Sheria ya madini inufaishe taifa


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 25 August 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amenukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema Muswada wa Sheria mpya ya Madini ya Mwaka 2009 utawasilishwa bungeni mwaka huu.

Amesema sheria mpya itafuta Sheria ya Madini ya mwaka 1998 iliyotokana na Sera ya Madini ya Mwaka 1997. Bali waziri hakusema iwapo muswada huo unatokana na mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Jaji Bomani au ile ya Tume ya Jenerali Robert Mboma.

Vyovyote iwavyo, ripoti zote mbili hazijawahi kuwekwa hadharani. Kuhusu Tume ya Jaji Mark Bomani, waziri amenukuliwa akisema, “imeonyesha mapungufu mengi katika sekta ya madini, hivyo serikali inaendelea kuifanyia kazi.”

Hii ina maana kwamba ni waziri na labda watendaji kadhaa serikalini ambao wameona ripoti hiyo. Wananchi wengi hawajaiona na hawajaichangia mawazo.

Nilitaraji waziri angesema kuwa muswada wa sheria atakaouwasilisha bungeni unatokana na mapendekezo ya ripoti hiyo ya Tume ya Jaji Bomani na hata ile ya Tume ya Jenerali Robert Mboma.

Haiwezekani muswada uwe tayari, lakini wakati huohuo ripoti ya Tume ya Jaji Bomani ikiendelea eti kuchambuliwa au kwa maneno ya kisiasa “kuifanyia kazi”.

Suala la raslimali kama madini limekuwa ni jinamizi lingine katika uchumi wa nchi hii. Ufumbuzi wake lazima upatikane kwa kuwepo sheria isiyotoa mwanya tena kwa wawekezaji kupora madini yetu wakituachia mashimo tu.

Naamini Tume ya Bomani na hata ile ya Jenerali Mboma ilifanya kazi nzuri ikitumia kihalali fedha za walipakodi na hivyo si vizuri ikapotea bure. Hii inatokana na umakini wa wajumbe wa tume hiyo.

Wajumbe walikuwa John Cheyo (UDP ), Zitto Kabwe (Chadema), Dk. Harrison Mwakyembe (CCM) na Ezekiel Maige (CCM).

Hadidu za rejea za Tume zilikuwa pamoja na kuchunguza mikataba ya madini kutokana na sheria zake, kuchambua mfumo wa kodi, kupitia mfumo wa usimamizi wa uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali, na kukutana na taasisi zinazosimamia madini na wadau wengine wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo.

Kwa hiyo Ripoti ya Tume ya Jaji Bomani ni ufumbuzi wa masuala mengi kuhusu raslimali kubwa ya madini ya aina mbalimbali nchini, hususan dhahabu ambayo inachimbwa na makampuni makubwa ya Ulaya na Marekani.

Watanzania tunataka kujua tunavyoweza kunufaika na madini hayo, kama ambavyo rais mwenyewe amekuwa akisema mara nyingi akiwa na nia hata ya kutaka mikataba iliyopo ibadilishwe ili serikali inufaike kwa kiasi chote cha madini yanayochimbwa.

Wakati Ngeleja akionyesha manufaa ya madini yatakuwepo kwa mujibu wa sheria mpya, azingatie pia hoja za wadau wengine.

Kwa mfano azingatie hoja zilizojitokeza mwaka jana katika mjadala kati ya wanaharakati watafiti wa masuala ya rasilimali asilia na mazingira wakiongozwa na Wakili Tundu Lissu wa LEAT na Chama cha Wachimba Madini na Nishati [TCME].

Wakili Tundu Lissu na mwanaharakati mmoja mzungu, Mark Curtis, waliandika kitabu kilichodhaminiwa na asasi za madhebu ya Kikristo na Kiislam wakieleza jinsi sekta ya madini, hasa dhahabu, isivyonufaisha nchi.

Kwa upande wake TCME imeeleza kwamba utafiti huo haukuwa na ukweli wowote kuhusu hali halisi kwani wachimbaji madini wakubwa [LSM] wana mchango mkubwa kwa pato la taifa.

Kutokana na mjadala na malumbano yaliyoenda na takwimu, tunataraji Ripoti ya Tume ya Jaji Bomani imesema ukweli ambao sasa unahitaji kulindwa kisheria.

Mara nyingi sheria zetu zimekuwa ni sawa na kitanzi tunachojitengenezea wenyewe. Mfano ni sheria ile ya Madini ya Mwaka 1998 ambayo itafutwa. Nadhani ni moja ya sheria mbovu sana zilizowahi kutungwa nchini. Imewanufaisha sana wawekezaji wakubwa katika madini.

Siyo vibaya kukumbuka jinsi machifu wa Tanganyika (wakati huo) walivyoingizwa mkenge katika mikataba na Carl Peters wakati wa kuanza kwa ukoloni wa Wajerumani. Waliwapa wakoloni hao nchi kwa mikataba ya kijinga ambapo malipo yalikuwa pipi, shanga na bunduki (magobole).

Enzi hizo za ujinga hazipaswi kurudi tena kupitia watawala wetu wa sasa ambao ni wasomi kama akina Ngeleja (mwenye shahada mbili za sheria za mikataba na uwekezaji).

Hapana budi kujifunza kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye hakuruhusu masuala ya ardhi na madini yachezewechezewe ovyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: