Sheria ya Gharama za Uchaguzi haitekelezeki


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Rais Jakaya Kikwete

SHERIA ya uchaguzi iliyosainiwa kwa mbwembwe na Rais Jakaya Kikwete, imetajwa kuwa “imekufa kabla ya kutumika.”

Wapo wanaodai pia kwamba sheria ya hiyo “imetungwa gizani” kwa lengo la kurudisha taifa katika ujima.

Baadhi ya vifungu vya kanuni zilizopendekezwa kutumika, vinapingana na Katiba ya Jamhuri. Vingine vinakinzana na katiba ya baadhi ya vyama vya siasa nchini.

Kanuni nyingi zilizotungwa, zinashurutisha vyama kufuata mfumo wa kupata wagombea unaotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kana kwamba vyama vyote vimejiweka katika kwapa la chama hicho.

Jumatano iliyopita, Rais Kikwete alisaini sheria ya gharama za uchaguzi ikulu Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza, hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na watu kadhaa mashuhuri, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, majaji, viongozi wa vyombo vya dola na waandishi wa habari.

Ndani ya ikulu, matarumbeta yalipigwa. Viongozi walijipanga mduara kushuhudia rais akitenda jambo lililoitwa la “historia.”

Hata hivyo, pamoja na sheria iliyosainiwa na Kikwete kufanyiwa “ukarabati mkubwa” kabla ya kupitishwa bungeni, imetungiwa kanuni zilizorudisha kinyemela baadhi ya maeneo yaliyoondolewa.

Kwa mfano, kifungu cha 14(e) cha kanuni kinaongeza sharti jipya ambalo halikuwamo katika sheria iliyopitishwa na Bunge.

Serikali inataka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye kazi ya ukaguzi wa hesabu za kila mgombea. Kifungu hiki kilikuwamo katika mapendekezo ya sheria iliyowasilishwa bungeni, lakini pendekezo hilo lilikataliwa na Bunge.

Badala yake, sheria inataka mgombea kuandaa taarifa ya matumizi ya fedha alizotumia katika kampeni zake. Kanuni iliyotungwa inamtaka mgombea kuwasilisha “taarifa iliyokaguliwa” na CAG.

Katika kukiondoa kifungu hiki, bunge lilisema kwamba CAG hatakuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kutokana na mazingira hayo, kuongeza kifungu hiki ambacho hakimo katika sheria ni batili.

Aidha, kifungu cha 5(5) cha kanuni kinaenda kinyume na Katiba ya Jamhuri kwa kushindwa kutoa haki ya kusikilizwa kwa mgombea. Hii ni kinyume na sheria ya uchaguzi iliyopitishwa na kusainiwa na rais.

Mapungufu mengine katika sheria hiyo, ni pale sheria iliporuhusu vyama vya siasa kuchangiwa na mtu binafsi au taasisi ya umma, zikiwamo taasisi za kidini.

Sheria inatoa uhuru kwa taasisi au mtu binafsi kuchangia kampeni za vyama vya siasa au wagombea mmoja mmoja. Kwa upande wa mtu binafsi, sheria imeruhusu Sh. 1 milioni na vyama Sh. 2 milioni.

Mchango unaozidi kiasi hicho cha fedha unatakiwa uripotiwe katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndani ya siku 30 tangu ulipopokelewa.

Hii ina maana kwamba kama mtu binafsi atachangia Sh. 999,999 na taasisi Sh. 1,999,999, hatalazimika kutoa ripoti kwa msajili. Hapa kuna mapungufu mawili makubwa.

Kwanza, hatua ya kuruhusu taasisi za umma kuchangia kampeni za mgombea au chama cha siasa, inaweza kutumbukiza taifa katika ukwapuaji mwingine wa fedha za umma.

Tayari umma unakumbuka kilichotendeka mwaka 2005 ambapo mabilioni ya shilingi yalikwapuliwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited na washirika wake wengine.

Pili, kukosekana kwa kipengele kinachobana wagombea au vyama kutofikisha kwa msajili taarifa ya fedha walizokusanya na kukatiwa risiti, kutaifanya ofisi ya msajili kushindwa kutimiza majukumu iliyopewa na sheria hii.

Hata kule kutolazimisha msajili kutaja hadharani wachangiaji, kutaifanya sheria iliyopitishwa kuwa kibogoyo.

Ibara ya 12 ya sheria iliyopitishwa na ambayo imesainiwa na Rais Kikwete, inaminya haki za raia wa Tanzania waliopo nje ya nchi kushiriki katika mchakato wa kisiasa nchini. Huu ni ubaguzi inaokatazwa hata na katiba ya Jamhuri.

Sheria inakataza raia hao kutoa michango, kusaidia katika kutangaza kampeni au mgombea wanayemtaka. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, serikali kuwatenga raia wake.

Wakati serikali ikifanya hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendeshwa kwa fedha kutoka nje. Hata serikali yenyewe, kwa kiwango fulani, inaendeshwa kwa fedha za wahisani.

Lakini kibaya zaidi, sheria iliyotungwa haikatazi wageni walioko nchini kuchangia vyama vya siasa.

Jingine ni pale sheria inapokataza hata ahadi kutolewa na wagombea kwa lengo la kushawishi wananchi. Inakatazwa mgombea kufanya makubaliano na wapigakura kwa kuahidi, “Mkinichagua nitafanya hili au lile.” Hii ni katika ibara ya 21.

Hata kifungu cha 15(3) cha kanuni, kimepachikwa kinyemela na hakiendani na sheria iliyotungwa. Kimsingi kanuni hiyo haitekelezeki.

Katika kifungu hicho, kanuni inamtaka mgombea kuweka kumbukumbu zake kwenye “Electronic Form” – zilizonaswa au kunakiliwa kwa mfumo wa elektroniki.

Katika mazingira ya Tanzania ni mgombea gani au msaidizi gani wa mgombea ubunge asiyekuwa waziri, au mfanyabiashara mkubwa, anayeweza kutimiza sharti hili la kanuni?

Sheria inakubali stakabadhi na taarifa za fedha zilizosainiwa kulingana na mazingira yaliyopo. Kanuni iliyotungwa na ambayo serikali inataka kuipitisha, imesahau hata sheria inayotaka wagombea kujua kusoma na kuandika tu.

Kimsingi sheria ina matatizo mengi. Kanuni zilizotungwa na ambazo serikali imeshikia bango kutaka kuzipitisha zimejaaa utata. Hata hivyo, katika mazingira ya sasa ya CCM, waathirika wa kwanza wa sheria hiyo watakuwa wagombea wa chama hicho.

Hii ni kwa sababu, wagombea wengi ambao hawatatakiwa na wakubwa wa CCM wataondolewa kwa kutumia visingizio visivyokuwa na macho.

Hata utaratibu wa CCM wa kuendesha kura za maoni utaibua matatizo mengine ndani ya sheria iliyopitishwa.

Kwa mfano, iwapo CCM itatekeleza mkakati wake wa kubeba wagombea wake pamoja, kuna uwezokano mkubwa wa baadhi ya wagombea kutofikia wapigakura kwa kuwa ratiba na vitendea kazi vitatolewa na chama chenyewe.

Je, CCM ya sasa inaweza kusimamia hili katika misingi ya haki? Inaweza kubeba wagombea wote katika gari moja, wakati ambapo hata Kikwete anajua kuwa baadhi yao hawaaminiani hata kuachiana glasi ya maji?

Au Kikwete anata kutuambia kwamba haya yanaweza kumalizika katika kipindi hiki kifupi cha miezi minne iliyosalia?

Hii ndiyo maana baadhi yetu tunaamini kuwa kabla ya Kikwete kuibuka na sheria hii, kwanza angeimarisha chama chake. Angekirudisha katika misingi yake ya asili – Ujamaa na Kujitegemea – kabla ya kutafuta ugomvi na wenzake.

Angeimarisha idara yake ya maadili kwa kuipa nyezo za kufanyia kazi yale yatakayoletwa kwake. Ingekuwa kama ilivyokuwa wakati wa kipindi cha kwanza cha utawala wa Benjamin Mkapa.

Rais Mkapa alitumia kamati ya maandili kufyeka wagombea wasiokuwa na sifa ya uongozi kupitishwa na chama chake.

Hata hivyo, alishindwa kusimamia hilo wakati anaondoka madarakani. Wengi wasiokuwa na sifa ndio waliopitishwa. Hata tuhuma za wazi alizopelekewa na kamati anadaiwa kutozifanyia kazi.

Moja ya tuhuma kubwa ambazo anabebeshwa Mkapa ni ile ya kuweka kapuni taarifa ya kamati ya maadili iliyokuwa inatuhumu wapambe wa Kikwete kuwa walitumia fedha kununua kura.

Kabla ya Kikwete kupitisha sheria hii, angeshughulikia kwanza viongozi aliodai kuwa wanakipeleka chama chake nje ya misingi yake kwa kuzika miiko ya uongozi.

Angevunja mitandao iliyotapakaa kuanzia ngazi ya chini hadi taifa inayoundwa mara uchaguzi mmoja unapomalizika kwa lengo la kuratibu mbinu za ushindi wa makundi katika uchaguzi unaofuata.

Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miaka mitano, hakuna kazi ya maana ya maendeleo inayofanyika. Ni vikao vya kufitiniana na kuchafuana mtindo mmoja.

WanaCCM, katika ngazi zote, wako katika makundi. Kuna wanaounga mkono uongozi unaokuwepo katika ngazi zote na wengine wanaunga mkono “viongozi watarajiwa” wanaopiga jaramba kuwania uongozi mara huyu aliyepo anapomaliza muda wake.

Katika mazingira haya, ni vigumu kuwa na sheria inayoweza kuwajibisha viongozi wa aina hii. Kinyume chake unakuwa na sheria inayohubiriwa kupitia majukwaani na vyombo vya habari, lakini inayoshindwa kutenda kazi.

Rais angejiuliza sheria hiyo anataka kuitumia kupitia chama gani: Hiki kilichoitwa “kokoro” na mwasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere? Hiki kinachoingiza wanachama kwa mtindo wa “papo kwa papo” na bila kujali itikadi?

Je, sheria hiyo anataka kuitumia katika serikali ambayo kipaumbele chake hakijulikani?

Hapa rais angepaswa kujitazama yeye binafsi. Kwa mfano, kama anashindwa kuwajibisha watuhumiwa wa ufisadi kupitia vikao halali vya chama chake, anawezaje kuwajibisha wanaotumia rushwa kuingia madarakani?

Jingine ambalo rais angelifanya kabla ya kuleta sheria iliyolenga kuengua wenzake katika chama, ni kujiuliza iwapo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeenea katika ngazi ya kata, vijiji na vitongoji ambako uchaguzi unafanyika?

Angejiuliza iwapo Takukuru wana nyezo za kufanyia kazi anayotaka kuwapa; mtandao wake ukoje, kama wana ubavu wa kusimamia sheria iliyopitishwa na kama yeye yuko tayari kuiachia ifanye kazi yake hata kama itamuumbia binafsi.

Vinginevyo, sheria iliyosainiwa kwa mbwembwe itakuwa ya kibaguzi kwa kuonea mwenye haki na kufumbia macho rafiki wa mtawala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: