Sheria ya madini chafu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Waziri wa Nishati na Madini,  William Ngeleja

HAPO zamani wananchi walioishi katika maeneo yenye madini waliamka asubuhi na kuokota madini yaliyoota kama uyoga. Waliuza na kumaliza shida zao.

Kuna waliokutana na dhahabu wakiwa wanachimba vyoo, makaburi au wakielekeza maji yaliyopotea njia na kuingia kwenye vibanda vyao.

Nao walichukua madini hayo, yawe dhahabu, almasi, tanzanite, madini mengine au vito vya thamani, kuyauza na kujikimu.

Ni kujikimu kwa kuwa madini yaliyopatikana kwa njia hiyo yalikuwa machache. Hata hayo machache yaliuzwa kwa wachache waliojua thamani; hivyo wauzaji walikuwa hawapati bei ya soko la kimataifa.

Kuja kwa uchimbaji mkubwa kuliongeza bei ya madini yaliyookotezwa. Miji mdogo iliyoko katika maeneo ya madini ilijengwa kwa fedha zilizopatikana kutokana na kuuza madini ya kuokoteza au yaliyokombwa kwenye mabaki ya mawe na mchanga uliotolewa migodini; au kutokana na uchimbaji wa kijima kwa kutumia majembe, vijiti, visu, vihosho, na vitu vingine vyenye ncha.

Bali kuja kwa wachimbaji wakubwa kuliambatana na tabia ya kuhodhi. Wananchi walisukumwa kutoka makazi yao ya miaka nendarudi. Walisukumwa mbali na migodi.

Kwa kuwa, kwa mfano nchini Tanzania, madini yameshonana chini kwa chini na kwa masafa marefu, bado hata walioswagwa na kupelekwa mbali waliweza kupata madini.

Tarehe 23 mwezi uliopita mjini Dodoma, bunge lilipitisha muswada wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Chini ya sheria hii ni wale tu waliosajiliwa rasmi au mawakala wao ambao wataruhusiwa kukutwa na madini mkononi, mfukoni, nyumbani au kokote kule kwenye miliki yao.

Kama huna leseni – ya uwakala, uchimbaji, kunua au kuuza – kitendo tu cha kuwa na mdini ni jinai ya aina yake.

Kwa sheria hiyo, iwapo rais atasaini muswada huo (na atausaini kwa kuwa ulipelekwa bungeni chini ya hati ya dharura), mara moja wote watakaokutwa na madini, ni wahalifu.

Dhahabu, almasi na madini mengine, kwa mujibu wa sheria hii, siyo tena mali ya wananchi wote kama ilivyokuwa. Itabidi wayatazame kwa woga na hata kuyakimbia.

Muswada ukisainiwa na Rais Jakaya Kikwete, utaleta sheria inayofanya madini kuwa mali ya wengine; na hasa mali ya wazungu au wamarekani au makaburu wa zamani au wenyeji wenye fedha nyingi za kuwekeza machimboni.

Watu masikini waliokuwa “wakibahatika kuokota” dhabu au almasi, watakuwa wakiayaangalia kwa uchungu.

Tofauti ya watu hao na mbuzi katika eneo hili la kuwa au kutokuwa na dhahabu, ni kwamba mbuzi hajui ni kitu gani lakini binadamu atajua kuwa ni hatari kuwa nayo. Sheria mpya ya madini.

Sheria inaelekeza kila anayeokota kipande cha madini sharti akipeleke kwa mwenye leseni. Waziri muhusika ameelekezwa na bunge kutunga kanuni za kurahisisha utaratibu – utekelezaji na hasa urahisishaji utekelezaji wa “unyang’anyi” huo.

Kuna wabunge walioonekana kushangilia Kifungu 18 (1) cha sheria hiyo kinachonyang’anya haki, fursa na hata bahati ya mkazi wa maeneo yenye madini kukusanya madini bila leseni.

Baadhi ya wabunge wamekwenda mwendo wa ushabiki wakidai kuwa kila kipande cha dhahabu kikikusanywa na kuuzwa panapoelekezwa, basi mrabaha wa serikali utakuwa mkubwa.

Ndoto? Ufinyu wa mawazo? Iko wapi harufu ya mrabaha ambao imekuwa ukitolewa? Kwani kuziba fursa za masikini kuneemeka na “walichopewa na Mungu,” kuna uhusiano gani na kukua kwa uchumi au uboreshaji wa maisha yao?

Kama wananchi waliokoteza madini na kujenga makazi yao, madogo na ya thamani ndogo kama yalivyo, leo wakinyang’anywa haki ya kuvuna utajiri wao, nani ataangalia maisha yao katika mazingira ya ufisadi na unyang’au usiomithilika?

Kuna suala la taratibu. Mwananchi anayeishi kilometa 50 hadi 100 kutoka aliko mwenye leseni ya kuwa na madini, atamfikiaje mtu huyo mwenye ruhusa ya kipekee ili awasilishe jiwe lake?

Kupatikana kwa kipande cha dhahabu, kwa mfano katika mazingira ya shamba na ya umasikini, ni habari kuu isiyoweza kufichwa.

Mchwa, sisimizi, ndege, mifugo, wanyama, nyasi, miti na hata upepo – vyote vitanong’ona – Masele kaokota “zaabu” au almasi. Sasa Masele atapita wapi kufikia mwenye leseni katika mazingira ya sheria hii?

Kipande cha dhahabu au almasi kinatosha kumfanya mtendaji wa kijiji au kata, mwenye uroho wa fisi, kuanzisha vitimbi na hata kuamuru mwenye “muokoto” kukamatwa kwa madai ya kutenda kosa la jinai.

Kwa kosa la kukutwa na madini yanayopatikana katika maeneo ya wananchi, na siyo ndani ya migodi – kwamba mtu binafsi atozwe faini isiyozidi Sh. 10 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote viwili – hakika ni kutangaza jahanamu kwa wengi.

Raia anafungwa kwa kuwa na kipande cha utajiri katika eneo alikozaliwa au kuishi kwa muda mrefu, lakini tajiri na raia wa nje anapewa leseni ya kuvuna kwa wepesi na wakati mwingine kwa ubia wa wizi na maofisa wa serikali.

Ni sheria chafu. Itakomoa wengi. Itanyang’anya haki, fursa na kupoteza “bahati” za wengi. Wanaoipenda wana lao jambo: kuvuna pamoja na wenye leseni. Waulize watifuaji ardhi kwa koleo ambao wameishi kwa anjia hiyo kwa miaka yote ya maisha yao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: