Shamhuna mahiri Donge, si jasiri


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MWANASIASA mkongwe nchini, Ali Juma Shamhuna, amewahi kusema kuwa kwa uoni wake, demokrasia anayoiamini ni ile ambayo wananchi wenyewe wanairidhia. Wakisema tunataka hivi au tumeamua hivi, watiiwe.

Shamhuna, naibu waziri kiongozi na waziri wa habari, katika serikali inayomaliza muda wake, alitoa kauli hiyo wakati alipochukua fomu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuomba ateuliwe kugombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa 31 Oktoba.

Aliitisha mkutano wa waandishi wa habari baada ya hatua hiyo na alipomaliza kueleza sababu za kutaka urais aliruhusu kuulizwa maswali.

Swali langu kwake nilimuuliza anaielewaje dhana ya demokrasia iwapo amekuwa akichaguliwa mwakilishi katika uchaguzi ambao vyama vingine havipewi nafasi ya kufanya kampeni jimboni kwake Donge?

Donge ni moja ya majimbo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja linalojulikana kama ngome kuu ya CCM kwa mkoa huo. Hapo, imekuwa vigumu kwa vyama vya upinzani kuruhusiwa na serikali kufika kwa ajili ya kutafuta kura za wananchi.

Kwa mfano, chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Wananchi (CUF) chenye nguvu kubwa Zanzibar, kilipoteza dhamana wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya mgombea wake kushindwa kupata angalau asilimia 10 ya kura zote jimboni.

Mgombea wa CUF alipata chini ya asilimia 10 ya kura zilizopigwa, matokeo yake akapoteza haki ya kurudishiwa fedha alizoweka dhamana wakati wa kuomba ridhaa ya wananchi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar .

Kitu kibaya kinachofanyika siku zote ni dola kusuka mikakati ya kuhakikisha CUF haifanyi kampeni zake Donge. Ina maana CUF inazuiwa kushawishi wapiga kura wa Donge kuwachagua wagombea wake.

Hata wakati kukiwa hakuna uchaguzi inakuwa shida na iwapo chama kingine kitaruhusiwa kwenda, basi hulazimishwa kufanya mkutano viwanja vya sehemu zisizo na watu wengi.

Mwaka 2005 kabla ya uchaguzi, CUF iliruhusiwa kufika Donge lakini ilijikuta ikihutubia wanachama wake tu waliotoka mjini tena katika uwanja uliokuwa katikati ya mashamba ya mikarafuu na minazi; mbali na walipo wananchi.

Wakati wa uchaguzi mwaka huo, CUF ililazimishwa kufanya mkutano katika uwanja ulioko kiasi cha kilomita tatu kutoka pale ilipojiandaa kufanya mkutano wake wa kampeni.

Lakini hata hapo, hatimaye haikufanikiwa kufika. Msafara wa magari ya wanachama na viongozi wake ulishambuliwa kwa milipuko ya risasi za mipira na za moto mita chache na kilipo kituo cha polisi cha Mahonda.

Mkutano ukashindikana kufanyika na hiyo ikawa maana yake CUF ilishiriki uchaguzi jimbo la Donge pasina kufanya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo .

Hali hiyo inatokea ilhali vyama vimeundwa kwa mujibu wa sheria ya bunge ya mwaka 1992, ambayo pia inafanya kazi Zanzibar kwa sababu siasa ni suala la kimuungano.

Chama cha siasa hupata wafuasi kwa njia nyingi. Mojawapo ni kufanya mikutano ya hadhara kule waliko wananchi ambapo hueleza dhamira yake na nini kitafanya iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza serikali.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi ni wakati muafaka kutekeleza hatua hiyo ya haki kikatiba. Vyama vinapata nafasi ya kujieleza mbele ya umma ili kushawishi kuaminika na kutaraji kuungwa mkono.

Mikutano ya hadhara ndio njia iliyozoeleka zaidi ya kutafuta wanachama. Tukumbuke vyama vilisajiliwa kwa mujibu wa sheria baada ya kila kimoja kupata idadi inayotakiwa ya wanachama wakati wa kuomba hati ya usajili wa kudumu.

CUF ilifanya hivyo kama ilivyofanya CCM. Kulingana na kumbukumbu zilizoko kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania , CCM ndio chama kilichosajiliwa cha kwanza na kufuatiwa na CUF.

Kwa mara nyingine, serikali imeshindwa kuheshimu wajibu wake wa kusimamia kampeni za uchaguzi kwa kutoa haki kwa kila chama na mgombea kufanya kampeni pale anapohitaji.

Imeshindwa kuhakikishia CUF na mgombea wake wa urais wanafanya mkutano wa kampeni Donge kwa sababu hawakuruhusiwa kukutana kwenye uwanja wa mpira wa skuli ya Donge waliopanga kukampeni.

Kilichotokea ni mbinu zilizoratibiwa na mkuu wa mkoa, Pembe Juma Khamis na serikali ya wilaya ya Kaskazini B chini ya Vuai Ali Vuai ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar za kutengeneza mazingira ya makusudi kuhakikisha Maalim Seif hafanyi kampeni yake Donge.

Viongozi wa CUF wilaya ya Kaskazini B na wale wa jimbo la Donge walishafanya mazungumzo na uongozi wa skuli ya Donge na ruhusa ya uwanja ilitolewa.

Lakini, tayari mbinu za CCM kwa kuwatumia makada wake katika serikali, mkoani na wilayani, zilikuwa zimeanzishwa kwani ilitoka kauli eti siku ambayo CUF inataka mkutano Donge, kungekuwa na wanafunzi wanaofanya mapitio kujiandaa na mitihani. Mkutano wa CUF ulipangwa Jumamosi 16 Oktoba siku ambayo mitihani ya kidato cha nne ilishakamilika.

Baada ya vitisho, mwalimu mkuu alilazimika kumwandikia Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Zanzibar kumwarifu kuwa haruhusu uwanja wa skuli kufanywa mkutano wa kampeni ya kisiasa.

Ni barua hiyo ya 10 Oktoba iliyotumiwa na Mkuu wa Mkoa kumwandikia mkurugenzi huyohuyo kumjulisha suala hilohilo. Huyu aliandika barua yake 12 Oktoba – siku ambayo anaeleza kuwa aliitisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ambayo yeye ndiye mwenyekiti – akimjulisha kutoruhusiwa uwanja wa skuli kutumika na akapendekeza badala yake utumike uwanja wa Mwanakombo.

Uwanja wa Mwanakombo uko pembeni mwa jimbo la Donge, yapata kilomita tatu kuifikia skuli ambako ni katikati ya jimbo na eneo lililo karibu kwa maeneo yote ya jimbo.

Tarehe 15, siku moja kabla ya mkutano, Meneja wa mgombea alipokea barua ya mkurugenzi wa uchaguzi Zanzibar iliyoandikwa 14 Oktoba kumjulisha kuwa serikali ya mkoa imekataa CUF kutumia uwanja wa skuli kufanyia kampeni yake.

Sasa Donge limekuwa ni jimbo ambalo vyama vya upinzani vinanyimwa nafasi ya kueleza sera zake na mazingira yanaonyesha namna viongozi wa serikali na CCM wanavyofanya ushawishi kudumisha utamaduni huo wa kihafidhina.

Wananchi wana haki ya kupata taarifa za vyama mbalimbali ili wenyewe waamue wanataka chama au mgombea yupi. Kufanya mikutano ni haki ya chama wakati wowote muradi taratibu za kisheria zimefuatwa.

Donge ni sehemu ya Zanzibar ambako wananchi wake wana haki hiyo vilevile kikatiba. Kama CCM inaruhusiwa kufanya kampeni katika majimbo ambayo wakati wa uchaguzi inaambulia kura 300 tu kwanini isiwe hivyo kwa CUF ambacho kinakubalika Donge ndio maana kinaongeza idadi ya kura mwaka hadi mwaka?

Shamhuna na wenzake katika CCM wanaweza kuwa mahiri kisiasa bali wanazidi kuthibitisha wasivyo jasiri kukabiliana na ushindani ndani ya mfumo wa vyama vingi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: