Sheikh Gorogosi hakujua fitina


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Tanzia

SHEIKH Suleiman Gorogosi, mmoja wa wanazuoni mahiri nchini na daruweshi muhimu, ametutoka.

Alifariki dunia Jumamosi iliyopita, 27 Juni katika Kijiji cha Mnolela Wilaya ya Lindi Vijijini katika ajali ya gari.

Gari alilokuwa akisafiria lilipasuka tairi la mbele na gari kupinduka. Ilikuwa majira ya saa nane mchana katika barabara ya Mtwara-Lindi.

Sheikh Gorogosi alikuwa Naibu Mufti na mara kadhaa alikuwa Kaimu Mufti katika Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Wakati huohuo alikuwa sheikh wa BAKWATA mkoa wa Lindi.

Nimemfahamu vema Sheikh Gorogosi tangu miaka saba iliyopita. Ni katika uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mufti Mkuu wa Tanzania, uliofanyika 13 Oktoba 2002.

Uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biashara (CBE), mjini Dodoma. Ulifuatia kifo cha Sheikh Mkuu Hemed Bin Jumaa bin Hemed.

Sheikh Gorogosi alikuwa miongoni mwa wagombea tisa waliojitokeza katika kuwania wadhifa huo. Hakushinda. Alishika nafasi ya pili, nyuma ya Mufti wa sasa, Sheikh Shaban Bin Simba. Hakuwa na kinyogo.

Wengine walioshiriki katika kinyang’anyiro hicho ni mbunge wa zamani wa Kibiti, Pwani, Sheikh Profesa Juma Mikidadi, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Ma’amur, Dar es Salam, Sheikh Suleiman Kilemile, Sheikh Ahmed Twalib na Imamu Mkuu wa Msikiti wa Manyema, Kariakoo, Hamid Jongo.

Alipopewa nafasi ya kusema neno la shukurani baada ya matokeo kutangazwa, Sheikh Gorogosi aliwaliza baadhi ya masheikh waliokuwapo wakiwamo wale ambao hawakuwa wamemuunga mkono katika kinyang’anyiro hicho.

Alisema, “Bakwata kuna makundi ya fitina. Watu hawapendani; uchaguzi uliomuingiza Sheikh Simba madarakani umeacha vidonda vingi ambavyo ni Mufti pekee mwenye uwezo wa kuviponya. Kushindwa kushughulikia masuala hayo sasa, ni kuizika BAKWATA.”

Ni hekima. Ni uchambuzi wa hali halisi ya wakati huo. Ni utabiri wa yajayo.

“Watu watakwambia mengi,” alimwambia mufti mpya. “Watakwambia Gorogosi hili na lile, lakini jua kwamba umejipa dhima mbele ya Mwenyezi Mungu, si kuwagawa Waislamu, bali ni kuendeleza umoja na mshikamano wao. Hili ni jukumu ambalo usipolitekeleza utaulizwa mbele ya haki,” aliasa.

Sheikh Gorogosi alikuwa akirejea kauli na matendo ya baadhi ya masheikh waliokuwa wanashiriki uchaguzi huo na hata wale waliokuwa wanafuatilia.

Baadhi ya masheikh walifikia hatua ya kuwakejeli kwa maneno machafu baadhi ya wagombea, akiwamo Sheikh Simba mwenyewe aliyetuhumiwa kuvuta sigara, kupiga ramli na kwamba “si mcha Mungu.”

Siku zote Sheikh Gorogosi alikiri udhaifu uliopo katika chombo hicho, lakini alisema dawa si kukivunja, bali ni kwa waislamu kukisimamia ili kiwe bora.

Hakujawahi kutokea uchaguzi uliojaa hila na kila aina ya vituko kama ule uliomtupa Gorogosi na kumuibua Mufti Simba. Gorogosi ndiye aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.

Je, kifo cha Sheikh Gorogosi kina maana gani kwa mustakabali wa BAKWATA na uislamu kwa jumla?

Hakika, msiba huu ni mkubwa na umeacha pengo la aina yake. Ni wazi kwamba kuna mengi yatakosekana kutokana na kifo chake.

Kwanza, Sheikh Gorogosi alikuwa nguzo muhimu katika kuunganisha makundi ya waislamu ndani na nje ya BAKWATA.

Pili, Sheikh Gorogosi hakuwa mnafiki. Alikuwa mkweli na mcha Mungu. Hili linathibitishwa na hatua yake ya kukubali kushika nafasi ya Naibu Mufti, pale alipoteuliwa na yule aliyeshindana naye katika uchaguzi.

Hatua yake hiyo iliweza kupunguza, japo kwa kiwango kidogo, makundi yaliyokinzana ndani ya baraza hilo.

Tatu, Sheikh Gorogosi alikuwa kiunganishi kati ya Waislamu na watu wa madhehebu mengine; kati ya serikali na Waislam na wengi walikubaliana na baadhi ya mambo aliyotenda ili kuleta muwafaka.

Kwa mfano, muandamo wa mwezi wa Ramadhani. Mara kadhaa utasikia Waislamu wanauliza, “Mwezi umeandama? Nani ametangaza?” Jibu likiwa ni Gorogosi, wale waliokuwa na mashaka basi yanaisha na utakuta wakifunga au kufungua.

Ni Gorogosi aliyekuwa anakutana na viongozi wa madhehebu mengine kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana mawazo kwa mustakabali wa taifa. Hatua yake hiyo ilimjengea uadui kwa wenzake. Lakini hakujali. Aliendelea kufanya kazi hiyo hadi mauti yalipomkuta.

Ni ukweli usio na shaka kwamba Sheikh Gorogosi alikuwa mkweli na muumini mzuri wa Kiislamu; alitumia karibu maisha yake yote duniani kuitumikia BAKWATA.

Sheikh Gorogosi alizaliwa mwaka 1959 mkoani Lindi. Alipata elimu ya msingi mkoani humo kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Azra, nchini Misri ambako alihitimu shahada ya kwanza ya uenezi katika Uislamu.

Alianza kushika nyadhifa katika BAKWATA kama Katibu wa Mufti, cheo ambacho alikaa nacho kwa muda mrefu. Alishika pia nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Dini na mjumbe wa Baraza la Ulamaa ndani ya baraza hilo.

Kuna udhaifu na malalamiko ndani ya BAKWATA. Waislamu wanalalamikia hatua ya Sheikh Mkuu kuvunja Halmashauri Kuu ya BAKWATA (chombo kikuu cha maamuzi) na hivyo kufanya maamuzi mengi yeye binafsi.

Lakini kule kuwapo mtu mwenye uwezo, angalau wa kufafanua hatua hiyo na kuielezea kiufasaha, kulisaidia kupunguza munkari wa baadhi ya Waislamu, hasa wale wenye mawazo kuwa BAKWATA ni “chombo cha serikali.”

Jingine litakalokosekana kwa Waislamu, ni mawaidha yake kwao na hata kwa wale ambao si waumini wa madhehebu hayo.

Sheikh Gorogosi alikuwa hachoki. Kila alipotembelea mikoa mbalimbali nchini, alizungumza na Waislamu katika misikiti yao na kutoa darasa.

Kila anapopata nafasi ya kuzungumza, iwe kwenye radio, televisheni, au katika misikiti, Sheikh Gorogosi hakuweza kumaliza mawaidha yake, bila kuombea amani taifa lake. Hili nalo ni jambo jingine kubwa ambalo litakosekana kutoka kinywani kwa Sheikh Gorogosi.

Ndani ya Bakwata bado kuna makundi. Ni wazi kuwa kifo chake hakitayapunguza. Huenda kikayazidisha.

Ni wazi kwamba pamoja na msiba huu kuwa wa Waislamu wote, lakini walioondokewa zaidi na kuachwa wapweke, ni Mufti Simba na familia ya Gorogosi mwenyewe.

Habari za ndani ya Bakwata zinadai kuwa Mufti hana tena rafiki wa kweli. Pamoja na Gorogosi kuijua vizuri Bakwata na kushindwa katika uchaguzi na Mufti Simba, lakini bado alikuwa mtiifu kwa kiongozi wake huyo.

Alikuwa mshauri wake wa kweli na kwa hakika, bila Gorogosi, Mufti Simba angeshang’oka kitambo.

Lakini sasa wale waliokuwa wanataka Simba aharibikiwe, hawatataka wafuasi wa Gorogosi wabaki ndani ya baraza. Watataka kuwatokomeza.

0
No votes yet