Sheria ya Tendwa utata mtupu


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
John Tendwa

UAMUZI wa Msajili wa Vyama Vya Siasa, John Tendwa juu ya pingamizi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), umefichua utata uliopo katika sheria tatu za uchaguzi nchini.

Tendwa alitupilia mbali juzi Jumatatu, pingamizi la CHADEMA dhidi ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kuhusu ukiukaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa mtiririko wa usimamizi wa haki, kama rufani itashindikana kwa msajili, walalamikaji waweza kwenda mhakamani kudai haki, kama sheria ya matumizi inavyoelekeza.

Kwa mujibu wa mwanasheria na wakili maarufu nchini, Dk. Sengondo Mvungi, sheria tatu zinaongoza uchaguzi mkuu unaofanyika mwaka huu.

Dk. Mvungi anayefundisha Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alizitaja sheria hizo kuwa ni sheria ya gharama za uchaguzi, sheria ya uchaguzi na sheria ya serikali za mitaa.

Sheria ya gharama na ile ya uchaguzi zinatumika katika uchaguzi wa rais na wabunge na sheria ya serikali za mitaa inashughulika na chaguzi za vitongoji na vijiji.

“Tatizo kubwa la Tanzania ni kwamba kuna sheria tatu tofauti zinazohusika na uchaguzi moja kwa moja. Hili ni jambo ambalo linaweza kuleta matatizo huko tuendako.

“Kwa mfano, sheria ya uchaguzi hairuhusu vyama kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani. Sheria ya gharama inaruhusu walioshindwa kwenye pingamizi waende mahakamani. Huu ni mkanganyiko,” alisema katika mahojiano na gazeti hili juzi Jumatatu.

Mvungi ambaye mwaka 2005 aliwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, alisema sheria ya gharama za uchaguzi ilipitishwa kwa pupa.

“Kama Tendwa amekataa pingamizi hilo la CHADEMA, mimi nawashauri waende mahakamani haraka, hata leo ikiwezekana, ili tukajue kama nayo (mahakama) itatoa maamuzi kama ya Tendwa,” alisema Mvungi.

Tendwa ameandika katika uamuzi wake juzi kwamba malalamiko yote ya chama hicho dhidi ya CCM na Kikwete “hayana msingi na yanaamsha chuki baina ya wanachama wa vyama hivyo viwili.”

Hata hivyo, matokeo ya uamuzi huo yanaweza kuibua matatizo makubwa kwa serikali kutokana na mkanganyiko wa kisheria ulioletwa na uamuzi huo.

Wakili Mabere Marando ambaye ni mmoja wa washauri wa CHADEMA, alizungumza na gazeti hili juzi usiku na kusema hawakutarajia kitu tofauti kutoka kwa Tendwa.

“Tulijua kabisa kwamba Kikwete na Tendwa lao ni moja. Walikutana kabla hajatoa uamuzi na ushahidi tunao. Sheria iko wazi (ya gharama za uchaguzi). Tendwa akasoma hiyo sheria na kutoa baadhi ya vipengele ili apate visingizio,” amedai Marando.

Marando amesema Kikwete ndiye amesema uongo majukwaani, kwamba ameongeza mishahara. Hili linathibitishwa na chama chenyewe kwa kauli ya Yusuf Makamba, katibu mkuu wa CCM, kwamba Kikwete hajaongeza mishahara.

“Akiongea kwa simu kutoka ofisini kwake, Marando alisema Kikwete alikataa kura za wafanyakazi na baadaye akawadanganya wafanyakazi kuwa amewaongeza mishahara; kumbe si kweli, hajaongeza chochote,” ameeleza.

Alipoulizwa na gazeti hili iwapo CHADEMA wana mpango wa kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Tendwa, wakili Marando alisema; “Hatuendi. Tuna kazi moja kubwa ya kuwaambia wananchi kuwa Kikwete ni muongo aliyekubuhu. Serikali yake imejaa wezi.”

“Na chama chake na yeye mwenyewe (Kikwete), wamefaidika na fedha za EPA; na wala hana ubavu wa kupambana na mafisadi kwa vile hao wanaoitwa mafisadi ni marafiki zake,” amesema Marando.

Mgogoro kati ya sheria ya gharama na ile ya uchaguzi umeonekana pia katika mabango ya kampeni yanayotumiwa na CCM kumnadi Kikwete.

Kwa mujibu wa sheria ya gharama, Tendwa aliwaambia waandishi wa habari juzi kwamba CCM hairuhusiwi kutumia picha zilizotengenezwa au zinazoihusisha CCM moja kwa moja na alama za serikali.

Hata hivyo, Makamba, alizungumza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) baada ya mkutano wa Tendwa na waandishi na kusema, chama chake hakikukosea kutumia mabango hayo.

Makamba alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, mabango yote ya kampeni yanatakiwa kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kabla ya kutumika na mabango yote ya CCM yamepitishwa.

“Anayeruhusu mabango ya kampeni ni NEC kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi. Nina barua ya tume inayoniruhusu kutumia mabango tunayoyatumia. Hatujavunja sheria yoyote,” alisema.

Agosti 30 mwaka huu, CHADEMA iliwasilisha pingamizi lake katika ofisi za Tendwa jijini Dar es Salaam ikiwa na malalamiko makubwa matatu.

CHADEMA ililalamika kwamba Kikwete akitumia nafasi yake kama Rais wa Tanzania, ameongeza na au kuahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi nchini.

Madai mengine ni kwamba mgombea wa CCM alitumia nafasi yake kama rais kuahidi kulipa Chama cha Ushirika cha Nyanza kiasi cha Sh. bilioni 5 ili kilipe madeni yake.

Aidha, CHADEMA ilikuwa imelalamika pia kuwa mgombea wa CCM alikuwa akitumia wadhifa wake wa rais kama alivyofanya huko Kagera kuahidi watu wa mkoa huo kuwa atanunua meli mpya ya kisasa itakayotumika kwa safari za kutoka Bukoba hadi Mwanza.

Walidai kuwa vitendo hivyo vilikuwa na nia ya kushawishi wafanyakazi kama wapiga kura kumpigia kura Kikwete kutokana na nyongeza hiyo ya mishahara.

CHADEMA iliwasilisha pia ushahidi wa baadhi ya magazeti ambayo yalikuwa yameripoti kwa kina matukio ya Kikwete kutoa ahadi zake hizo kwenye mikutano ya kampeni.

Akijibu malalamiko hayo ya CHADEMA, Tendwa amesema ununuzi wa meli na ulipaji wa deni la Nyanza ni miongoni mwa mambo yaliyomo katika utekelezaji wa ilani ya CCM kwa mwaka 2010.

Alisema ahadi hizi hazina tofauti na zile za wapinzani wanaoahidi kwamba watakapoingia ikulu watasomesha watu bure kuanzia elimu ya msingi na kufuta kodi zote kandamizi.

Pia alisema ahadi hizo haziwezi kuchukuliwa kuwa kama hongo kwa vile, katika mazingira ya kwaida hongo hutolewa katika mazingiya ya kificho, lakini Kikwete alizungumza hadharani katika mambo ambayo yamewekwa wazi kwenye ilani.

Kuhusu nyongeza ya mshahara, Tendwa alisema CHADEMA ilishindwa kuonyesha ushahidi kwamba Kikwete ameongeza mshahara katika kipindi hiki cha kampeni.

Pia alisema nyongeza ya mshahara anayozungumzia Kikwete kwenye mikutano ya kampeni ni ile ya hadi Sh. 135,000 ambayo ilipitishwa bungeni Juni 10 mwaka huu, kabla ya kampeni za urais kuanza.

Tendwa alikosoa pingamizi la CHADEMA akidai kwamba lilionyesha udhaifu mkubwa wa weledi wa sheria ya gharama za uchaguzi na tuhuma nyingi zilikuwa hazikuthibitishwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: