Shamhuna, mvunaji wa alichokipanda


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SUALA la eneo la bahari kuu la maji ya Zanzibar kujumuishwa katika ombi la Tanzania la kutaka nyongeza ya eneo tengefu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, limeacha kitendawili.

Baada ya mjadala mkali ndani ya Baraza la Wawakilishi kwa kubainika kuwa ombi hilo limepelekwa Umoja wa Mataifa bila ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikishwa, sasa SMZ yenyewe ipo shakani.

Inatakiwa msimamo. Wazanzibari wanasubiri serikali inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ieleze ukweli.

Umma unataka kujua ni kweli serikali haikujua; au ni kizungumkuti tu kinachofumbwa kwa wenye nchi – Wazanzibari waliotoa ridhaa ya serikali iliyopo madarakani.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyorekebishwa mara ya mwisho mwaka 2010, inataja wananchi kuwa ndio wenye mamlaka ya utawala wa nchi, ila wameipa dhamana serikali kuwaongoza.

Ibara ya 9 ya katiba, toleo la 2010, kifungu Na. 2(a), inaeleza: mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wa Serikali kufuatana na Katiba, utatoka kwa wananchi wenyewe.

Kwa tafsiri ya kawaida, maana yake ni kwamba hakuna kitakachofanywa na serikali, chochote kiwacho, bila ya wananchi kujua. Wao ndio wenye mamlaka yote kuhusu nchi yao.

Maelezo yaliyopo Baraza la Wawakilishi, chombo chao mahsusi cha kutunga sheria na kuwakilisha katika kuisimia serikali kiutendaji, ni kuwa serikali haikushirikishwa.

Serikali yenyewe, kupitia kiongozi wake katika Baraza, haikusema moja kwa moja haikushirikishwa. Maelezo yaliyobaki ni yale ya Ali Juma Shamhuna, waziri anayehusika na ardhi na maji.

Kiongozi wa shughuli za serikali barazani, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, hakutoa kauli ya kuthibitisha au kukana ushiriki wa serikali katika suala hilo.

Alichokisema ni kutaka serikali ipewe nafasi ya kujadili suala hilo kwenye Baraza la Mapinduzi (BLM), na baadaye kuja barazani kueleza msimamo wao.

Hapa ndipo nisemapo suala hili ni kitendawili. Kumbe itachukua muda mpaka wananchi watakapoelezwa “ukweli” ulivyo.

Nimeliwekea alama maalum neno ukweli, kwa sababu akilini mwangu naona kama serikali inalijua jambo hili.

Ndio kitendawili ninachosema. Zipo fununu serikali inajua, lakini pengine uongozi wa juu wa SUK, kupitia Balozi Iddi, umeona haukuwajibika sawasawa.

Kuna wakati unaweza kufanya kosa usijue haraka. Inapotokea kujua umekosea, unatafuta pa kujificha. Sisemi SUK inataka kuficha ukweli, maana najua hilo ni jambo la hatari zaidi – ni kujikaanga.

Hali hii ndiyo hasa inayonipeleka kuhofia kama SUK itathubutu kumkana Waziri Shamhuna, ambaye yumo katika shinikizo za kumtaka ajiuzulu kwa kuipeleka puta serikali au kwa karibu zaidi, kuwaingiza wananchi katika ubia usiowapendeza.

Ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zipo taarifa za maofisa waandamizi wa wizara anayoiongoza Shamhuna kushiriki vikao vingi vya mashauriano na wizara ya ardhi ya muungano kuhusu jambo hilo.

Katika hali ya kawaida, tuamini kwamba yote hayo yaweza kufanyika bila ya Shamhuna kuiarifu serikali?

Shamhuna nimjuae nahofia kama anaweza kufanya hivyo. Kiutendaji huyu ana akili; hataki kufanya makosa yakamsulubu. Anajipenda kiuongozi; lakini pia anajua ni muhimu sana kulinda hadhi yake kwa umma.

Pale alipobaini kuna makada wenzake CCM wanamchimba na wamejipanga kumuengua katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Shamhuna alipanga mkakati wa kujinusuru.

Ni bahati nzuri tu kwa wapinzani wake, mbaya kwake, walifanikiwa. Walimtupa nje na mpaka leo ni miongoni mwa viongozi wa juu serikalini wasiokuwa wajumbe wa NEC.

Sasa Shamhuna anakuwa macho asianguke kijinga. Anajua ikifika kuhojiwa, aweza kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Zamani makada wa CCM waliomo serikalini, hawakuogopa sana kuhilikishwa na uongozi wa juu wa serikali. Zaidi walihofia mkong’oto wa chama. Hali sasa ni tofauti.

Siku hizi SMZ imejengeka kivingine. Kuendeshwa kwake kwa mfumo wa ushirikiano na Chama cha Wananchi (CUF), kumeifanya iwe ya kuogopwa na kila kiongozi, wakiwemo makada wenye jeuri kama Shamhuna.

Shamhuna, kama alivyo mtu yeyote mzima, anaogopa pia, licha ya kuwa mkakamavu na jeuri. Anajua akilikoroga peke yake, pia atalinywa peke yake.

Ipo namna nyingine ya kumtathmini au kumjua Shamhuna. Ni mbabe. Huutumia ubabe baadhi ya wakati hasa anapoona maslahi yake yanahatarishwa.

Alitumia ubabe alipohangaika kujinusuru na anguko la kihistoria wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM 2007 makada wenzake Mkoa wa Kaskazini walipojipanga kutaka kumuangusha asiwe MNEC pamoja na kuwa naibu waziri kiongozi.

Alitumia hata raslimali za serikali kupanga mkakati wa kuwashinda wabaya wake hao. Aliita watu kutoka vijijini waende ofisini kwake Migombani.

Aliwatisha pale ambapo sasa ndio ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Kitu ambacho labda hakukijua ni kwamba wote aliowaita na kuwatisha, alipowaachia tu, walikimbilia kwa “kundi” lao kupiga ripoti.

Kila alichokipanga na kukitekeleza wakati ule, kilijulikana na wapinzani wake. Kwa hali hii, ni rahisi kusema Shamhuna alishindwa kuingia NEC kwa sababu mbinu zake zilihujumiwa haraka kimkakati.

Huyu ndiye Shamhuna nimjuae. Ndiye aliyetoa kauli “mbaya sana” kwa dhana ya utawala bora, utiifu kwa sheria na haki za binadamu, pale alipoliambia Baraza la Wawakilishi mwaka 2003:

“Tena gazeti hili (la Dira) siyo tu limekufa, kwa hakika ndio limezikwa hasa.”

Alitoa kauli hii ilhali akijua fika kwamba mezani kwake (akiwa Waziri wa Habari) kuna maombi ya usajili wa gazeti la Dira, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ambayo serikali ilishitakiwa.

Kampuni ya ZIMCO (Zanzibar International Media Co.) iliyokuwa mmiliki wa gazeti hilo lililokuwa likichapishwa kila Ijumaa, ilifungua kesi kutaka amri ya kutengua uamuzi wa Waziri wa Habari, kufungia Dira.

Jaji Mshibe Ali Bakari aliyesikiliza kesi hiyo ya mwaka 2003, aliamua kwamba ZIMCO waombe usajili upya wa gazeti hilo iwapo wataona inafaa au kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake wa kuthibitisha ubatili wa usajili na kusafisha ZIMCO kuwa siyo iliyokosea.

Jaji Mshibe alibaini serikali yenyewe ndiyo iliyokosea kuwajibika kisheria kuhusu Bodi ya Usajili wa magazeti.

ZIMCO wakawasilisha tena maombi ya usajili mpya kwa Msajili wa magazeti Zanzibar, ambaye yupo chini ya Wizara ya Habari. Wakati hatua hiyo ikitekelezwa kwa mujibu wa maelekezo ya Mahakama, Shamhuna akachafua barazani.

Tamko lake lilikuwa na maana mbili kubwa: Kwanza, serikali (labda yeye binafsi kwa chuki tu) kudharau mahakama. Pili, kuonyesha serikali isivyofuata sheria na katiba.

Chanzo cha hayo ni Ali Juma Shamhuna, yule niliyemtaja hapo kabla kuwa miongoni mwa sifa zake, ni ujeuri na ubabe.

Kiongozi mwenye sifa hizi, miongoni mwa nyingine ikiwemo ya weledi na umakini, hawezi kufanya kosa kipuuzi. Shamhuna amefanya kosa zito akijaribu ujinga.

Hapo, anastahili kujiuzulu hata kama serikali ilishirikishwa katika suala linalosubiriwa hatima yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: