Shamhuna, Khatib wako nchani kwisha


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

"CCM haihitaji kushirikiana na chama chochote ili kuunganisha Wazanzibari kwani ndio chama pekee kinachoweza kuunganisha Wazanzibari," anasema Muhammed Seif Khatib.

Kwa kauli hii, waziri huyu chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), anataka kuonyesha ulimwengu kuwa CCM ni kila kitu. Ni chama dola kinachojitosheleza.

Ajue anazungumzia chama ambacho kimeshindwa kazi. Hiki chama makundi sasa. CCM si tena kile alichokiasisi Mwalimu Nyerere na wazee Rashid Kawawa na Aboud Jumbe. Kimebadilika kila kitu.

Kimegawa nchi na wananchi. Kimetupa asili yake ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi. Sasa ni chama cha kulea ufisadi. Wakuu wake hawaelewani. Mivutano ndio funzo.

Matokeo ya kuparaganyika yanaonekana: Wanachama haweshi kugombana wakiwa ndani na nje ya vikao; viongozi haweshi kulaumiana na kutunishiana misuli.

Kutofautiana misimamo hata kwa masuala ya maslahi ya taifa na Watanzania ni jambo la kawaida; kila kiongozi ana kundi la viongozi wanaoridhia anayoyaridhia yeye.

Matatizo yamehamia kwa umma na dola. Matumizi mabaya ya fedha na mali ya umma yameshamiri serikalini; wahujumu wanatetewa na kulindwa; viongozi wake wanadharau na kukejeli wananchi hadharani; mipango ya serikali inazorota na siri zake zinavuja ovyo.

Unapokuwa na chama kiongozi ki dhaifu hivi, hutegemei uongozi uliotukuka; ule unaozingatia misingi ya utawala bora; utawala wa sheria; hekima na busara. Ukosefu wa nyenzo hizi unakuza umasikini – kuzidisha pengo la matajiri wachache na mafukara wengi, na demokrasia ni ndoto.

Viongozi hawajali wananchi. Mara nyingi hawategemei kuchaguliwa. Kwa kujua hawakuchaguliwa kihalali, wanajenga kiburi. Ndio tunasikia baadhi wakitamkia wananchi, “Nimetumia fedha zangu kuchaguliwa hamnibabaishi kitu.”

Siku hizi kuchaguliwa kunategemea unazo ngapi? Hapana. Umegawa ngapi. Shauri ya umasikini kuzama katika jamii, hata wapigakura wamejisahau. Wanahongeka kiulaini.

Wanahongwa wao na waomba uongozi wanahonga wanaoteua majina ili mtu ugombee kupitia CCM.

Ndio kusema Tanzania sasa uchaguzi unavurugwa mchana kweupe. Tunapohoji tunaitwa wambeya. Na afadhali kuitwa hivo. Waweza kuitwa muongo. Tunasema uheke.

Tumeyaona haya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika 25 Oktoba Tanzania Bara. Vurugu tupu na hila.

Ipo mitaa hadi muda huu haijatangaziwa matokeo rasmi ya uchaguzi. Maeneo mengine mtaa mmoja una matokeo mawili. Yaliyobandikwa usiku ule na mengine yaliyobandikwa mchana wa 26 Oktoba.

Mfano mzuri ni Chamanzi, Wilaya ya Temeke na Msewe wilayani Kinondoni, Dar es Salaam. Hadi hivi unavyosoma hapa, msimamizi wa Chamanzi hajajulisha wagombea matokeo rasmi.

Nako Msewe, jimboni Ubungo, idadi ya kura za mwenyekiti aliyetangazwa mshindi, ni zaidi ya zile zilizopigwa. Mote humo waliopewa ushindi wanaogopa kufika ofisini kufanya kazi.

Zanzibar halkadhalika. Uvurugaji uchaguzi imekuwa ada kiasi kwamba wakubwa wanaamini ni haki ya kikatiba. Hutumia hata walinzi wa amani. Mwaka 2005 zilienea ripoti kuwa walipelekwa JKT kudhibiti kelele baada ya kura kuibwa.

Watu wananyimwa haki ya kupiga kura. Kwa hivyo, ni sahihi kusema viongozi wengi waliopo hawakuchaguliwa kihalali. Wapo wabunge, wawakilishi na madiwani walijichagua.

Si kutwa hata waziri Khatib na Ali Juma Shamhuna hawakuchaguliwa kutokana na uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi. Majimboni kwao, kulikuwa na wapigakura mamluki.

Donge palikuwa na kambi ya Janjaweed eneo la Pangatupu. Hawa ni vijana masikini waliotumika kusaidia mikakati ya ushindi ya CCM Unguja na Pemba. Vijana hawa walipelekwa kila jimbo lililohitaji nguvu ili kuiba kura au kumpatia mgombea urais kura za hila.

Hakuna chama kilichoingia Donge kufanya kampeni. Ni CCM pekee. Nilikuwa safarini kwenda Donge kwa mkutano wa kampeni ya mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, nikaishia Mahonda.

Pale nilikuta mabomu ya machozi na bakora za polisi vikimiminiwa raia waliosimamishwa wasiendelee kwenda Donge. Nilipouliza Polisi, wakajibu, “Tumeona hali ya usalama hairuhusu. Tumefuta mkutano wa kampeni.”

Alas, hali ya usalama ipi wakati tuna Polisi wa kutosha kulinda mkutano? Wapi imeelezwa Polisi wanaweza kufuta mkutano wa kampeni? Polisi hawakuwa na amri ya Tume ya Uchaguzi inayoratibu mikutano ya kampeni.

Wenyewe CUF wanasema hawahitaji ulinzi maana vijana wa Blue Guard wanatosha. Wanalinda viongozi wao, wanalinda wanachama wenzao. Mhuni gani atapenya hapo?

“Usalama mdogo” ndio kaulimbiu ya tawala za kidikteta. Hizi ni tawala zinazokandamiza harakati za wananchi za kujenga demokrasia. Hawapendi kusikia wananchi wanadai haki zao.

Walitamba kupata ushindi mkubwa. Waziri Khatib alitamba bungeni eti alipata asilimia 97 ya kura.

Khatib ambaye ni waziri mzoefu zaidi katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete, anaamini serikali ya ushirikiano haihitajiki Zanzibar. Shamhuna naye haiafiki.

“Watu wengi wanafikiri serikali hiyo ndio suluhisho la matatizo ya kisiasa Zanzibar. Hata ikiundwa matatizo hayataondoka maana masuala yaliopo yanatokana na baadhi yetu kuweka mbele umimi badala ya utaifa.

Anasema “Kadiri umimi utakavyokuwepo miongoni mwetu wanasiasa, tatizo ndio litaendelea. Kwa hivyo kuundwa au kutoundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa hakutasaidia.”

Pia anahimiza wanasiasa kujenga “utamaduni wa kukubali kushinda na kushindwa yanapokuja matokeo ya uchaguzi.” Anamhimiza nani hasa? Chama cha CCM au CUF?

Anaongeza, “Lakini watu wanasahau Zanzibar ni nchi ya kimapinduzi. Wanadhani ni nchi ya watu kupiga kura na kutangazwa tu huku wengine wakifikiri Zanzibar ni nchi yenye watu walegevu.”

Mwanasiasa mmoja anamtaja Shamhuna kuwa ndiye muumini mkubwa wa umimi. Ni mbinafsi anayependa kudandia fursa za kisiasa. Ni kigeugeu.

Hata mimi najua aliwahi kuisema vibaya serikali ya Rais Amani Karume alipokosa kuteuliwa waziri. Akaongoza kundi lililoitwa Pentagon barazani akiwa na akina Hafidh Ali Tahir (Dimani) na Machano Othman Said (Mwembemakumbi).

Tuliokuwa tukisaidia kazi za gazeti kipenzi cha Wazanzibari, Dira, lililodumu kwa mwaka mmoja tu, tulihariri makala zake alizoandika kwa jina la Haji Nahoda.

Alipoteuliwa tu waziri mwaka 2003, aligeuka na kuwa mtetezi wake mkubwa hata kuhitilafiana na ndugu zake Donge wakiwemo viongozi waandamizi katika chama na serikali.

Alikuwa Shamhuna huyohuyo aliyekuja kuapa ndani ya Baraza, baada ya Dira kufungiwa, kwamba, “Siyo tu limefungiwa, kwa hakika ndio limekufa kabisa.”

Jeuri na makeke yake yalimgharimu akakosa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM) uchaguzi wa 2007. Vijana wadogo waliopata baraka ya wazee walifanikiwa kumwangusha na kuzima ukinara wake.

Shamhuna na Khatib Wanaamini mabadiliko ni dhambi. Wanaona CCM tu ndio halali kuongoza serikali, licha ya kujua siasa za ushindani zimeruhusiwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na mazonge ya CCM, nahisi siku zao ziko nchani sana kisiasa. Kama anavyonaswa ndege mjanja kwenye tundu bovu, ndivyo Shamhuna na Khatib watanasa kwenye urimbo. Makeke yao yatakwisha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: