaidia kurekebishwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo imeweka sharti la uwekaji hati fungani za ukarabati wa mazingira kutoka kwa waendeshaji wa migodi.

Katika hatua nyingine, ukaguzi wa TMAA katika mapato, gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi umebaini kuwa serikali imekuwa ikipoteza mabilioni ya shilingi kwa muda mrefu, kutokana na udanganyifu wa kampuni za uchimbaji.

Ripoti ya TMAA imeeleza mbinu ambazo zimekuwa zikitumika katika udanganyifu huo kuwa ni kuwapo kwa gharama kubwa za uwekezaji na uendeshaji ambazo hazina vielelezo.

Pia, ilibaini kujumuishwa kwa gharama za uendeshaji zisizostahili katika ukokotoaji wa kodi ya mapato, na utoaji wa taarifa zisizokuwa sahihi za mauzo ya madini.

Vilevile wawekezaji katika madini wamekuwa wakidai unafuu wa kodi katika gharama za uwekezaji kwa viwango visivyostahili, na kuwa wawekezaji hao wamekuwa wakichukua mikopo kwa kampuni zenye uhusiano nao, na kutoza riba bila idhini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“…Tumebaini pia kuwapo kwa mitaji midogo ya uwekezaji ukilinganisha na mikopo…pia, kumebainika malipo pungufu ya mrabaha utokanao na mauzo ya madini,” amesema Masanja katika taarifa hiyo.

Udanganyifu mwingine uliobainika ni kuwapo kwa tofauti kubwa ya upembuzi yakinifu na matokeo halisi ya shughuli za migodi.

Vilevile gharama za utafutaji madini nje ya eneo la leseni zimekuwa zinajumuishwa kwenye gharama za uendeshaji wa mgodi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, hasara itokanayo na biashara ya dhahabu imekuwa inajumuishwa katika ukokotoaji wa kodi ya mapato na kuikosesha serikali mabilioni ya shilingi.

Gazeti hili, mwaka juzi lilifanya uchunguzi katika migodi mikubwa nchini na kubaini adha za wananchi wanaofukuzwa ili kuanzisha migodi, wafanyakazi kutokuwa na ajira za uhakika na wakazi kuathirika vibaya kutokana na mazingira ya migodini.

Aidha, uchunguzi ulibaini pia jinsi serikali isivyopata mapato halali kutokana na utajiri wa raslimali zake na jinsi kampuni za madini yanavyojilimbikizia utajiri yakiacha serikai utupu.

Ukaguzi wa TMAA ulioshirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), umeongeza kasi ya ulipaji kodi ya mapato kwa migodi ya dhahabu ya Geita (GGM) unaomilikiwa na AngloGold Ashanti na Golden Pride wa Resolute (T) Limited.

Kwa mujibu wa ripoti ya Masanja, Golden Pride umelipa kodi ya mapato Sh. 62.6 bilioni kuanzia mwaka 2009 hadi 2011; wakati GGM imelipa Sh. 12.7 bilioni katika kipindi hichohicho. GGM inatarajia kulipa dola za Marekani 50 milioni mwaka huu.

Migodi inayomilikiwa na African Barrick Gold (ABG) ililipa dola 2 milioni kama tozo ya mafuta ambayo ilikuwa haijalipa hadi mwaka 2010, na Pangea imekubali kulipa dola 32 milioni kama kodi ya mapato kwa mgodi wa Tulawaka kwa mwaka 2008.

Malipo hayo yanafanyika baada ya kuondolewa kwa gharama za uwekezaji za mgodi wa Buzwagi ulioanza kuzalisha mwaka 2009.

0
No votes yet