Shuhuda wa ajali ya meli anena


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

ALIYENUSURIKA kwenye ajali ya meli Zanzibar anasema meli ilikuwa na abiria wengi kuliko waliotajwa na serikali.

Mbezi Wilbard Bilungi, anasema “waliokuwa katika meli ile, hasa deki mbili za chini, ni wengi kuliko wale waliookolewa na wale walioopolewa wakiwa wamekufa.” Hataji idadi kamili ya waliokuwemo.

Ajali ya meli ya mv. Spice Islander ilitokea katika mkondo mkuu wa bahari wa Nungwi, visiwani Zanzibar wiki mbili zilizopita.

“Kule chini walikuwa wamekaa wanawake wengi, watoto na wazee ambao bila shaka yeyote watakuwa wamekufa kutokana na kushindwa kuokolewa kujiokoa au kuokolewa,” anaeleza Bilungi.

Anasema hali hiyo ilisababishwa na hatua ya wafanyakazi wa meli hiyo kufunga mlango wa chini ambako maelfu ya abiria walikuwa wamekaa katika jitihada zao za kujiokoa.

Hadi shughuli za uokoaji zinasitishwa Alhamisi iliyopita, serikali ilikuwa imetangaza watu 203 kupoteza maisha na wengine zaidi 619 kuokolewa.

Maelezo ya Bilungi yanashabihiana na madai yaliyotolewa na mbunge wa Ziwani, kisiwani Pemba, Ahmed Juma Ngwali, kwamba waliokufa katika ajali hiyo ni 1,721 ambao ni kutoka mikoa miwili ya Kaskazini na Kusini.

Ngwali amesema kwa mujibu wa uhakiki uliofanywa nyumba kwa nyumba visiwani humo, zaidi ya watu 1,700 hawajulikani walipo; lakini inafahamika kuwa walikuwa kwenye meli hiyo.

Idadi hiyo ni nje ya abiria 203 waliopatikana wamekufa na nje ya abiria ambao wanatoka nje ya kisiwa cha Pemba.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, ambayo yamechapishwa kwa ukamilifu katika toleo hili, Bilungi anasema, “Watu wengi waliofanikiwa kujiokoa ni wale waliojirusha kwenye maji.”

Bilungi anasema alishuhudia, kwa macho yake, wafanyakazi wa meli wakifunga mlango wa kwenda chini wakati wao wakihangaika kujiokoa.

Tayari serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeunda tume kuchunguza kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo. Hata hivyo, duru huru za uchunguzi zinasema kuzama kwa meli ya mv. Spice Islander kumetokana na kuzidiwa uzito kulikotokana na wingi wa abiria na mizigo, pamoja na uchakavu.

Meli ya mv. Spice Islander ilitengenezwa nchini Ugiriki mwaka 1967 ambapo ilipewa jina la Mariana; mwaka 1988 iliuzwa na kupewa jina la Apostolos na mwaka 2007 ikauzwa tena kwa kampuni ya Honduras, ya nchini Marekani Kusini na kupewa jina la sasa la mv Spice Islander.

Kwa sasa, ni mali ya kampuni ya Visiwani Shiping Ltd., inayomilikiwa na baadhi ya vigogo waandamizi ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinasema wengi wa vigogo hao wamemilikisha hisa zao kwa ndugu zao au marafiki wa karibu.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)