SHERIA YA UCHAGUZI: Nani wa kumnyooshea kidole Kikwete?


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

KWA muda mrefu sasa kutoweka kwa maadili, utawala bora na uwajibikaji ndani ya uongozi wa juu wa nchi kimekuwa si kitu cha mjadala.

Lakini hakuna wakati katika historia ya nchi hii ambapo mapungufu haya yanaonekana waziwazi na kutisha, kama siyo kukera wengi kama wakati huu wa kampeni za uchaguzi.

Wenye kumbukumbu na historia nzuri ya nchi yetu, watakubaliana nami kwamba kampeni za uchaguzi za mwaka huu uongozi ulioko madarakani umegubikwa na vitendo na kauli nyingi zinazoonyesha kuporomoka kwa uzingatiaji wa maadili, uwajibikaji na uvunjifu wa sheria na kanuni kuliko wakati mwingine wowote uliopita.

Lakini kikubwa zaidi kinacholeta wasiwasi mkubwa ni kwamba viongozi wa vyombo au taasisi ambao wana uwezo na mamlaka ya kukemea vitendo na kauli hizo wamekuwa kimya – hali ambayo inazidi kuingiza hofu ya mwelekeo wa nchi.

Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kiko madarakani, na serikali yake ndiyo inayoandaa mazingira ya uchaguzi na kuusimamia. Kama ni mchezo wa mpira, basi yenyewe ndiyo mchezaji na mwamuzi.

Maadili mema pekee – achilia mbali uzingatiaji wa kanuni za vyombo vya sheria hususan mahakama – yanataka mtu asiingilie mienendo ya kesi zilizopo mahakamani, na kama mtu huyo ni mgombea urais ambaye tayari ni rais, basi ukiukwaji huo uchukuliwe kwa uzito wake.

Lakini iwapo mgombea huyo atapuuza maadili, sheria na kanuni hizo, basi awajibishwe, au hata akaripiwe, haidhuru kwa lengo la kukumbushana.

Ili uwe wa maana, uwajibishaji au ukaripiaji huo usitoke kwa wananchi wa kawaida pekee, bali utoke kwa viongozi wa vyombo au taasisi husika zilizopo – hususan zile zinazoguswa na ukiukwaji huo.

Nitatoa mifano miwili. Katika uchaguzi wa mwaka 1980, Chediel Mgonja (sasa marehemu), ambaye alikuwa waziri katika serikali ya awamu ya kwanza, alishinda kiti chake cha Same, lakini baadaye mpinzani wake alifungua kesi mahakamani kupinga ushindi wake na kufanikiwa kutengua ushindi wake.

Aidha katika hukumu yake, Mahakama Kuu iliyosikiliza kesi hiyo ilitoa amri kwamba kwa kuwa ushahidi uliotolewa ulithibitisha Mgonja alitoa hongo kwa wapiga kura, basi asipewe uongozi wowote wa taifa kwa kipindi cha miaka kumi.

Baada ya uchaguzi Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa rais wakati huo alimteua Mgonja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga – kinyume kabisa na amri ya Mahakama Kuu.

Hili liliwaudhi sana majaji wa Mahakama Kuu. Haraka wakampelekea rais malalmiko wakionya kwamba pindi Mgonja akiapishwa nafasi ya ukuu wa mkoa walikuwa tayari kujiuzulu kuliko kupuuzwa na mhimili wa dola yaani ule wa utawala chini ya rais.

Nyerere alipima hoja akaona uzito wake akafuta uteuzi wa Mgonja kuwa mkuu wa mkoa. Pili, Nyerere alianzisha mahakama maalum (special tribunals) kushughulikia watuhumiwa waliokamatwa katika ile ‘vita’ dhidi ya ‘wahujumu uchumi’ nchini mwaka 1983.

Sheria ya Economic Sabotage (Special Provisions) Act, 1983 iliyopitishwa na Bunge kwa spidi ya zimamoto ndiyo ilianzisha mahakama hizo ambazo zilikuwa nje ya mfumo wa mahakama za kawaida.

Rais ndiye aliteua majaji kusikiliza kesi hizo akisaidiwa na wazee wawili wa baraza. Aidha mtuhumiwa alikuwa haruhusiwi kuweka wakili wala kupewa dhamana. Hukumu za ‘mahakama’ hizi zilikuwa za mwisho kwani hakukuwa na kukata rufaa.

Madhumuni ya kufanya vile, Nyerere alisema kwamba kwa kutumia fedha walizonazo, baadhi ya watuhumiwa wangeweza kuyumbisha mahakama katika ule mfumo wa kawaida na hivyo kujihakikishia kutotiwa hatiani.

Hata hivyo, baadhi ya majaji waligoma kushiriki katika ‘mahakama’ hizo wakisema uanzishwaji wake ulikiuka Katiba ya nchi ambayo inataja waziwazi kutumia mfumo wa mahakama uliowekwa kikatiba.

Majaji, wasomi, taasisi na vyama mbali mbali walimjia juu Nyerere kuhusu mahakama hizo, kwamba ulikuwa ukiukwaji wa katiba licha ya nia yake kuwa njema ya kutaka kuonyesha uthabiti wake katika kushughulikia ufisadi, (kuliko kiongozi aliyepo sasa hivi), na hivyo kuwa tayari hata kukiuka Katiba katika azma hiyo.

Nyerere alizingatia hoja za wasomi hatimaye akasalimu amri. Alizifuta mahakama hizo baada ya mwaka mmoja tu na kesi zote ziliingizwa katika mfumo wa mahakama za kawaida, baada ya kurekebisha sheria iliyozianzisha.

Mifano hii miwili inaonyesha vitu viwili vilivyokuwapo huko nyuma: Kwanza ni jinsi vyombo vya dola, taasisi na watu wengine mashuhuri katika jamii walivyokuwa tayari kumnyooshea kidole mkuu wa nchi anapokiuka sheria, katiba au kanuni au kwenda kinyume na maadili. Pili yeye mwenyewe kuwa tayari kuwasikiliza wananchi na mara moja kubadili maamuzi yake.

Uadilifu kama huu wa Mwalimu Nyerere haupo kabisa hapa nchini. Leo rais anaingilia moja kwa moja mienendo ya mahakama katika kesi zinazosikilizwa kwa lengo la kuathiri maamuzi ya kesi hizo ili, anavyoamini yeye, kujijengea mazingira mazuri katika chama chake katika uchaguzi.

Hiyo inajionyesha alivyowatakasa mgombea ubunge wa Rombo, Basil Mramba na mshindi aliyeenguliwa Jimbo la Iringa Mjini na hatimaye kufunguliwa kesi ya rushwa, Frederick Mwakalebela.

Aidha kuna wagombea wengine wanaobeba tuhuma nzito za ufisadi, baadhi ya tuhuma hizo kuthibitishwa na Bunge nao wameambiwa na Rais Kikwete kwamba ‘hawana hatia, walisingiziwa’.

Hii ina maana ya kwamba moja kwa moja vyombo vya sheria, hususan mwendesha mashitaka mkuu wa serikali hatakiwi tena kufuatilia au kukamilisha tuhuma za jinai za hawa.

Kikwete anaonekana kuogopa kunyooshewa kidole na serikali au taasisi za nje ya nchi kuliko za humu ndani. Ndiyo maana alikwepa kumnadi Andrew Chenge, kwa mbwembwe, mgombea ubunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, ambaye tuhuma zake za ufisadi kuhusu rada zinafuatiliwa na taasisi ya serikali ya Uingereza – SFO.

Wako wapi majaji, mahakimu na wanasheria wengine? Inasikitisha sana, lakini kwa upande wa mahakama, maana ya dola ilikwisha ‘kukiri’ kwamba haina uwezo wowote wa kuingilia masuala yanayopitishwa na Bunge kwa kushirikiana na mhimili wa Utawala.

Ukiukwaji wa maadili na kanuni unaofanywa na mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete pia haukemewi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Haya ni pamoja na matumizi ya nyenzo za serikali katika kampeni.

NEC inadai kwamba ni lazima kwanza ipelekewe malalamiko rasmi ndipo inayashughulikia. Lakini Alhamisi iliyopita, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akikionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kauli iliyotoa kwamba kulikuwapo njama za kuandaa karatasi za kupiga kura za kuwezesha ushindi wa Rais Jakaya Kikwete.

Je, nani alilalamika kwa NEC? Na kama tuhuma hii ni kuhusu NEC yenyewe, mbona kuna tuhuma nyingi tu dhidi ya taasisi hiyo zinazotolewa majukwaani na wagombea mbali mbali ambazo hawataki kuzijibu?

0
No votes yet