Shy-Rose Bhanji atafuta ubunge kwa misamiati


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Asema mwaka 2010 ubunge unahitaji tafsiri mpya
Abainisha umuhimu wa ofisi kila kata jimboni
Shy-Rose Sadruddin Bhanji

NI mwandishi wa habari mzoefu aliyeingia katika nyanya ya uongozi wa mashirika makubwa. Ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sasa anataka kuingia ndani ya siasa za vyama.

Shy-Rose Sadruddin Bhanji ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano cha Benki ya NMB, amechukua fomu kutafuta ubunge na ametangaza kugombea jimbo la Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

Amekuwa kiongozi wa ngazi za chini wa CCM na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UV-CCM), amekuwa miongoni mwa wana-CCM wa kwanza kuchukua fomu ofisi za wilaya kwa ajili ya kuomba uteuzi wa kugombea ubunge majimboni.

Uchukuaji wa fomu za kuomba kugombea ubunge na udiwani ulianza Jumatatu kwa CCM. Watu kadhaa walichukua fomu kuwania uteuzi huo jimbo la Kinondoni ambalo mbunge anayemaliza, Iddi Azzan naye amechukua fomu kutetea nafasi hiyo.

Shy-Rose anasema kwa mtazamo wake nafasi ya ubunge inahitaji tafsiri mpya mwaka huu, kwa vile “kwa sasa mbunge anatakiwa kuwa ni kiungo cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo.”

“Mwaka 2010 ni mwaka wa mabadiliko na ndio maana nimeona kwamba ili kila mwananchi kuwajibika, nafasi ya mbunge inahitaji kutafsiriwa upya ili iendane na wakati na matatizo yanayokakabili wananchi,” amesema katika mahojiano na MwanaHALISI, yaliyofanyika mara baada ya hatua yake hiyo.

Aonavyo yeye, hata sifa za mbunge zinahitaji kutafsiriwa upya, kwani majukumu yake yamebadilika kulingana na wakati. Ametaja baadhi ya sifa hizo mpya kuwa ni mhamasishaji, kiungo muhimu, kufanya kazi usiku na mchana na kuwa na ofisi katika kila kata ndani ya jimbo husika ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.

“Naomba nitoe tafsiri mpya ya neno ubunge. Mbunge sasa anatakiwa awe ni kiungo muhimu kati ya walio na kipato kikubwa, kipato cha kati na wasio na kipato ili kwa pamoja jimbo liweze kupata maendeleo.

“Mimi nitahakikisha kwamba nina ofisi katika kila kata ili niweze kuwafikia wananchi katika kata zote kwani wakati napita kuomba kura ninawafuata na baada ya kufanikiwa kutimiza azma yangu ni wakati wa kuendelea kuwafuata na siyo wao wanifuate,” anasema.

Shy-Rose amesema sera yake kubwa akiwa mbunge itakuwa ni kumshirikisha kila mwananchi jimboni katika shughuli za kuleta maendeleo ili kila mtu atumie fursa ya haki ya kutoa maoni na mchango wa hali na mali katika kuleta maendeleo ya ukweli.

Amesema hata mwananchi ambaye atakuwa hana uwezo wa kipato, atabeba tofali kutoka upande mmoja hadi sehemu husika.

“Nimeamua kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo hili ili niweze kuleta mageuzi makubwa katika jimbo letu… naomba mfahamu kwamba kila mwananchi amebarikiwa akili, vipaji, uwezo na Mwenyezi Mungu lakini asiposhirikishwa hataweza kutoa mchango wake. Mimi nitahakikisha kila mmoja kwa uwezo wake na nafasi yake anachangia katika kuleta maendeleo,” anasema.

Kuna mambo ambayo Shy-Rose atayapigania. Anataja elimu, afya, ajira kwa vijana, kupiga vita utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana, haki za wasanii, kusaidia wajane katika kujikwamua kiuchumi na kuleta msukumo mpya katika masuala ya mahusiano na jamii eneo analosema linahitaji msukumo mpya.

Shy-Rose amesema kutokana na uzoefu wa kazi zake tangu akiwa mwandishi wa habari, mtangazaji na meneja uhusiano sehemu alizofanyia kazi, anaamini amekuwa mwanafunzi mzuri katika kutambua matatizo yanayoikabili nchi nzima na hususan jimbo la Kinondoni.

“Kwa kuzingatia uzoefu wangu ndani ya jamii na baada ya kufikiria namna nitakavyotumia akili, elimu, uwezo, busara na vipaji vingi nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu na nafasi yangu katika jamii, ndio maana nimeamua kujitosa kuomba kuteuliwa kugombea ubunge,” anasema.

Anajinasibu kuwa amefanya tathmini ya kutosha; amejiuliza maswali mengi na kuomba ushauri kwa viongozi wa chama, familia yake, rafiki zake na wanachama wenzake katika chama.

Kwa namna ya pekee, anasema amefarijika kwa vile walivyompa hamasa alipowaeleza kuwa anakusudia kuomba chama kimteue kugombea ubunge.

Shy-Rose amesema ana kila sifa kwani amekulia kwenye chama tangu akiwa Umoja wa Vijana (UV-CCM), tanuri la kupika vijana wa kushika nafasi za uongozi na hatimaye kuingia ndani kabisa ya chama.

“Mkiangalia wasifu wangu mtaona haya ninayoyasema. Mimi sijapitia tu katika chama, nimetokea ndani ya UV-CCM, nimezunguka na viongozi mbalimbali wa chama na serikali nchi nzima na nimejifunza mengi kuhusu utumishi kwa jamii, na jinsi sera na ilani ya chama inavyofanya kazi za kila siku,” anasema.

Lakini pia Shy-Rose anamtaja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwamba amemsukuma katika kuomba ubunge. Anasema kauli ya rais kutaka wanawake wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, imemvutia na ameamua kuitekeleza kwa vitendo.

“Rais Kikwete anahimiza wanawake tujitokeze kugombea uongozi ili uwakilishi wetu katika vyombo vya maamuzi ufikie asilimia 50. Uamuzi wangu ni kutekeleza maelekezo ya rais kikwete,” anasema.

Sababu nyingine ya kuingia kuomba nafasi hii, anasema ni kuonyesha mfano vijana wenzake ambao wanapenda siasa lakini wametawaliwa na woga. “Wanaogopa kugombea majimboni. Nataka niwe mfano kwao. Kuingia kwangu kutawatia moyo vijana na wanawake wengine kuingia mwaka 2015,” anasema.

Shy-Rose ameingia kinyang’anyiro hicho ndani ya ushindani mkali kwani wanachama kadhaa nao wamechukua fomu kuwania uteuzi wa nafasi hiyohiyo Kinondoni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: