Shibuda sasa ajifunze kwa Msabaha, Nyaruba, Anjelina


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

NIWAKUMBUSHE wasomaji mwanamama mmoja aliyejulikana kwa jina la Anjelina Levarasi a.k.a ‘Anjelina Mrema. Alivuma sana nchini.

Huyu alidaiwa kuzaa na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augsutine Mrema. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilijua fika jambo hilo, lakini ni baada tu ya Mrema kujiengua kwao.

Anjelina alitoka na kutangaza hilo hadharani na  CCM ikamdaka kuendeleza kampeni chafu hiyo kwa kumtumia ili kumvunjia staha Mrema; wakati huo akiwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Mwanamama huyo alikwenda nyumbani kwa Mrema kudai hili na lile. Alifikia hatua ya kuvua nguo zote na kubaki uchi. CCM wakachekelea.

Hata hivyo, Anjelina alifika mwisho bila kupata cha maana kutoka CCM waliomtumia. Mwishowe alikuja kufa kifo cha kusikitisha akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni bila ya msaada wowote. Waliokuwa wakimtumia hawakumsitiri.

Michael Nyaruba aliyekuwa kiongozi mwandamizi Chama cha Wananchi (CUF), ni mfano mwingine. Hakuwa mali kitu kwa CCM hadi pale alipokosana na viongozi wa CUF.

Alihamia CCM ambako alionekana lulu. Akatumiwa kuvuruga CUF. Alijinasibu kujua siri za aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF wakati huo, Seif Sharif Hamad, ambaye sasa ni katibu mkuu wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Siri alizodai kuzijua zikihusisha viongozi wa CUF zikatumika kutengeneza “kesi ya uhaini” Zanzibar.

Nyaruba alikuwa anakwenda Zanzibar kama mfalme. Akikodishiwa hadi ndege na kuandaliwa mikutano ya hadhara uwanja wa Malindi, kwa ufadhili wa iliyokuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Rais aliyepachikwa jina la Komandoo, Dk. Salmin Amour.

Siyo tu alihudumiwa usafiri na matumizi kwa safari za kwenda na kurudi Zanzibar kuandaa ushahidi dhidi ya Maalim Seif ili ashitakiwe mahakamani, bali pia alipewa ulinzi mzito.

Hakufika mbali. Aliishia tu mtu wa kutumwa na kazi yake ilipoonekana haina tena tija, akatekelezwa na CCM. Kwa kuwa angali hai, mwenyewe anaweza kueleza haya vizuri zaidi.

Mtu mwingine wa mfano huo ni Salum Msabaha Mbarouk, kijana aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, jimbo la zamani la Mkunazini, kupitia CUF.

Wapinzani wa CUF walipofanikiwa kumlaghai, alidai ametekwa katika tukio ambalo halijawahi kuelezwa bayana mpaka leo. Alidai amefichwa kusikojulikana na mara moja akamtaja aliyekuwa mwanasheria mkuu wa SMZ, Idi Pandu akidai kuwa alihusika.

Wakati huo alishatangaza kujiuzulu uwakilishi. Hapo CCM ikaona imepata. Ilimtumia Msabaha ili kuidhoofisha CUF. Hatimaye alijiunga na CCM ili maisha yaendelee kwa kuwa jamii ilianza kumchukulia ni msaliti.

Watatu hao wanatosha kuonyesha kuwa CCM ina jadi ya kutafuta watu wa kudhoofisha nguvu za upinzani, lakini baadaye hukwama huku wakikosa walichokitarajia.

Ninahofu John Shibuda, Mbunge wa Maswa Mashariki (CHADEMA), anataka kufuata mkondo huo; labda kwa kujua au kutokujua.

Shibuda ambaye alikuwa mbunge kupitia CCM kabla ya kuhama wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 na kugombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), pengine hatumwi ila baadhi ya kauli zake zinatia shaka.

Semina ya wakuu wa wilaya na mikoa iliyokuwa mjini Dodoma ikisimamiwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye alitoa mada, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi wengine waandamizi na wataalam kadhaa na wastaafu, iliendeshwa chini ya usiri mkubwa.

Hakuna ruhusa vyombo vya habari kushuhudia mijadala ya mada zinazowasilishwa. Kikubwa kinachotolewa kwa umma ni maamuzi ya maofisa wa habari wa ama Ofisi ya Rais, Ikulu au Ofisi ya Waziri Mkuu.

Lakini, pamoja na kuendesha semina hiyo ya siku 10 kwa mbinu ya kufunika habari, taarifa moja ilitolewa rasmi ikimhusu Shibuda na kauli aliyoielekeza kwa Rais Kikwete.

Akihutubia semina kuhusu ripoti ya Mpango wa Kujitathmini kwa Utawala Bora Bara la Afrika (ARPM), Shibuda alifikia kutukana vyama vya upinzani kwa kuvifananisha na ‘chokoraa.’ Anasema vyama hivyo ni kama mtoto wa mitaani aliyekosa malezi ya baba na mama.

Hiyo ndiyo kambi ya upinzani kwa upeo wake, kambi ambayo Shibuda anatamani mwaka 2015 imsaidie kuwania urais.

CCM kwa kuwa wanamjua Shibuka ni ndege asiyefugika, waliacha vyombo vya habari viwepo wakati akizungumza kwa kuwa walijua ataridhia “kutoboa ngalawa yake mwenyewe.” Muhimu kwake ni kushangiliwa na makada wa CCM.

Shibuda anafanya haya yote akidhani anajijenga; akiamini ana nguvu katika CHADEMA. Anafanya haya kwa kuwa anajiona ni “jabali” la siasa za Tanzania.

Alichosahau haraka ni tabia ya wanyama kushuhudia mwenzao analiwa bila ya kuchukua hatua kumhami huku wasijue adui akimaliza anawafuata wao ili kuongeza shibe.

Inawezekana Shibuda anafikiri si rahisi kutumiwa na CCM kujitafuna mwenyewe, lakini ajue anachofanya hakitofautiani na walichokifanya kina Anjelina, Msabaha, Nyaruba na wengine. Mwisho wameishia kubaya.

Shibuda anasahau haraka sana kuwa CCM hiihii anayoshabikia na kutukuza leo, ilimkataa miaka na miaka. Ilimkataa mara mbili asiwe Mwenyekiti wa Wazazi. Akumbuke rufani yake ilifikia wapi katika kupinga ushindi wa Iddi Simba katika nafasi hiyo? Zile zilikuwa zama za katibu mkuu Philip Mangula.

Shibuda ajiulize ni nani aliyeshushwa kwenye treni akitokea Mwanza kwenda Dodoma kuhudhuria mkutano mkuu wa CCM wa uchaguzi?

Shibuda ajiulize kwa nini CCM mwaka 2010 ilimtosa asigombee ubunge Maswa Mashariki, hata akafanyiwa zengwe asipige kampeni kwenye jimbo lake.

Je, leo CCM wameona Shibuda amebadilika; amekuwa mpya; amepakwa sukari na asali kiasi cha kumpenda? Sasa wanakumbatia na kumpa uwanja katika mkutano ili ajifarague mbele ya vyombo vya habari?

Shibuda anaamini amepata uwanja wa kujivuna na kupaka matope CHADEMA – chama kilichompa ubunge.

Je, anadhani atakuwa salama ndani ya CCM alikoishi kama mtoto wa kambo asiyependeka, licha ya kukisifu chama hicho kuwa kinajua kulea?

Shibuda arudishe kumbukumbu. Azingatie  yaliyowafika kina Anjelina, Msabaha na Nyaruba. Huenda akajifunza mawili, matatu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: