Sheria ya Gharama Uchaguzi imekwama kabla kuanza


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 April 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

NATHUBUTU kusema kwamba sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 itaakayoanza kutumika kwenye uchaguzi wa mwaka huu, hakika haitaweza kuzuia rushwa kwenye uchaguzi kwa sababu tu ya kushindwa kujielekeza kwenye mambo mengi ya msingi kuhusu fedha za kushawishi uchaguzi.

Ninasema haya kwa sababu moja tu, kwamba wakati sheria inajielekeza kwenye uchaguzi kwa kuangalia mchakato wa uchaguzi kuanzia wakati wa kura ya maoni, kuteuliwa kwa wagombea, kuendesha kampeni na kisha upigwaji kura na kutangaza matokeo, imesahau kitu kimoja muhimu sana; kwamba ni vitendo gani hasa vya mbunge anayeshikilia jimbo la uchaguzi vinaweza kutajwa kama rushwa kwa mwaka wa uchaguzi?

Wakati nikiwa na ujasiri wa kufikia hitimisho hilo hapo juu jaribu kutafakari kwa kina matukio haya mawili; Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa, alituhumiwa hivi karibuni na wapinzani wake wa ndani na nje ya chama chake kwamba anacheza mchezo mchafu kwa kuwa amegawa Sh. 500,000 kwa kila kata ya jimbo lake.

Inadaiwa kwamba fedha hizo zimelenga kusaidia chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiimarisha. Wakati ya Profesa Mwakyusa yakitanda, wilayani Hai, Mbunge wao, Fuya Kimbita, anadaiwa kugawa vitabu kwa shule zote za sekondari za wilaya hiyo ambavyo vina thamani ya Sh. 168 milioni.

Vitabu hivyo vingi vikidaiwa ni vya sayansi vinaelezwa ni msaada kutoka taasisi ya Mama Anne Mkapa ya Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) na kwamba mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hai amekabidhiwa vitabu hivyo ili vigawanywe kwa shule zote za sekondari za wilaya hizo, za serikali na zile za binafisi.

Ukizipa mgongo taarifa hizi mbili, kuna zile za wabunge wengine wawili pia wa CCM, Basil Mramba wa Rombo na Aloyce Kimaro wa Vunjo, kuhudhuria hafla na viongozi wa dini kwa kisingizio cha kujadili maendeleo ya majimbo yao, lakini kimsingi wakieleza nia zao za kuendelea na kazi hiyo ya ubunge kama watateuliwa na vyama vyao.

CCM kwa upande wake, imeweka mipaka juu ya vitendo hivi, kwamba ikitokea anayefanya ni mbunge aliyeko madarakani kwake ni sawa, lakini akifanya mwananchi mwingine yeyote inaonekana kama ni hatari na ni uvunjaji wa kanuni na taratibu; kwa hiyo wananachi wengine ambao si wabunge wanakatazwa kwa kuwa eti kipindi cha kampeni bado hakijaanza.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba taifa hili limejikuta likijiruhusu katumbukia katika kina kirefu cha maangamizo ya kujitakia. Mwaka 2005 wakati rais Benjamin Mkapa anamaliza kipindi chake aliwambia mawaziri wake kwamba atashangaa sana kama kuna waziri atakataliwa na wananchi kwa sababu hakutimiza ahadi alizoahidi.

Mkapa alisema hivyo kwa sababu aliamini kwamba alikuwa amewapa mawaziri wake rasilimali nyingi na za kutosha kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika majimbo yao.

Kwa maelezo mengine mawaziri hawa walikuwa wamepewa upendeleo wa kutumia rasilimali za nchi kwa ajili ya majimbo yao, huu ndio utamaduni ambao umeachwa kuota mizizi kidogokidogo katika kuhamasisha maendeleo, wanasiasa sasa wamegeuzwa kuwa ndio wenye bajeti za maendeleo ya maeneo yao.

Lakini swali gumu likibakia, ni wapi wanapata fedha na rasilimali hizi? Je, ni kwa kuunganisha nguvu za wananchi au ni kusaka wafadhili? Au ni kwa kuchota kwenye mfuko mkuu wa serikali?

Utamaduni huu ndio umeifikisha nchi kwenye maamuzi ya kuanza kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) sasa wabunge ambao kwa mgawanyo wa madaraka ya dola wao ni wasimamizi wa serikali (utawala) sasa wanajiingiza moja kwa moja kuwa watendaji.

Hao ndiyo watakabidhiwa fedha ingawa kimkakati kutakuwa na kamati za maendeleo za kata ambazo zitakuwa zinaibua miradi kabla ya kupeleka mapendekezo yao ili fedha zitoke kwenye mfuko huo, bado kuanzishwa kwa mfuko huo ukimhusisha mbunge kwa karibu kiasi hicho ni mwendelezo wa kushindwa kutibu maradhi yetu sawasawa kama taifa ili tupate njia bora za kuleta tija na ufanisi katika kujitawala na kutawala nchi yetu.

Ni kwa nini mbunge anagawa fedha? Ni kwa nini mbunge anataka awe na mfumo wa fedha za maendeleo ya jimbo? Je, kuwepo kwa fedha hizi kunagongana au kunasaidia vipi majukumu ya halmashauri kwa mfano ambazo zina wajibu wa kushughulikia maendeleo ya wilaya husika?

Majibu ya maswali hayo hapo juu yanatufikisha kwenye hitimisho moja tu, kwamba wabunge wamepanua mno wigo wa majukumu yake kiasi kwamba hawajui wafanye nini na waache nini, ndiyo maana wabunge wanakuwa wafadhili, wanakuwa serikali na sasa wanataka kukamata bajeti ya serikali waitekeleze wao.

Katika mkanganyiko wote huu picha inayojengwa ni moja tu, kwamba ni vitendo gani vinaweza kutajwa kuwa ni ukiukaji wa kanuni na sheria za uchaguzi, kama mbunge aliyeko madarakani anaruhusiwa kuwa benki, mfadhili, mtendaji wa serikali na hapo hapo mwanasiasa wa kusimamia shughuli za serikali?

Inawezekana vipi iwe ni kosa kwa mwananchi mwingine yeyote kumwaga fedha kwenye jimbo kipindi ambacho mbunge naye anamwaga lakini isionekane kuwa kosa? Ni kwa sababu tu wabunge wamejipanua na sasa hawajui hata ukomo wa majumu yao.

Wabunge badala ya kuwa wahamasishaji na wasimamizi wa shughuli hizi sasa wanafanya wenyewe na kwa bahati mbaya serikali imepotea njia kwa kuruhusu kupitisha sheria ya kuwafanya wabunge kuwa na nguvu katika mifuko hii.

Ni vigumu sasa kutenganisha vitendo vya kununua wananchi kwa kujielekeza tu pale kura za maoni zinapoanzia, huku kipindi kingine mbunge akiruhusiwa kuendesha vitu hivyo bila hata usafi wa fedha anazotumia kuhojiwa kokote.

Ni kwa njia hii kadri nguvu za wanasiasa zinavyoachwa kujitanua na kupora madaraka ya mihimili mingine, ndivyo inazidi kuwa vigumu kupiga vita fedha chafu katika uchaguzi, kwa sababu kwa majimbo mengine harakati za uchaguzi zinaanza mapema miaka miwili au hata mitatu kabla ya uchaguzi, kwa hali hii sheria hii ya fedha za uchaguzi itatusaidia nini? Tumekwama kabla ya kuanza!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: